Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
jana tarehe 17 Machi, 2025 alifungua Kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda na Divisheni, na kusisitiza mambo 12 wanayotakiwa kuzingatia
wanapotekeleza majukumu yao katika muktadha mzima wa utoaji haki nchini.
Mhe. Prof. Juma aliwapongeza Majaji Wafawidhi kwa
sababu wao, katika nafasi zao kama Viongozi ni wasimamizi wakubwa, sio tu
katika muhimu utoaji wa haki, lakini pia katika maboresho ya maendeleo.
“Matunda makubwa tunayapata chini ya Uongozi wenu,
maboresho yanafanyika makubwa, mmesimamia vyema hili gurudumu ambalo linasukuma
mbele maboresho. Mradi wa maboresho wa Benki ya Dunia wasimamizi wake wakubwa
wamekuwa ni nyinyi Majaji Wafawidhi…
“Nyingi ndio mmekuwa mkisimamia matumizi ya teknolojia
katika utoaji haki na kazi hii mmefanya kwa mafanikio makubwa kiasi kwamba
imekuwa ni kawaida mara kwa mara kupokea maombi ya Mahakama kutoka Nchi
nyingine kutaka kuja kujifunza kazi kubwa ambayo tunafanya,” Mhe. Prof. Juma
alisema.
Jaji Mkuu alitaja ugeni uliokuja kujifunza ni kutoka
Uganda kwa mara kadhaa, kutoka Malawi, kutoka Zimbabwe, kutoka Angola, Korea
Kusini, Uturuki, Jamhuri ya Watu wa China, pamoja na Vietnam na kwamba
wanatarajia ugeni kutoka Kazkazistan, Nchi ambayo imepiga hatua katika teknolojia.
Kadhalika, Mhe. Prof. Juma aliwashukuru Majaji kwa kusaidia
kuweka msingi imara wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na namna
ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050.
Kuendeleza mabadiliko ya kifikra na mitazamo
Jaji Mkuu aliwaeleza Majaji Wafawidhi kuwa maboresho
hayawezekani bila mabadiliko makubwa ya kifikra na mitazamo na kwamba msukumo
wa maboresho ambao unaendelea ni lazima uendelezwe.
“Tayari
uwekezaji mkubwa umefanywa katika Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi, katika Mfumo wa
Usimamizi wa Mashauri na usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao. Haya yote
hayatadumu kama hatutayaendeleza na wenye uwezo wa kuyaendelea ni sisi wenyewe,”
alisema.
Jaji Mfawidhi kioo katika Kanda au Divisheni
Jaji Mkuu aliwakumbusha Majaji Wafawidhi kuwa Watumishi
waliopo chini yao mara nyingi hufuata anachokifanya Kiongozi wao. “Ukiwa una
kawaida ya kuchelewa kufika ofisini, nao watachelewa. Ukiwa ni mjanja mjanja,
na wao watakuwa wajanja wajanja,” alisema.
Hivyo, aliwaeleza kuwa wao kama kioo katika Kanda na
Divisheni ni lazima waonyeshe uongozi katika hii zama ya matumizi ya akili
bandia na teknolojia.
“Ukionekana wewe Kiongozi unatumia teknolojia unakuwa
na uwezo wa kushawishi wale ambao unawaongoza kuweza vile vile kutumia
teknolojia. Ukiwa wewe ni Kiongozi kazi yako ni kulalamika au kulaumu
utawaambukiza wote unaowaongoza wao wawe ni watu wa kulalamika na kulaumu,”
Jaji Mkuu alisema.
Majaji Wafawidhi watatuzi wa changamoto
Jaji Mkuu amewashukuru Majaji Wafawidhi kwa kufanya
kazi hiyo kwa umakini mkubwa, jambo ambalo limesababisha changamoto chache kufika
kwa Jaji Kiongozi na yeye hajapata changamoto kwa muda mrefu.
“Kwa hiyo, mnauwezo mkubwa wa kupima na kutatua
changamoto mbalimbali ambazo tunakumbana nazo ambazo zimewawezesha kufanya
maamuzi ambayo yana msaada mkubwa sana kwetu sote,” alisema.
Kadhalika, Mhe. Prof. Juma aliwashukuru Majaji hao kwa
kuwa madaraja ya mahusiano mema baina au miongoni mwa mihimili kwani kaatika
kazi zao wanakutana na Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Kata ambao wana tabia na mitazamo
tofauti kuhusu Mahakama.
“Kwa hiyo, tuhakikishe tunakuwa hatuna migongano
ambayo haisaidii Wananchi, migongano ambayo haisaidii Taasisi zetu, siku zote
tujaribu kutatua kama jambo ni zito unalipandisha juu, huku juu kuna njia za
kuweza kupata utatuzi,” alisema.
Kuwalinda Majaji, Wasajili, Mahakimu wasishambuliwe
kwa hila, kuonewa.
Jaji Mkuu wa Tanzania amewaambia Majaji Wafawidhi hao
kuwa wasikae kimya pale wanapoona Hakimu anashambuliwa kwa hila au kwa kuonewa
kwani wana mamlaka makubwa ya kusimamia nidhamu.
Alifafanua kuwa Sheria inawataka wasimamie nidhamu na
kutokukaa kimya wakati Hakimu kesi inaendelea huku wahusika wanatoka nje na
kuanza kuzungumzia kilichoongelewa ndani.
“Unachotakiwa kufanya ni kumuita mhusika na kushow cause,
tuna mamlaka ya contempt, usipoweza kutumia hayo mamlaka utakuwa umeshindwa
kufanya kazi yako kama Jaji au Jaji Mfawidhi,” alisema.
Jaji Mfawidhi kuwa wabunifu
Jaji Mkuu amewahimiza Majaji Wafawidhi kuwa wabunifu
katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuwasaidia Watumishi wanaokuja na mawazo Chanya
katika eneo hilo.
Alitoa mfano wa Mtumishi mmoja anasoma PhD Chuo cha
Mandela, ambaye ameongea anaweza kuleta software ambayo ikapunguza kazi za
Mahakama ya Rufan na kuwafanya Majaji wa Mahakama ya Rufani kuwa hawana kazi
tena.
‘Hiyo ni provocation nzuri sana. Mtu ambaye atasaidia
kupunguza kazi, huyu lazima tumsaidie kwa kile tunachoweza ili huo ubunifu
utusaidie,” alisema.
Kutafuta maarifa kwa kujisomea
Jaji Mkuu aliwakumbusha Majaji Wafawidhi kujilinda na
matumizi mabaya ya akili bandia na kujitafutia maarifa kwa kusoma taarifa
mbalimbali. Aliwaeleza kuwa kama Kiongozi ni muhimu kuhamasisha wengine
kufanya.
“Kwa hiyo, tuwe na kawaida ya kusoma kila kitu
kinachokuja kwetu kinachohusu maboresho. Tusiingie katika mtego, unapata
nyaraka ambayo ni muhimu sana unampa msaidizi wako asome ili akushauri, hapo
unakuwa umekosa maudhui kamili ya kilichomo mle ndani,’ alisema.
Kutoa elimu, kusahihisha upotoshaji.
Jaji Mkuu aliwahimiza Majaji Wafawidhi kuwavuta karibu
Wadau wote na kuwaelimisha pale panapokuwa na malalamiko na kusahihisha kama
kuna upotoshaji wa aina yoyote.
‘Jukumu ni lenu kuhakikisha kwamba mnasahihisha ule
upotoshwaji. Muwe karibu na Wananchi na kuwasikiliza wanapolalamika, unapomsikiliza
anakusaidia kufahamu changamoto ambayo ipo katika Taasisi yako,’ amesema.
Kushughulikia malalamiko yanayojitokeza katika Vyombo
vya Habari
Jaji Mkuu amewaeleza Majaji Wafawidhi hao kuwa yeye
binafsi huwa najifunza mambo mengi kutokana na malalamiko katika Vyombo vya Habari
na wakati mwingine katika mitandao ya kijamii.
“Wakati mwingine unaweza kufahamu kinachoendelea
katika ofisi yako kwa kusomwa kinachoandikwa nje, na wakati mwingine
tunafahamiana vizuri kutokana na ufafanuzi unaoandikwa kuhusu wewe,” alisema.
Mhe. Prof. Juma aliwasisitiza kutofunga milango ya
kuwaruhusu Wananchi kulalamika na kuleta dukuduku zao, hivyo wanapaswa kuwapa
utaratibu wa kushughulikia malalamiko na majibu.
‘Kwa hiyo tusizibe hizi nafasi za wale wanaokuwa na
dukuduku zetu kwa sababu uelewa wa Sheria na taratibu za kimahakama bado ni
mdogo sana katika jamii yetu,” alisema.
Umuhimu wa teknolojia miaka 25 ijayo
Jaji Mkuu amewaeleza Majaji Wafawidhi kuwa zamani walikuwa
awnapambana kutokujua kusoma na kuandika, lakini katika karne ya 21 kwenye zama
za Dira ya 2050, mtu ambaye hataweza kutumia mifumo ya teknolojia atakuwa ni illiterate.
‘Tunaenda katika Dunia miaka 25 ijayo ambayo huwezi
kuishi bila teknolojia. Kwa hiyo, tujitayarishe kuachana na illitrace
inayotokana na matumizi ya teknolojia,’ amesema.
Kadhalika, Jaji Mkuu amewahimiza Majaji Wafawidhi
kusoma tena Sera, hususan Dira ya Taifa ya Maenedeleo 2025 na kufanya tathmini
katika maboresho yaliyofanyika kwa msaada mkubwa wa Benki ya Dunia.
‘Tunaweza kujiuliza kama tumeweza kutekeleza yote yaliyoainishwa katika Dira ya
2025. Kama kuna mambo ambayo hatujaweza kuyatekeleza tunaweza kuyaleta tena chini
ya Dira 2050. Kwa sababu tunajinazifu kwamba sisi Mahakama tumekuwa ni mfano wa
utekelezaji wa Dira ya 2025,’ alisema.
Kujitayarisha kuwa mfano wa utekelezaji Dira 2050.
Jaji Mkuu pia amewahimiza Majaji Wafawidhi kusoma kwa
makini Dira ya Taifa ya Maendeleao 2050 na kuilinganisha na shughuli wanazofanya
kila siku.
Alitoa mfano wa Dira hiyo inaposema ifikapo 2050, Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania itakuwa na watu million mia moja arobaini, hivyo unaweza
kujenga picha majengo ya Mahakama yaliyopo kama yatatosha kutoa huduma kama
inavyotolewa sasa na kama kasi ambayo tunaenda nayo sasa itaweza kumudu.
‘Kwa hiyo, huu wakati ni wa kujitayarisha na nyinyi
Viongozi katika kikao hiki tuanze kutafakari kwa sababu mpango mkakati wetu wa
miaka mitano nadhani unaisha Januari, mwakani,’ alisema.
Kufikiria mpango mkakati wa Mahakama wa miaka mitano
ijayo.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa kwa kuwa mipango iliyopo inaisha
na Mradi wa Benki ya Dunia nao unafikia mwisho, ni vema kwa Viongozi hao
kufikiria mpango mwingine wa miaka mitano ijaypo.
“Isije kuonekana kwamba uhai wetu na maboresho yetu
umesukumwa zaidi na uwekaji mkubwa ambao tumepata kutoka Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambayo imetuwezesha kufanya maboresho makubwa. Tutafute
namna gani ya kuendeleza hicho ambacho tumekianza,” alisema.
Utayarishaji kwa wakati vitabu vya rufaa
Jambo lingine ambalo aliwaambia Majaji Wafawidhi hao ni
kutafuta namna ya kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa vitabu vya rufaa baada
ya wadaawa kuwasilisha taarifa ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Alibainisha kuwa taarifa za kukata rufaa nyingine ni
za muda mrefu lakini Mahakama ya Rufani hawapokei vitabu kwa muda muafaka.
“Kwa hiyo vitengo vya Mahakama ya Rufani ambavyo vipo
kwenu ni sehemu ya majukumu yenu kusimamia, mhakikishe vile vile inatengewa
bajeti ya kutosha ili viweze kutayarisha vitabu vya Mahakama ya Rufani, kwa
sababu visipoweza kufanya hivyo kutakuwa na changamoto kubwa katika usikilizaji
wa rufaa,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni