Jumanne, 4 Februari 2025

MKUU WA WILAYA KIBAHA ASISITIZA UPENDO KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon ametoa rai kwa watumishi wa Mahakama kutanguliza upendo katika utendaji kazi wao. 

Mhe. Simon aliyasema hayo jana tarehe 03 Februari, 2025 katika hafla ya Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani alipokuwa akimwakilisha Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.

“Haki ni upendo unaoonekana mahali penye upendo ujue kuna haki na ukitenda haki una uwezo pia wa kukemea uovu, msingi wa sheria ni kupata haki na haki ni upendo unaoonekana hadharani,” alisema Mhe. Simon.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi alisema kauli mbiu ya mwaka huu inatoa hamasa kwa taasisi zinazosimamia haki madai kutoa maoni au mapendekezo yao kwa kuzingatia majukumu na masuala yanayotekelezwa na taasisi hizo ambayo wanaona ni muhimu kuzingatiwa katika malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Mhe. Mkhoi alisema taasisi zinazosimamia haki madai wanao pia nafasi ya kuipitia na kutoa maoni na mapendekezo yao ya nini cha kuongeza, kuondoa kuboresha na hatimaye kuwezesha kupatikana kwa malengo makuu ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050. 

“Maoni ya kila taasisi inayosimamia Haki Madai ni thamani katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 yatakayokidhi maratajio na mahitaji ya Taifa, ni dhahiri Watanzania wana matamanio na matarajio ya kuona uchumi wao ukiwa umeimarika, umestawi na maisha ya kila tanzania yakiwa yameboreshwa ndani ya kipindi cha miaka 25,” alisema Mhe. Mkhoi

Naye Mkuu wa Mashtaka Pwani, Wakili Faraja George aliziomba ofisi na taasisi zote zinazohusika katika utoaji haki kujaza dodoso zinazotolewa na Tume ya Taifa ya Mipango kupitia tovuti yao za kukusanya maoni juu wa ufikiwaji wa watanzania ya mwaka 2050 ili kufikia mwaka 2050 kusiwe na changamoto.


Mkuu wa Wilaya ya Kibaha , Mhe. Nickson Simon akizungumza wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria iliyofanyika jana tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani. 

Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini jana tarehe 03 Februari, 2025 katika viwanja vya Mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani. 

Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani, Mhe. Emmael Lukumai 

Picha mbalimbali za maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni