Alhamisi, 6 Februari 2025

MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMANI YANAVYOLETA NEEMA KWA WANANCHI

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye shughuli za kimahakama yameleta mafanikio makubwa kwa Wananchi, ikiwemo kupunguza gharama na muda kwenye mchakato mzima wa utoaji haki.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani hapa leo tarehe 6 Februari, 2025, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa TEHAMA inamwezesha Mwananchi kufungua shauri popote alipo na kusikilizwa kwa njia ya kielektroniki bila ya kulazimika kwenda mahakamani.

Ametaja baadhi ya mifumo mbalimbali inayomilikiwa na Mahakama ya Tanzania ambayo inamwezesha Mwananchi kupata huduma mbalimbali za kimahakama kwa urahisi kama Mfumo wa kielektoniki wa Kuratibu Mashauri (e-CMS), Mfumo wa Kunukuu na Kutafsiri Mwenendo wa Mashauri (TTS), Mfumo wa Takwimu (Data Hub) na Mfumo wa Taarifa za Hukumu na Sheria Tanzania (TanzLII).

“Mfumo wa TanzLII umeondoa kabisa malalamiko ya Wananchi ya kupata hukumu baada ya shauri kumalizika kwa upande wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani. Kwa sasa hukumu zinapandishwa kwenye Mfumo huo siku hiyo hiyo baada ya kusomwa. Hadi sasa jumla ya uamuzi 60,319 umechapishwa katika mfumo wa TanzLII,” Mtendaji Mkuu amesema.

Prof. Ole Gabriel ameeleza baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana kufuatia matumizi ya TEHAMA mahakamani, ikiwemo kufanikisha upatikanaji wa takwimu za Mahakama za Mwanzo kupitia Mobile App na kufanikisha upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wateja kupitia mfumo.

Mafanikio mengine ni upatikanaji wa taarifa mbalimbali za mwenendo wa mashauri kupitia ujumbe mfupi (SMS), utoaji wa namba za mashauri kupitia mfumo wa kielektroniki na kuwezesha usajili wa mashauri kwa njia ya kielektroniki, hivyo kupunguza muda na gharama na mwingiliano kati ya Watumishi wa Mahakama na Wananchi.

“Maboresho katika nyanja ya TEHAMA ni endelevu hususan katika kuhakikisha huduma ya utoaji haki inafanyika kwa haki na kwa wakati,” Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania amesema na kuongeza kuwa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni nyenzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma mahakamani.

Prof. Ole Gabriel amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa Mahakama ya Tanzania itaendeleza matumizi ya TEHAMA katika shughuli mbalimbali za Mahakama kwa ngazi zote na kuongeza wigo wa huduma za TEHAMA kwa kujumuisha mifumo inayotumia akili mnemba kupitia simu za mkononi.

Kadhalika, Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kutoa mafunzo kwa Majaji, Mahakimu, Makarani na maafisa TEHAMA; kuimarisha ushirikiano na Wadau katika kubadilishana taarifa ili kuongeza ufanisi na kuendeleza ubunifu na kuzingatia mahitaji ya watumiaji wa mifumo ya TEHAMA katika kutumia teknolojia ya hali ya juu.

Kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) na 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chombo chenye mamlaka na kauli ya mwisho katika kutekeleza utoaji haki ni Mahakama ya Tanzania. Mahakama ya Tanzania ipo katika ngazi za Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu (Kanda na divisheni), Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Mwanzo.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Morogoro leo tarehe 6 Februari, 2025 kuhusu utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025.


Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri wakati wa mkutano huo. Picha chini ni sehemu ya Waadishi wa Habari wakichukua kumbukumu muhimu.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni