Jumatano, 5 Februari 2025

JAJI MTULYA AHIMIZA UTENDAJI WA HAKI


Na KANDANA LUCAS – Mahakama, Musoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya. Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya amehimiza vyombo vyote vya utoaji haki kutenda haki katika utoaji wa maamuzi mbalimbali,ili kuweza kuhakikisha  malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka2050 yanafikiwa

Aidha Mhe. Mtulya amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania ni sehemu ya Dira ya  Taifa Maendeleo ya Mwaka 2050, hivyo inao wajibu kisheria kutenda haki kwa wakati, kutochelewesha usikilizaji wa mashauri, kutumia usuluhishi katika kutatua migogoro na kutoa maamuzi bora yenye uwazi bila upendeleo.

Akizungumza hivi karibuni akiwa mgeni rasmi wa hafla  ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, Mhe Mtulya  ameeleza namna Mahakama ya Tanzania ilivyojipanga ili kuhakikisha malengo ya Dira ya hiyo yanafikiwa.

“Mahakama ya Tanzania kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka  2050, ni sehemu ya maendeleo ya nchi hii kwani imeweka mikakati mbalimbali yenye dhamira kuu ya kusimamia haki kwa wote, kutoa maamuzi yenye ubora,maamuzi yanayozingatia haki, uwazi bila upendeleo wowote na kutoa maamuzi bila kuchelewa kama ilivyo kwenye Dira ya Mahakama inayosema Utoaji Haki kwa Wakati na kwa watu wote,” Jaji Mtulya amesema.

Kwa upande mwingine, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa namna ilivyojipapambanua katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) na uboreshaji wa miundombinu ya majengo kwani maboresho hayo yamesogeza huduma kwa wananchi ikiwa ni viashiria chanya katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka  2050.

“Mhe. mgeni rasmi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, nichukue nafasi hii kupongeza jitihada zilizofanywa na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kufanya maboresho makubwa ya miundo mbinu ya majengo ya Mahakama na kuwekeza kwenye matumizi ya TEHAMA. Maboresho haya ni chachu ya kuyafikia malengo ya Dira ya  Taifa ya Maendeleo ya  Mwaka 2050,”.

Katika maadhimisho hayo, viongozi wengine waliosoma hotuba zao ni pamoja na Wakili Mfawidhi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mara, Bw. Kitia Turoke na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika Chapta ya Mara, Bw. Otieno Onyango pamoja na viongozi wa dini ambao walisoma dua na sala za kuiombea Mahakama kuelekea kuanza mwaka mpya wa kimahakama.

Ambapo Mhe. Mtulya aliwaongoza wadau, wananchi na watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma, kusherekea Siku ya Sheria nchini iliyohitimishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu Musoma baada ya Maonesho ya Wiki  ya Sheria  yaliyofanyika  kuanzia tarehe 25 Januari, 2025 hadi 1 Januari ,2025, na kilele chake kufanyika tarehe 3 Februari, 2025.

Vilevile maadhimisho hayo yamefanyika katika Mahakama zote za Wilaya mkoaniMara ambazo ni Bunda, Tarime, Serengeti, Butiama na Rorya.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu HamiduMtulya akipokea salaam za heshima kutoka kwa maaskari (hawapo pichani) kabla ya ukaguzi wa gwaride. 

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya akisoma hotuba yake ya Siku ya Sheria. 

 Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara.

 Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Mara, Bw.Kitia Turoke akisoma hotuba ya Wakili Mkuu wa Serikali.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya (katikati kwa waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wahe. Majaji, viongozi mbalimbali na Mawakili wa Serikali (waliosimama).

 Muonekano wa mbele wa Mahakama Kuu Tanzania  Kanda ya Musoma, wakati maadhmisho ya Siku ya Sheria.


Wananchi wakifuatilia kwa makini uendeshaji wa shauri la mauaji kwa njia ya TEHAMA likiashiria ufunguzi wa shughuli la kimahakama.

Meza kuu katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma (waliosimama).

 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bunda (kushoto mwenye suti nyeusi) akikabidhi mahitaji mbalimbali ya wafungwa na mahabusu wa Gereza la  Wilaya Bunda ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizofanyika kuazimisha Siku ya Sheria katika Kanda ya Musoma.

 (Habari hii imehaririwa na MAGRETH KINABO- Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni