Alhamisi, 6 Februari 2025

UMALIZAJI, UONDOSHAJI MASHAURI MAHAKAMANI WAZIDI KUPAA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama ya Tanzania imeendelea kutekeleza jukumu lake la kikatiba la utoaji haki kwa Wananchi kwa ufanisi mkubwa kwa mwaka 2024, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani hapa leo tarehe 6 Februari, 2025 kuhusu utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025, Prof. Ole Gabriel amebainisha kuwa Mahakama imepiga hatua katika viashiria vyote vikuu vya utendaji kazi ikilinganishwa na mwaka 2023.

Ameeleza kuwa kiwango cha umalizaji wa mashauri kimeongezeka kwa asilimia 101, huku kiwango cha uondoshaji wa mashauri kikipanda kwa asilimia 84 na wastani wa muda wa kumaliza shauri ukipungua hadi siku 78.

“Mahakama za Mwanzo ambazo zimehudumia Wananchi wengi zaidi kwa asilimia 70 wanaotafuta haki kwenye mfumo wa Mahakama zilitumia wastani wa siku 37 kumaliza shauri moja. Wastani wa mashauri kwa kila Jopo umepungua toka mashauri 234 mwaka 2023 hadi 227 mwaka 2024,” amesema.

Akizungumzia Mahakama Inayotembea, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa mashauri 39 yalivuka mwaka na mashauri 2,369 yalifunguliwa, ambapo jumla ya mashauri 2,374 yamesikilizwa na kumalizika, sawa na asilimia 98.5 ya mashauri yote.

“Mahakama Inayotembea imeendelea kutoa huduma kwa Mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza. Wigo wa huduma katika kipindi husika umeongezeka kwa Mikoa ya Mbeya na Dodoma. Hivi karibuni, huduma zitaanza mkoani Tabora. Huduma hii kwa sasa imenufaisha watu 14,225, wakiwapo wanawake 7,697 na wanaume 6,528,” amesema.

Prof. Juma ameeleza pia kuwa kwa sasa Mahakama Inayotembea inatoa huduma katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo, hivyo kusogeza huduma karibu na Wananchi na imeonesha kuwa na ufanisi kwa kusikiliza mashauri mengi kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi.

Ameeleza kuwa siri ya mafanikio hayo inatokana na utendaji na uwajibikaji nzuri wa Majaji, Mahakimu, Watendaji na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla, ushirikiano wa Wadau, matumizi ya teknolojia na uwezeshaji wa Serikali katika maeneo mbalimbali, ikiwemo rasilimali fedha na watu.

Katika kipindi husika, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa jumla Majaji watano wa Mahakama ya Rufani na Jaji mmoja wa Mahakama Kuu ya Tanzania wameteuliwa, hivyo kuongeza kasi ya usikilizaji na umalizaji wa mashauri.

Aidha, Prof. Ole Gabriel amesema, katika kipindi husika, Mahakama ya Tanzania imeajiri jumla ya watumishi 498, kati yao wakiwa Mahakimu Wakazi 88, Watumishi 1,167 wamepandishwa vyeo na wengine 107 wamebadilishwa kada, kati yao wakiwa Mahakimu Wakazi 43.

Mahakama ya Tanzania, katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, inatumia Mpango Mkakati wa Mwaka 2020/21- 2024/25 ambao umeweka vipaumbele katika maeneo mbalimbali.

Maeneo hayo ni kuharakisha utatuzi wa mashauri na kutekeleza mkakati wa kumaliza mashauri ya muda mrefu; kuimarisha uwezo katika ukaguzi na usimamizi wa shughuli za Mahakama na kuendelea kutekeleza Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali.

Maeneo mengine ni kuboresha Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama nyenzo muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma; kuongeza ushirikiano na Wadau ili kuharakisha huduma ya utoaji haki na kuimarisha maendeleo ya rasilimaliwatu, ikiwa ni pamoja na mafunzo na nidhamu kwa Watumishi.

Kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) na 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chombo chenye mamlaka na kauli ya mwisho katika kutekeleza utoaji haki ni Mahakama ya Tanzania. Mahakama ya Tanzania ipo katika ngazi za Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu (Kanda na divisheni), Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Mwanzo. 


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (juu na chini) akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka 2024/2025 leo tarehe 6 Februari, 2025 mjini Morogoro.


Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri wakati wa Mkutano huo.


Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali (juu na chini) wakitekeleza majukumu yao.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni