- Awaomba kulinda afya zao kwa gharama yoyote
- Awashauri kula mbogamboga, matunda kiasi cha kutosha
- Aeleza ‘glass’ ya wine siyo muhimu kwa afya
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza
Kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda na Divisheni, kinachofanyika jijini hapa, leo tarehe 18 Machi,
2025 kimeingia siku ya pili, huku Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Prof. Abel Makubi akiwapitisha Majaji hao kwenye mada muhimu kuhusu afya.
Wakati akiwasilisha mada yake inayosema, ‘Mchango
wa Uchunguzi wa Afya juu ya Utambuzi na Kinga dhidi ya Magonjwa’ Prof. Makubi aliwaomba wajumbe wa Kikao hicho
kinachoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed
Siyani kulinda afya zao kwa gharama yoyote.
‘Mungu ametupa uhai, ulinde kwa gharama yoyote na kuwa
na kiasi kwa mambo yote,’ Mkurugenzi huyo amekiambia Kikao hicho
kinachohudhuriwa pia na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na
Viongozi wengine Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania.
Prof. Makubi aliongeza, “Uwezo wa kutunza afya yako ni
mhimili mkubwa wa maisha yako marefu na ufanisi katika kazi na familia. Kufanya uchunguzi
wa afya yako kila mara ni muhimu kwa ajili ya kutambua magonjwa mapema na
kupewa elimu ya kinga.”
Akiwasilisha mada hiyo, Mkurugenzi huyo aliwaambia
Majaji hao kuwa kuna makundi makuu mawili ya magonjwa, yaani yale ya
kuambukizwa ikiwemo Ukimwi, Maleria, Ajali, Kifua Kikuu na mengine ya
maambukizi na yale yasiyokuwa ya kuambukizwa kama magonjwa ya moyo, kansa, kisukari
na maengine.
Amesema kuwa idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana
na magonjwa yasiyoambukizwa ni mara mbili zaidi ya wale wanaotokana na magonjwa
ya kuambukiza.
‘Tatizo la magonjwa yasiyo ya kuambukiza linakua kwa
kasi katika Nchi zinazoendelea, kama Tanzania na moja ya mambo yanayochangia
kuongezeka kwa magonjwa haya, ni mabadiliko ya taratibu za kimaisha
zinazohusisha matendo yanayoweza kusababisha ugonjwa,” amesema.
Prof. Makubi ametaja baadhi ya taratibu hizo kama kutofanya
mazoezi, mfano: kukaa darasani, ofisini, kuangalia runinga, kutumia lifti,
kupanda magari na kutoshiriki michezo na ngoma za utamaduni.
Nyingine ni ulaji usiofaa kama kula chakula kuzidi ya mahitaji
ya mwili na hivyo kunenepa, kula mafuta na chumvi zaidi ya mahitaji ya mwili, kutokula
mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha na kula
nafaka zilizokobolewa.
Mkurugenzi huyo pia aliwaambia Majaji kuwa matumizi ya
pombe, tumbaku na madawa ya kulevya pamoja na msongo wa mawazo husababisha
magonjwa hayo.
‘Magonjwa mengi yasiyoambukiza hayana dalili za mapema.
Magonjwa mengi yasiyoambukiza yanaweza kuzuilika kwa kubadili tabia na mtindo
wa maisha. Magonjwa mengi yasiyoambukiza yana gharama kubwa ya tiba. Tuendelea
kupata elimu ya magonjwa ili kufahamu dalili na njia za kujikinga’ amesema.
Katika siku ya pili ya Kikao, Washiriki pia
wamepitishwa kwenye mada inayohusu taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya
huduma za Mahakama iliyowasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu
wa Kitengo cha Maboresho, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.
Wajumbe pia walipokea uzoefu kuhusu usimamizi madhubuti
na umalizaji wa mashauri ndani ya muda uliotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda na kuhusu
ushirikishwaji wa Wadau kwenye utekelezaji wa majukumu ya masingi ya Mahakama
uliotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe.
Kevin Mhina.
Kadhalika, wajumbe walipokea uzoefu kutoka kwa Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga
kuhusu ufanisi wa Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi na ule unaohusu mbinu za kumaliza
mashauri ya mlundikano uliotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi.
Baadhi ya Viongozi wa Mahakama wanaohudhuria Kikao
hicho ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Msajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji wa Mahakama Kuu-Kanda, Mtendaji wa
Mahakama Kuu-Divisheni, Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, Wakurugenzi
mbalimbali, Naibu Wasajili na wengine.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina akiwasilisha mada kwenye Kikao hicho.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni