Na INNOCENT KANSHA-Mahakama
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 18 Machi,
2025 amekutana na Ujumbe wa Banki ya Dunia na kufanya mazungumzo ya kina juu ya
shughuli za maboresho yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama kupitia ufadhili wa
Banki hiyo.
Akizungumza
na Ujumbe huo ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma, Prof. Ole
Gabriel ameushukuru ujumbe huo kutoka Banki ya Dunia kwa namna unavyoendela
kutoa ushirikiano na ushauri katika maeneo mbambali ili kufanikisha utekelezaji
wa mradi ya uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za haki nchini.
“Jambo
la msingi ninalotaka kuwahakikishia ni kwamba, tutasimamia miradi yote kwa ufanisi
na weledi wa hali ya juu, kwa viwango vinavyokubalika, hatutayumbishwa katika kusimamia
na tutahakikisha tunasimamia kwa kuzingatia ubora unaokubalika kitaalam, kwani
wataalum wa ndani wapo wa kutosha kuhakikisha miradi tunayoiendesha yote inakamilika
kwa kuzingatia thamani ya fedha,” amesisitiza Mtendaji Mkuu.
Vilevile
Prof. Ole Gabriel ameuambia ujumbe huo kuwa Mahakama itahakikisha inasimamia
ubora, usalama wa miradi na kuhakikisha kasi ya utekelezaji wa miradi inakwenda
kama ilivyopangwa bila kuathiri ubora wa miradi ya miundombinu inayoendelea
kutekelezwa.
Aidha,
Mtendaji Mkuu ameuhakikishia ujumbe huo kwamba ni matarajio ya Mahakama ya
Tanzania kuwa ndani ya kipindi cha miezi sita hadi kufikia Desemba 31, 2025
miradi yote ya ujenzi wa miundombinu itakayotumika kutolea haki itakuwa imekamilika
kwa asilimia 100.
“Kukamilika
kwa miradi hiyo itakuwa suluhisho la kudumu kwa wananchi hasa wale wenye
mahitaji maalum wanaohangaika kuzifikia huduma za haki nchini. Aidha, amesisitiza
kuwa Mahakama itaendelea na jitihada za kuboresha huduma hizo katika ngazi
mbalimbali za kimahakama na kuhakikisha Mahakama inamfuata mwananchi badala ya
mwananchi kuifuata Mahakama,” ameongeza Prof. Ole Gabriel.
Akiongoza
Ujumbe kutoka Banki ya Dunia uliomtembea Mtendaji Mkuu wa Mahakama ofisini kwake, Meneja Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa Mashariki mwa Afrika Bw. Manuel Vargas amesema,
“ni fahari kubwa kwa Banki ya Dunia na timu nzima ya ushauri iliyoko hapa kuwa
sehemu ya mafanikio haya yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika hatua
nzuri za kuboresha ya mifumo ya utoaji haki kwa wananchi,” Bw. Vargas.
Meneja
Mtendaji huyo Bw. Vargas ameongeza kuwa, Miradi ya Mahakama inayotekelezwa
ambayo Banki ya Dunia imekuwa mshirika inaonyesha taswira ya utengamano na ushirikiano
imara hasa katika kutekeleza malengo ya pamoja yaliyokusudiwa ya kumsongezea
mwananchi huduma ya utoaji haki karibu zaidi.
“Ikiwa
mradi huu wa maboresho ya miundombinu na matumizi TEHAMA unaelekea ukingoni ni
matarajio ya Banki ya Dunia kuona unakamilika na kutimiza adhima iliyokusudiwa na
kuacha alama kubwa kwa Jamii, Taasisi na Serikali ya Tanzania,” amesema Bw.
Vargas.
Vilevile,
Bw. Vargas amefafanua kuwa, Benki ya Dunia na timu nzima itaendelea kutoa ushirikiano
na kupanua wigo katika ufadhili kwa maeneo mengine muhimu kama vile kukuza
masuala ya usuluhishi (ADR), matumizi ya akili mnemba (IA) na matumizi ya
TEHAMA kwa ujumla ili kuongeza ufanisi katika shughuli za utoaji haki.
“Mahakama
ya Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika kuhakikisha inaimarisha miundombinu
ya kuwezesha urahisi wa utoaji haki kwa wananchi, mathalani tumeona ujenzi wa kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki kisiwani Pemba huko Zanzibar. Banki ya Dunia inaona
fahari ya kuendelea kufanya kazi na Mahakama ili kuboresha zaidi sekta hii,”
ameongeza Bw. Vargas.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo alipotembelewa na Ujumbe wa Banki ya Dunia leo tarehe 18 Machi, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma, kushoto ni Kiongozi wa Ujumbe huo Meneja Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa Mashariki mwa Afrika Bw. Manuel Vargas.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo alipotembelewa na Ujumbe wa Banki ya Dunia (haupo pichani).
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia Meneja Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa Mashariki mwa Afrika Bw. Manuel Vargas alipotembelewa na Ujumbe huo leo tarehe 18 Machi, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni