Jumatano, 5 Februari 2025

MKUU WA WILAYA NJOMBE AWAASA WANANCHI KUTATUA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda ametoa rai kwa wadau wa Mahakama pamoja na wananchi   wa Wilaya na Mkoa wa Njombe kumaliza matatizo yao nje ya Mahakama  kwa njia ya usuluhishi.

Mhe. Sweda aliyasema hayo tarehe 03 Februari, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.

 “Mashauri mengi huchukua muda mrefu kutokana na utafiti pamoja na kukusanya ushaidi kwa maana kwamba ukishindwa kwa njia ya usuluhishi basi ndo uje kwa njia ya maamuzi ya kisheria ambayo yatatolewa mahakamani,” alisema Mhe. Sweda.

Alitoa mifano mbalimbali huku akiwaasa wananchi wa Wilaya ya Njombe kukaa na Wazee pamoja na Viongozi wa Dini ili kutatua changamoto wanazokutana nazo na kueleza kuwa, kuna haki ya kushinda na kushindwa zote ni haki.

Mhe. Sweda aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua aliyofikia huku akitoa pongezi kwa Viongozi, Watendaji wa Mahakama, Wanasheria pamoja na wadau wa Mahakama kwa ujumla kwa kazi nzuri wanazofanya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama alisema kwamba mashauri mengi ambayo yapo Mahakama ya Njombe ni ya mauaji pamoja na ubakaji na siyo mashauri ya kibiashara huku akiongeza kuwa, kwa sasa kuna ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Haki mkoani Njombe ambapo ujenzi unaendelea.

Aidha, alibainisha kuwa, ndani ya miaka mitano Mahakama imefanya maboresho kwa Mkoa wa Njombe hasa majengo yaliyojengwa ambayo ni Mahakama za Wilaya Makete na Wanging’ombe pamoja na Mahakama ya Mwanzo Luilo ambayo bado haijazinduliwa.

Mhe. Chamshama aliongeza kuwa, ujenzi unaoendelea wa Mahakama za Mwanzo Manda ambayo ipo Wilaya ya Ludewa na Mahakama ya Mwanzo Lupembe iliyopo Wilaya ya Njombe ambapo alisema ujenzi wa Mahakama hizo ni jitihada za Serikali katika kuhakikisha huduma za Mahakama zinawafikia wananchi wote.

Kadhalika, Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo, alisema ujenzi wa Kituo Jumuishi utakapokamilika huduma zote za kimahakama pamoja na mifumo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) zitakuwa zinapatikana kwenye jengo moja.  

Nao, Mwendesha Mashtaka Mfawidhi, Bw. Shabani Mwegole Kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na Wakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS), Bw. Innocent Kibadu kwa pamoja walisema kuna umuhimu wa Taasisi katika kusimamia haki madai utasaidia kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na Serikali kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw.Richard Mbambe aliwashukuru wananchi pamoja na wadau kwa kufika katika hafla ya Maadhimisho hayo.

Katika maadhimisho hayo, Bw.Mbambe  aliongoza zoezi la utoaji vyeti kwa Taasisi mbalimbali ambazo zimekuwa mchango mkubwa kwa Mahakama ambazo ni Msaada wa Kisheria Njombe, Njombe TC, Mamlaka ya Mji Njombe (NJUWASA), Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Njombe, Mamlaka ya Mapato Tanzania-Njombe (TRA) Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Njombe (TAKUKURU), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Njombe (NPS) na Mawakili wa Kujitegemea (TLS) na wengine.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Taasisi mbalimbali, Viongozi wa Dini, Ofisi ya Mashtaka Njombe, Mawakili wa Kujitegemea, Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Taasisi mbalimbali, wanafunzi kutoka Vyuo vya mkoani Njombe pamoja na wananchi.


Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda akizungumza na watumishi wa Mahakama, wadau mbalimbali wa Mahakama na wananchi wa Wilaya ya Njombe wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 03 Februari, 2025.

 

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda (kushoto) akiwa katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe. Katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya  ya Njombe na nyuma ni wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe, Magereza Wilaya ya Njombe na Jeshi la Akiba.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama akizungumza na watumishi, wadau na wananchi wa Wilaya ya Njombe wakati Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 03 Februari, 2025.


Mtendaji wa Mahakama  ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Njombe Bw. Richard Mbambe aliyeshika karatasi akifurahi  pamoja na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Njombe wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 03 Februari, 2025.


Wadau kutoka Taasisi mbalimbali wa Wilaya ya Njombe pamoja na wananchi waliojitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini wakifuatilia kinachojiri wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku hiyo.


Mawakili wa Kujitegemea kutoka Njombe wakiwa wamesimama kwa pamoja wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Njombe tarehe 03 Februari, 2025.

Mawakili kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (NPS) wakiwa katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 03 Februari, 2025.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni