Alhamisi, 6 Februari 2025

UBORESHAJI MIUNDOMBINU YA MAJENGO YA MAHAKAMA WASAMBAA KILA KONA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama kwa kujenga majengo ya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini ili kusogeza huduma za kimahakama karibu zaidi na Wananchi na kuimarisha mifumo ya utendaji kazi.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel mkoani hapa leo tarehe 6 Februari, 2025 alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa bajeti  na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025.

“Hadi kufikia Disemba, 2024, Mradi wa Maboresho kupitia fedha za Benki ya Dunia umeendelea kutekelezwa katika miradi ya ujenzi wa majengo ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa katika Mikoa ya Katavi, Simiyu, Songwe, Ruvuma, Geita, Lindi, Njombe, Singida na Pemba na Mahakama za Mwanzo 60 katika Mikoa mbalimbali hapa nchini,” amesema.

Prof. Ole Gabriel amebainisha kuwa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma umefikia asilimia 97.5 huku ujenzi wa nyumba za Majaji jijini Dodoma ukiwa umefika asilimia 98.5.

“Jengo hili litakapozinduliwa litakuwa la sita kwa ukubwa duniani na la kwanza katika Bara la Afrika. Tunaishukuru sana Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo hili la kihistoria katika nchi yetu,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ametaja miradi mingine inayoendelea kama ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Korogwe ambao umefikia asilimia 80 na ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Ubungo ambao upo asilimia 97.

“Ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo saba za Ilangala (Ukerewe) ambao umefika asilimia 20, Mbalizi (Mbeya) asilimia 64, Ketumbeine (Arusha) asilimia 80, Machame (Kilimanjaro) asilimia 10, Kinusi (Mpwapwa) asilimia 25, Rugwa (Manyoni) asilimia 0.05 na Haubi asilimia 28,” amesema.

Prof. Ole Gabriel ameeleza pia kuwa ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya nane nao unaendelea kwa viwango tofauti huku Mahakama ya Wilaya Kibiti (Pwani) ikifikia asilimia 3.5, Nachingwea (Lindi) asilimia 2, Simanjiro (Manyara) asilimia 2, Hanang (Manyara) asilimia 4.1, Mbulu (Manyara) asilimia 5, Chamwino (Dodoma) asilimia 15.3, Mkalama (Singida) asilimia 5 na Tunduru (Ruvuma) asilimia 1.5.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama amesema pia kuwa miradi ambayo ipo katika hatua za awali na manunuzi na Wakandarasi wamekabidhiwa maeneo ya ujenzi hivi karibuni kwa miradi ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kilosa; Uyui na ujenzi wa jengo la Mahakama za Mwanzo Magubike (Kilosa) na Kipili (Sikonge).

Ametaja miradi iliyo katika hatua mbalimbali za manunuzi kama ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Masasi, Handeni; Kishapu; Tarime; Kiteto; Kalambo; Mlele; Momba; Mkalama; Nyasa na Rufiji, ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Mkuyuni na Mkomazi na ukarabati wa nyumba za Majaji katika Mikoa ya: Iringa; Mbeya; Tanga na Tabora.

Prof. Ole Gabriel amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa Watumishi, kuendelea kuboresha taratibu za utaoji huduma ili kuongeza ufanisi, kuendelea kuboresha Majengo ya Mahakama yaliyopo na kujenga mapya na kuendelea kutekeleza Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa bajeti  na majukumu ya Mahakama ya Tanzania kwa nusu mwaka wa fedha 2024/2025 leo tarehe 6 Februari, 2025  mjini Morogoro. Picha chini ni Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakifutilia matukio mbalimbali wakati wa mkutano.





Sehemu ya Waandishi wa Habari (juu na chini) wakichukua matukio mbalimbali.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni