Jumanne, 4 Februari 2025

MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA YATOA MSAADA KWA WAFUNGWA NA MAHABUSU

CHARLES NGUSA- Mahakama, Geita


Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita leo tarehe 31 Januari, 2025 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali mkoani Geita wameungana pamoja katika kuendeleza Maadhimisho ya Wiki ya Sheria ambayo ilizinduliwa mnamo tarehe 25 Januari,2025 kwa kutoa msaada wa magodoro na vitu mbalimbali.

 

Vitu vingine vilivyotolewa ni  sabuni,dawa za meno,miswaki pamoja na taulo za kike kwa wafungwa na mahabusu katika magereza ya Chato na Geita. 

 

Akizungumza baada ya kuwasili katika Gereza la Chato, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina amesema kuwa katika ku aadhimisha siku hiyo, pamoja na mambo mengine yanayoendelea kufanyika wameona ni vyema kutoa msaada kwa wafungwa na mahabusu hao, kwa sababu  wakati wa ukaguzi uliopita waligundua kuna changamoto kubwa ya upungufu wa magodoro katika magereza yote, iIi kuwasaidia wafungwa na mahabusu wapate mahali pazuri pa kulala.

 

“Katika Wiki ya Sheria huwa tunatoa elimu pamoja na misaada, hivyo dhumuni la ujio wa leo ni kuja kuwaletea msaada wa magodoro pamoja na vitu vingine tulivyokuja navyo kama vile sabuni, miswaki na dawa za miswaki, hivyo wadau wote tulioambatana hapa tumeleta magodoro 82 ambayo yametokana na michango yao,” Mhe.Mhina amesema.

 

Kwa upande wake Bwana Mwita Marwa Nyakorema(Mfungwa katika gereza la Chato) akizungumza kwa niaba ya wafungwa na mahabusu katika gereza la Chato amesema kuwa wanashukuru  kwa msaada walioupata kwani kulikuwa na changamoto kubwa sya magodoro, hivyo anawaomba pia wadau wengine waweze kuwasaidia kama walivyofanya Mahakama na wadau wake.

 

Kwa niaba ya wenzangu, nashukuru sana kwa kutuletea msaada huu kwani tulikuwa na changamoto kubwa sana ya magodoro hivyo ujio wa haya magodoro umekuwa msaada mkubwa mno,ombi langu kwa wadau wengine,tunayo changamoto kubwa sana ya masufuria ya kupikia kwa kuwa haya tuliyonayo hayaendani na nishati tunayotumia kwa sasa ambayo ni makaa ya mawe hivyo yanaweza kubomoka muda wowote kwa kuwa yalikuwa yanaendana na nishati ya kuni,” amesema Mwita.

 

Naye Mkuu wa Gereza la Chato, SSP Anthony Mashauri, akizungumza baada ya kupokea msaada huo amesema kuwa walikuwa na upungufu wa magodoro 180, hivyo kupata msaada huo wa magodoro 82 ni msaada mkubwa mno kwa kuwa imepunguza changamoto yao.

 

Baada ya kuwasili katika Gereza la Wilaya ya Geita, Mkuu wa Gereza la Geita, SSP Jovin Bujwina amewashukuru Mahakama na wadau wote walioshiriki katika kutoa msaada huo wa magodoro na vitu hivyo vingine kwani vitasaidia sana katika kuondoa changamoto hiyo. 

 

“Nawashukuru sana Mahakama kwanza kwa kutuletea msaada wa magodoro, lakini pili kwa kutuondolea msongamano wa wafungwa na mahabusu gerezani kwetu , kwani kwa sasa gereza letu halina tena msongamano kama ilivyokuwa hapo awali, uwezo wa gereza letu ni wafungwa 401 lakini kwa leo tunatarajia kulala na wafungwa na mahabusu 311 tu,” amesema Bujwina.

 

Jumla ya magodoro 165 pamoja na vitu mbalimbali vyenye jumla ya Tsh 5,806,000 vilivyopatikana kutokana na michango ya watumishi wa Mahakama na wadau wake mbalimbali viligawiwa katika Magereza ya Chato na Geita.

                                                                                                                                                    

                                                                                                                                                         

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina(wa pili kushoto) akiwa pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita Mhe. Griffin Mwakapeje (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali walipokuwa katika Gereza la Wilaya Chato wakikabidhi msaada wa magodoro kwa Mkuu wa Gereza la Chato. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita,Mhe. Kevin David Mhina(wa nne kushoto) akiwa pamoja na watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali walipowasili katika Gereza la Wilaya Geita na kukabidhi msaada wa magodoro kwa Mkuu wa Gereza Wilaya ya Geita.


(Habari hii imehaririwa na MAGRETH KINABO-Mahakama, Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni