Na INNOCENT KANSHA- Mahakama, Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt.
Juliana Masabo leo tarehe 04 Februari, 2025
amefungua mafunzo ya kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa
kingono (Avoiding re-traumatization of victims and witnesses of sexual and gender-based
violance) mafunzo hayo yanatolewa kwa Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka na
Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mafunzo
hayo yanayofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) jijini Dodoma
yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama - Lushoto (IJA) kwa kushirikiana
na Taasisi ya Kimataifa ya Irish Rule of Law International (IRLI) chini ya
ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
“Leo
tumekutana hapa Maafisa Mahakama, Waendesha Mashtaka na Maafisa ustawi wa Jamii
kujifunza, kujadili kwa umoja wetu na kuchangia uzoefu wetu wa namna ya
kukabiliana na aina hii ya mashauri kwa uangalifu, ufanisi mkubwa na weledi wa
hali ya juu,” amesisitiza Mhe. Dkt. Masabo.
Aidha,
Mhe. Dkt. Masabo ameishukuru Irish Rule of Law International (IRLI) katika kufanikisha mafunzo hayo pamoja na juhudi
zao za kudumisha utawala wa Sheria, bila kuwasahau IJA pamoja na Mahakama ya
Tanzania kupitia Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyebariki
kufanyika kwa mafunzo hayo.
“Kazi
yetu kubwa leo ni kuhakikisha tunatoka na mbinu wezeshi na rafiki za kuhakikisha
waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia na kingono wanahudumiwa kwa kuzingatia
utu, nidhamu na heshima ili kuondoa na kuepuka kutonesha majeraha ya waathirika
wa ukatili huo,” amesema Jaji Masabo.
Mhe.
Dkt. Masabo ameongeza kuwa, watu wengine huwaita waathirika ama walionusurika
kwenye vitendo vya unyanyasaji ila majina hayo yote hayajalishi bali ni jukumu
lenu la msingi pale mtapokutana na waathirika hao mfanye nao kazi ili kuhakikisha wanahudumiwa
kwa kuzingatia utu na heshima.
“Hii
ina maanisha kwamba, kutumia lugha nzuri, nyepesi na ya huruma, kuwa wavumilivu
pale waathirika hao wanaposhindwa kujielezea kwa ufasaha wawapo maeneo yenu ya kazi ili kutengeneza mazingira
ya mahakamani kuwa salama kwake na kumtengenezea mazingira rafiki awapo mahakamani.
Pia tunatakiwa kutambua kwamba mshitakiwa naye ana haki za msingi ambazo zinatakiwa
kuheshimiwa ili haki iweze kutendeka bila upendeleo. Kwa muktadha huo hii ni
kazi ngumu kwa pande zote mbili zinazopigania haki. Haki ya mwathirika kwa
upande mmoja na na haki ya mtuhumiwa kwa upande mwingine ili kuhakikisha na kuona haki imetendeka
bila upendeleo,” amehimiza Jaji Mfawidhi.
Vilevile,
Jaji Mfawidhi huyo amesema, ameipitia ratiba ya mafunzo na mada zitakazo tolewa
na wakufunzi na kujiridhisha kuwa, watawapitisha katika njia za kuepuka
kutonesha majeraha ya waathirika wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na kingono
na kwa kupitia mada hizo na nyingine zitasaidia kujadili mbinu zinazotumika kwa
sasa na kuainisha maeneo ya kuboresha mbinu hizo.
Katika
hotuba yake, Mhe. Dkt. Masabo amewaasa washiriki hao kuzingatia yale yote
watakayofundishwa kwenye mafunzo hayo, kushiriki kikamilifu na kuuliza maswali
inapobidi na kuchangia uzoefu ili kujenga uelewa mzuri na wa pamoja kwa
kuhakikisha waathirika wa ukatili wa kingono wanakuwa na mazingira rafiki
kipindi wanatoa ushahidi wao Mahakamani.
“Ujuzi
na maarifa tutakayojengewa kupitia mafunzo haya visihishie hapa na kwetu peke yetu mathalani nimebaini katika mafunzo haya hawapo Mawakili wa kujitegemea (Practising
Advocates) kwenye kundi hili, ni rai yangu mkawashirikishe maarifa haya wenzenu
mnaofanya nao kazi, elimu mliyoipata hapa pindi mtakapo rejea makazini, mfano
binu za kuuliza maswali kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kingono ni
jambo la msingi sana kwa Mawakili wanaowawakilisha watu wenye mashauri ya aina
hii,” ameongeza Jaji Masabo
Mhe.
Dkt. Masabo ameongeza kuwa, Mahakama ya Tanzania pamoja na IJA wataandaa mpango
wa kufanya tathmini ya utekelezaji kuona kama kweli mafunzo hayo yamewasaidia
washiriki kupiga hatua katika kushughulikia na uendeshaji wa mashauri hayo
yanapofika mahakamani na kutoa matokeo chanya.
Mhe.
Dkt. Masabo akahitimisha kwa kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kufanya kazi
kwa ushirikiano ili kufanya mfumo wa utoaji haki kuwa rafiki na wenye ufanisi
mkubwa katika kuendesha mashauri ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa
kingono kwa kuzingatia maslahi mapama ya waathirika wa vitendo hivyo na pia
bila kuathiri haki za watuhumiwa wa vitendo hivyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo leo tarehe 04 Februari, 2025 amefungua mafunzo ya kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kingono (Avoiding re-traumatization of victims and witnesses of sexual and gender-based violance) mafunzo hayo yanatolewa kwa Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo leo tarehe 04 Februari, 2025 amefungua mafunzo ya kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kingono (Avoiding re-traumatization of victims and witnesses of sexual and gender-based violance) mafunzo hayo yanatolewa kwa Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Irish Rule of Law International Bi. Maria Mccloskey akifafanua jambo wakati wa hafla ya kufungua mafunzo ya ukatili wa kijinsia na ukatili wa kingono .
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Waendesha Mashtaka wanaoshiriki mafunzo ya kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili wa kingono. Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora Mhe. Dkt. Zainabu Mango (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Irish Rule of Law International Bi. Maria Mccloskey.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni