Na INNOCENT KANSHA – Mahakama, Morogoro
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mahakama
Inayotembea (Mobile Court) imeongeza kiwango kikubwa cha upatikanaji wa huduma
za haki nchini na huduma hiyo muhimu imekuwa chachu na kuongeza ufanisi wa
utoaji haki kwa wananchi. Mahakama inajivunia kutumia huduma hiyo kuwafikia
wananchi badala ya wananchi kuifuata Mahakama mahali ilipo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari na Umma kwa ujumla kupitia vyombo
vya Habari mkoani Morogoro leo tarehe 6 Februari, 2025 kuhusu utekelezaji wa
bajeti na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025,
Prof. Ole Gabriel amebainisha kuwa, huduma hiyo muhimu ya Mahakama mtaani
kwako ama Mahakama Inayotembea ilianza kutumika kama programu ya majaribio (Pilot
Program) kupitia Mikoa miwili ya Dar es salaam na Mwanza.
“Mahakama ya Tanzania imeongeza idadi ya Mahakama hizo kutokana na
umuhimu wa mahitaji ya huduma hiyo kwa wananchi kutoka mbili za awali na
kufikia nane kwa maana Mahakama zinazotembea sita tayari zimeagizwa mpaka sasa
Mahakama hizo tatu zimekwisha pokelewa na kupelekwa maeneo yenye uhitaji. Lakini
wigo wa huduma hiyo umetanuka na itapatikana katika mikoa ya Dodoma, Mbeya na
Tabora ambao ni mkoa mkubwa sana katika nchi yetu,” ameongeza Prof. Ole
Gabriel.
Prof. Ole Gabriel amesema, kwa kupitia huduma ya Mahakama
Inayotembea kuendesha mashauri yaliyofunguliwa na wananchi. Mashauri 39 tu ndiyo
yalivuka mwaka 2024 na mashauri 2369 yalifunguliwa na jumla ya mashauri 2374
yaliamuriwa sawa na asilimia 98.5 ya mashauri yote yaliyotolewa uamuzi mwaka
2024.
“Huduma ya utoaji haki kupitia Mahakama Inayotembea imewafikia
wananchi wapatao 14,225 hii ni idada kubwa kwa kipindi kifupi sana, ikiwemo
wanawake 7,697 na wanaume 6,528 hii inaonesha wanawake ni takribani asilimia 54
na wanaume ni asilimia 46 ya wale ambao wamefikiwa na kufungua mashauri yao
katika Mahakama hii,” amesema Mtendaji
Mkuu huyo.
Huduma ya Mahakama Inayotembea imehakikisha inazingatia pia kutoa
huduma bora kwa watu wenye mahitaji maalum imetengenezwa kumuwezesha mtu huyo
kutumia ngazi maalum itakayoweza kumwezesha kuingia kwenye Mahakama hiyo ili
kuhudumiwa kirafiki bila kujali hali ya muhusika. Kwa sababu Mahakama inaamini
kwamba Mungu ndiye amemuumba kila mtu kwa namna ambavyo alivyo, ameongeza Prof.
Ole Gabriel.
“Hivyo kwa maelekezo mahususi sana ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amesisitiza kwamba huduma zetu ziwe zinamlenga mwananchi
(Citizen Centric) kwa hali yoyote ile na hii huduma sasa imekuwa ikisaidia sana
kwa sababu huduma sasa imekuwa ikimfuata mwananchi badala ya wananchi kufuata
huduma,” amesisitiza Mtendaji Mkuu.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo akataja maeneo takribani sita ya vipaumbele
vya bajeti ya mwaka 2024/2025 pamoja na mambo mengine yamejikita katika kutekeleza
majukumu ya vipaumbele, mosi ni kuharakisha utatuzi wa mashauri kwa kuondoa
mashauri mlunikanao kwani kazi ya Mahakama ni kutoa maamuzi kwa njia ya
kusikiliza mashauri yanayoletwa na wananchi mahakamani, kuimarisha uwezo katika
usimamizi wa shughuli za kimahakama, kuendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na
ukarabati wa majengo katika maeneo mbalimbali nchini.
Vilevile, Prof. Ole Gabriel ameongeza kuwa vipaumbele vingine ni Uboreshaji
wa mifumo ya tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kutumia zaidi
wataalum wa ndani, lakini pia kuongeza ushirikiano wa wadau mbalimbali mfano; Jeshi
la Polisi, Magereza, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Taifa, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Ustawi
wa Jamii pamoja na wadau wengine katika mnyororo wa utoaji haki nchini na
kuboresha maeneo ya rasilimali watu (Human Capita Development HCD).
Mahakama ina amini inapowekeza katika mafunzo kwa watumishi inapata
watumishi wenye uwezo mkubwa na kupata matokeo chanya kwenye utendaji wa kutoa
huduma kwa ufanisi mkubwa wa kuwahudumia wananchi.
Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama akatoa rai na kuwasihi Waandishi wa
Habari nchini kuendelea kuandika mambo kwa ufasaha, weledi na kuyaandika kwa
fikira chanya ‘positive mind set’ ili kuuelimisha umma mambo yanayotekelewa na
mhimili kwa manufaa ya umma kwa sababu mwandishi atakapo andika habari
changanishi za kufanya yule mlaji wa habari achanganyikiwe itapunguza imani kwa
mwananchi dhidi ya chombo chao ni matumaini ya Mahakama kwa waandishi wa hapa
Morogoro lakini pia waandishi kote nchini watakuwa wamepokea rai hiyo na litakuwa
ni jambo la maana katika kuwahudumia umma wa watanzania.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari wakati wa mkutano wake kupita vyombo vya Habari mkoani Morogoro leo tarehe 6 Februari, 2025 kuhusu utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari wakati wa mkutano wake kupita vyombo vya Habari mkoani Morogoro leo tarehe 6 Februari, 2025 kuhusu utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni