· Maelfu ya wananchi wanufaika na elimu ya sheria
· Takwimu yaonesha kupungua kwa migogoro ya ardhi
· Mawakili vishoka kushughulikiwa
Na EVELINA ODEMBA – Mahakama, Morogoro
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga amesema kuwa jumla ya watu 23,310 wamefikiwa na kupewa elimu ya sheria na haki mbalimbali katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa Kanda ya Morogoro.
Mhe. Magoiga aliyasema hayo katika sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini jana tarahe 03 Februari,2025 ambako kwa Kanda ya Morogoro zilifanyika katika Viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki na kuhudhuliwa na wageni mbalimbali, wakiwemo Viongozi wa Serikali Mkoa na Wilaya, Wadau, Watumishi wa Mahakama na Wananchi.
Kaimu Jaji Mfawidhi alitoa takwimu kuwa miongoni mwa walionufaika na elimu hiyo, wanawake walikuwa 6,790, wanaume 6,234 na watoto ambao ni wanafunzi walikuwa 10,106. Alifafanua kuwa idadi hiyo haihusishi elimu iliyotolewa kupitia Vyombo vya Habari ambavyo vilitumika pia kutoa elimu ya sheria ndani ya kipindi chote cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
“Ukisifia mianzi kumbuka na aliyeipanda, natoa pongezi kubwa kwa Wadau wote wa Mahakama ambao wameshiriki kwenye utoaji wa elimu kwa umma katika Wilaya zote za Mkoa wa Morogoro, ninyi ni chachu ya kweli ya mafanikio haya makubwa tunayojivunia,” alisema Mhe Magoiga na kuitimisha kwa kuwashukuru wananchi wa Morogoro kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na hata kufika kwenye siku ya kilele.
Akitoa salamu za Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima ambaye alikuwa mgeni maalum, alitoa pongezi kwa Mahakama Kanda ya Morogoro kwa kazi nzuri wanayoifanya, huku akimwagia sifa utoaji wa elimu kwa jamii ambao kwa kiasi kikubwa umepunguza migogoro ya ardhi.
Mhe. Malima aliongeza kuwa kwa sasa migogoro mikubwa iliyokuwa ikiikabili Morogoro ilikuwa ni ile ya wakulima na wafugaji ambayo kwa sasa haipo tena. Alisema ni jambo la kupongeza kwa kuwa Serikali na Mahakama, kwa kushirikiana na Wadau, ndio chanzo cha kumalizika kwa migogoro hiyo.
“Kimsingi, Wananchi hawasemi Serikali ndio imemaliza haya yote peke yake isipokuwa sisi sote kwa pamoja, kuna kesi nyingine tukiwaletea mahakamani na Mahakama ikatoa adhabu stahili, watu wanapungukiwa hamasa ya kufanya uharibifu kwa wenzao, hivyo nawapongeza sana Mahakama, Wadau na Viongozi wa Serikari kwa umoja wetu tumeyatatua haya,” alihitimisha Mkuu wa Mkoa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS), Kanda ya Morogoro, Mhe. Baraka Rweka, akitoa salamu za chama alisema kuwa wanaungana na Mahakama katika siku hiyo muhimu inayoashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama.
Alitoa pongezi kwa Mawakili wote walioshiriki Wiki ya Sheria katika Wilaya zote za Morogoro, ikiwemo Malinyi, Ulanga, Kilombero, Kilosa, Mvomero, Gairo na Manispaa ya Morogoro.
Sherehe hiyo iliyoanza kwa dua toka madehebu mbalimbali ambazo waliiombea Mahakama katika kutekeleza majukumu yake ilihudhuliwa na Viongozi mbalimbalimbali akiwemo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, Viongozi wa dini, Viongozi Mahakama Kanda ya Morogoro, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, wadau wa Mahakama, Watumishi na Wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima akizungumza wakati wa kilele cha Siku ya Sheria nchini, nyuma yake ni Meza Kuu ikifuatilia yaliyokuwa yanayojiri.
Dua maalumu kuiombea Mahakama ikifanyika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni