Jumanne, 4 Februari 2025

KIGOMA YASHEREHEKEA SIKU YA SHERIA NCHINI

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Agustine Karichuba Rwizile ameongoza watumishi na wadau wa Mahakama mkoani humo kusherehekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viunga vya Mahakama hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo jana tarehe 03 Februari, 2025, Mhe. Rwizile alitoa rai kwa Taasisi za Haki Madai kuwa na malengo yanayoendana na kasi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa katika kuimarisha mifumo mbalimbali inayorahisisha utendaji kazi wa Mahakama.

“Taasisi zote za haki madai lazima zijipime ili kwenda pamoja na Taasisi za haki madai kwani nanyi mnatakiwa kuboresha na kujiimarisha katika mifumo hiyo ili kufikia kiwango cha ukomo wa usikilizwaji wa mashauri kwa Mahakama Kuu yaani miezi 12 na Mahakama za Wilaya miezi sita hii italeta uwajibikaji katika taasisi za haki madai,” alisema Jaji Rwizile.

Mhe. Rwizile alisema kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, iliyoanza mwaka 2000 ilikuwa na lengo la kuinua nchi kufikia uchumi wa kati kupitia kilimo cha kisasa, mageuzi ya viwanda, ujenzi wa miundombinu na teknolojia, na Dira ya 2050 nayo inalenga kuiondoa Nchi hatika uchumi wa kati na kufika kwenye uchumi wa juu. Ameongeza kwa kusema kwamba, “Dira hiyo ina nguzo sita ikiwemo ulinzi wa haki za kibinadamu kwa maana kila mtu ana haki ya kusimamia uhuru na kulindwa mpaka 2025 kwa mujibu wa Katiba.”

Aidha, Mhe. Rwizile alitumia jukwaa hilo kutoa historia fupi ya Siku ya Sheria nchini, ambapo alieleza kuwa, ilianza kuadhimishwa tangu tarehe 01 Machi, 1996 na katika kipindi hicho ilikuwa ni kwa ajili ya kuanza kusikiliza mashauri yaliyotokana na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995.

Kwa upande wa Wakili wa Serikali, Bw. George Kalenda alisema kuwa, Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu isemayo ‘Tanzania ya mwaka 2050: nafasi ya taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya dira ya Taifa ya Maendeleo’’ inazitaka Taasisi zinazosimamia haki kimadai kujipanga kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kushirikiana kwa pamoja ili kuisaidia Mahakama kutenda haki.

“Tunatakiwa kuwajibika katika shughuli zetu za kila ili kufikia malengo yetu jumuishi katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,” alisema Bw. Kalenda.

Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea, Bw. Eliutha Kivyiro alisema kuwa, malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, ni pamoja na kukuza taifa jumuishi lenye ustawi wa haki na linalojitegemea, hivyo, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ni Taasisi muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo yam waka 2050.

Aliongeza kuwa, ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ameshauri kuimarisha uwezo wa Wanataaluma na taasisi katika utatuzi wa migogoro kwa njia zote ikiwemo usuluhishi, utoaji endelevu wa huduma za msaada wa kisheria. Ameongeza kuwa,  TLS ina mchango mkubwa katika kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ambao wanashindwa kumudu gharama za huduma ya kisheria.

Wadau waliohudhuria Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini, ni pamoja na Watumishi wa Kanda hiyo, Mawakili wa Serikali, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Viongozi wa Dini, Wakuu wa Taasisi za Umma, Chuo cha Mafunzo Kigoma (KTC), Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole,  Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kigoma, wananchi kutoka sehemu mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma, Ubalozi mdogo wa Burundi na Kongo na wengine.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya  kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa mwaka 2025 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kigoma jana tarehe 03 Februari, 2025.

Wakili Mkuu wa Serikali Mfawidhi, Bw. George Kalenda akisoma risala katika hafla ya kilele ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika mapema jana tarehe 03 Februari, 2025 katika viunga vya  Mahakama Kuu Kigoma.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS), Bw. Eliutha Kivyiro akisoma risala wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viunga vya Mahakama Kuu kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akipokea salamu kutoka kwa kikosi maalum cha Askari wa (FFU) (hawapo katika picha) wakati wa sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa shughuli za Mahakama kwa mwaka huu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, akikabidhi cheti cha pongezi  kwa Bi. Nyakolema Mwita, Mwakilishi kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakiwa moja ya wadau  waliojitokeza kushirikiana na Mahakama kutoa elimu kwa umma wakati wa Wiki ya Sheria, 2025. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma,  Mhe. Aristida Tarimo (wa kwanza kushoto) akiwa na Mahakimu wengine wa Mahakama mbalimbali za mkoani humo katika sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika jana tarehe 03 Februari, 2025.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni