Na CHRISTOPHER MSAGATI-Mahakama, Manyara
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Rugalema
Kahyoza amewasisitiza wananchi na wadau wa Mahakama kuelimishana na kuwa na jamii
yenye maadili na tabia njema ikiwa wanataka kuwa na Nchi yenye maendeleo
kiuchumi, kisisasa na hata kijamii ifikapo Mwaka 2050.
Mhe
Jaji Kahyoza ameyaeleza hayo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria
Nchini kwa Mwaka 2025 jana tarehe 03 Februari, 2025 katika sherehe zilizofanyika
katika viwanja vya Mahakama Kuu Manyara.
‘‘Ni
kweli Serikali na Taifa kwa ujumla wetu tunatamani sana kuona kuwa tuna nchi
yenye Uchumi unaokuwa na wenye tija na faida kwa kila mtu. Haya yote
hayatawezekana endapo tutakuwa tuna taifa lenye watu wasiokuwa na maadili
katika jamii. Mkoa wa Manyara umekuwa na
changamoto ya makosa mengi ya ukatili wa kijinsia kama vile Ubakaji na Ulawiti,
sasa taifa haliwezi kufika mbali kimaendeleo kama hatutaacha tabia hizi’’
amesema Mhe. Kahyoza.
Akizungumzia
Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Mhe. Kahyoza alisema kuwa Mahakama ya Tanzania
imeunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha matumizi makubwa ya TEHAMA
katika shughuli zake na kuwezesha upatikanaji wa Haki kwa Wakati.
“TEHAMA
imetuwezesha sana kusikiliza mashauri yetu kwa wakati na hata kuyatolea maamuzi
kwa wakati, taarifa mbalimbali zinazohusu Mahakama pia zinapatikana kwa njia ya
mtandao. Kimsingi jitihada hizi zote zinalenga kuwezesha Taifa letu kuwa na
mazingira wezeshi ya Utoaji Haki ulio thabiti ambao pia unawahamasisha
wawekezaji wa ndani na Nje ya Nchi kufanya mambo yao kwa utulivu pasipo kuwa na
usumbufu wowote na jambo hili litafanya taifa letu kuwa na maendeleo
tuyatakayo”. alisema Mhe Kahyoza
Naye,
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, ameishukuru Mahakama kwa
utaratibu wa Wiki ya Sheria na kutoa mfano wa namna walivyoweza kutoa elimu
katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Manyara katika wiki nzima. Pia alitoa wito
kwa Mahakama na wadau wake kuendelea kutoa elimu zaidi ya masuala mbalimbali ya
kisheria kwa jamii, jambo litakalo saidia kupunguza malalamiko mengi ambayo
yanatokana na uelewa mdogo wa sheria.
“Mahakama
imejitahidi sana kutoa elimu kwa wananchi katika kipindi hiki. Nimeweza kufanya
ziara katika Wilaya za Mbulu, Kiteto na Simanjiro na katika meneo yote
nimefurahi kuona jinsi mlivyojipanga kuwaelimisha wananchi wa Mkoa wa Manyara.
Niwaombe suala hili liwe endelevu kwani kwa kiasi kikubwa litapunguza malalamiko
na moigogoro katika jamii”. alisema Mhe. Sendiga.
Mahakama
Kuu Kanda ya Manyara, kama zilivyo Mahakama katika Kanda nyingine nchini
imehitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Nchini kwa Mwaka 2025 ambayo yalianza
rasmi mnamo tarehe 25 Januari, 2025 na kuhitimishwa jana tarehe 03 Februari, 2025
kukiwa na mafanikio makubwa ya kumaliza asilimia 97% ya mashauri
yaliyofunguliwa mnamo mwaka 2024 kwa upande wa Mahakama Kuu na pia kutokuwa na
mashauri yaliyozidi miezi mitatu kwa upande wa Mahakama za Mwanzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Rugalema Kahyoza akihutubia wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama siku kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini Mahakama Kuu Manyara.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga akiwahutubia wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama katika sherehe za maadhimisho hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni