Jumatano, 5 Februari 2025

HAKI INAYOPATIKANA KWA WAKATI INAPUNGUZA MIGOGORO; JAJI MUGETA

Na SETH KAZIMOTO -Mahakama Kanda-Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Claud Mugeta amesema kuwa haki inayopatikana kwa wakati inapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro katika jamii kwani huachilia rasilimali zilizofungwa katika migogoro na kuziruhusu kuingia katika mnyororo wa uzalishaji mali na hatimaye kuwezesha ukuaji wa uchumi. 

Mhe. Mugeta aliyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha ambapo yeye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.

Mhe. Mugeta alibainisha kwamba, katika kuhakikisha Mahakama mkoani Arusha inamaliza migogoro kwa vitendo, inalenga kusikiliza na kuamua mashauri kwa muda mfupi zaidi kuliko ule uliopangwa ambapo alisema, “Mahakama Kanda ya Arusha inalenga kusikiliza na kuamua mashauri katika Mahakama za Mwanzo kwa kipindi cha miezi mitatu tu, Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi kwa miezi sita tu na Mahakama Kuu kwa miezi 12 tu.”

Alisema kuwa, mpango huo ya kuamua mashauri kwa wakati ni kutokana na ukweli kwamba haki inayotolewa kwa wakati inapunguza migogoro na kuruhusu rasilimali kuingia katika mnyororo wa uzalishaji mali.

Pia, Mgeni rasmi amehimiza matumizi ya usuluhishi katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kutatua migogoro mapema zaidi na kwa njia ambayo haithiri mahusiano ya wadaawa na hivyo kusaidia kujenga jamii yenye amani na kusisitiza juu ya matumizi ya mifumo mbalimbali kuanzia ngazi ya familia hadi Mahakama kuhakikisha kuwa migogoro inayoweza kutatuliwa kwa usuluhishi itatuliwe kwa njia hiyo.

Aidha, amezitaka Taasisi za Haki Madai kuhakikisha zinashirikiana na kutekeleza wajibu wao kwa wakati kwani kazi ya Taasisi moja ni malighafi ya Taasisi nyingine ili iweze kutekeleza wajibu wake, hivyo Taasisi moja inapozembea kutimiza wajibu wake inasababisha Taasisi nyingine kushindwa kufanya kazi zake na hatimaye kusababisha ongezeko la migogoro katika jamii na kuongeza umaskini kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika maelezo yake ya utangulizi, Mhe. Mugeta alisema kuwa, Wiki ya Sheria ilihitimishwa rasmi tarehe 01 Februari, 2025 ambapo katika kipindi hicho wananchi wengi walipatiwa elimu na msaada wa kisheria bure na kufahamishwa juu ya shughuli mbalimbali za utoaji haki zinazotolewa na wadau wa haki waliokusanyika pamoja katika maonesho yaliyofanyika katika viwanja vya Wakala wa Nyumba (TBA) jijini Arusha.

Mhe. Mugeta aliongeza kwa kusema kuwa, Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inataka ifikapo mwaka 2050, tuwe Taifa moja kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa na jamii inayothamini utu, haki, uhuru na demokrasia ikiwa ni pamoja na kuwa na Taifa ambalo linasimamia kwa ubora rasilimali za nchi na kuimarisha utamaduni na tunu za Taifa.

Aliongeza kuwa, ili kuyafikia malengo hayo Sekta mbalimbali hususani taasisi za Haki Madai ambazo zitahusika katika eneo la Utawala bora, Haki Jinai, Uhuru na Demokrasia ambapo ufanisi wa eneo hilo utapimwa kwa kutazama mwenendo wa Utawala wa Sheria nchini, Haki za binadamu, usawa mbele ya sheria na uwajibikaji  wa Taasisi za Utoaji Haki Madai kwa wananchi ili kufikia jamii isiyokuwa na vurugu wala ukatili.

“Ukimuuliza mwananchi wa kawaida kwamba anataka nini, atakujibu anataka huduma bora, ya haraka na kwa heshima” alisema Mhe. Mugeta huku akisisitiza kuwa, katika miaka 25 ijayo lazima kujiuliza tutakidhi vipi matarajio ya wananchi. 

Alisema, ili kujibu matarajio ya wananchi katika miaka 25 ijayo, lazima kufanyika mageuzi katika utekelezaji wa majukumu ya kila Taasisi na utekelezaji huo wa uzingatie sheria, kanuni na taratibu.

Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria nchini yalikuwa na Kauli Mbiu isemayo “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

Hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini Kanda ya Arusha yalihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Majaji Wastaafu, Mhe. Januari Msoffe, Mhe. Kakusulo Sambo, Mhe. Aishael Sumari na Mhe. Aisha Nyerere, wengine ni watumishi wa Mahakama, Viongozi wa Dini, Serikali na Taasisi mbalimbali, wadau na wananchi. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Claud Mugeta akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Claud Mugeta akikagua gwaride kuashiria uzinduzi wa mwaka mpya wa Mahakama wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 03 Februari 2025 katika viwanja vya  Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wastaafu (waliosimama). Walioketi ni Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, wa kwanza kushoto ni Mhe. Dkt. Dafina Ndumbaro, wa pili kushoto ni Mhe. Ayoub Mwenda, wa pili kulia ni Mhe. Aisha Bade na wa Mhe. Sylvester Kainda wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha utoaji Haki (IJC) Arusha.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 03 Februari, 2025.

Picha za matukio mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria mkoani Arusha tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni