•Yadhihirisha mbele ya waalikwa kuwa ipo kidijitali kwa kusikiliza shauri kwa njia ya mtandao
Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini Kanda ya Tabora ambaye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi amesisitiza juu ya umuhimu wa taasisi zinazohusika na haki za madai katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Mahakama Kuu Tabora, Mhe. Dkt. Mambi alisema kuwa, Sekta ya Sheria ina mchango muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
"Sekta ya Sheria ina mchango muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi. Taasisi zinazohusika na haki za madai ni nguzo muhimu katika mchakato wa maendeleo ya Taifa. Ili kufikia malengo ya taifa ifikapo mwaka 2050, ni muhimu kuimarisha mifumo ya utoaji haki ili kuhakikisha haki inapatikana kwa usawa na kwa wakati, hivyo kuchangia katika mafanikio ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi," alisema Jaji Dkt. Mambi.
Katika hotuba yake, Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza kuwa sekta ya sheria ina mchango muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi chini ya Kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.’
“Kaulimbiu hii inalenga kuonesha kuwa Taasisi za kisheria ni nguzo muhimu katika mchakato wa maendeleo ya taifa, na hivyo ni muhimu kuimarisha mifumo ya utoaji haki ili kuhakikisha kuwa malengo ya taifa yanatimia,” alisisitiza Mhe. Dkt. Mambi.
Katika hafla hiyo kulifanyika tukio la kipekee la kusikiliza shauri kwa njia ya mtandao hivyo, kuwapa fursa wananchi kujionea hatua kubwa ambayo Mahakama ya Tanzania imefikia katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mbinu za kisasa za kusikiliza mashauri.
Wadau na wananchi walikiri kuwa matumizi ya TEHAMA katika Sekta ya Sheria ni muhimu na kusisitiza kuwa katika uboreshaji wa huduma ya utoaji wa haki na huduma za kisheria nchini wamezishauri taasisi na wadau wengine kuiga mfano waliojionea ili kutoa huduma bora kwa wananchi wote.
“Matumizi ya teknolojia katika sekta ya sheria ni muhimu sana na ni hatua muhimu katika kuboresha utoaji wa haki na huduma za kisheria nchini, leo tumejionea jinsi teknolojia inavyoweza kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi. Tunawashukuru wadau wa sekta ya sheria kwa juhudi zao na tunatoa wito kwa taasisi na wadau wengine kuiga mfano huu ili kutoa huduma bora kwa wananchi wote," alisema Mwananchi mmojawapo aliyehudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Viongozi mbalimbali wa dini, Majaji, Watumishi, Viongozi wa Serikali, Wanasheria, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mawakili na wadau wa Sekta ya Sheria na wananchi kwa ujumla walihudhuria katika hafla hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akipokea salamu za heshima wakati wa gwaride rasmi kwenye maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Tabora tarehe 03 Februari, 2025.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akihutubia hadhara iliyojitokeza wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Tabora tarehe 03 Februari, 2025.
Watumishi na wadau wa Mahakama wakiwa katika shamrashamra za furaha, wakicheza nyimbo wakati wa hafla ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Tabora, Wakili Kelvin Kayaga akisoma hotuba yake katika sherehe za maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini zilizofanyika tarehe 03 Februari, 2025 katika Viwanja vya Mahakama Kuu Tabora.
Wakili wa Serikali, Carson Nkya akisoma hotuba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika sherehe za maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Deusdedith Katwale akizungumza neno kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni