Alhamisi, 13 Machi 2025

JAJI MUGETA AWAFUNDA MAHAKIMU WAPYA ARUSHA

   . Awasisitiza kuwa waadilifu, wachapakazi na kuzingatia sheria na miongozo ya kazi

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta amewapa nasaha na maelekezo Mahakimu wapya kuhusu namna ya kuwa Mahakimu bora na kuwahudumia wananchi kwa viwango vinavyotakiwa. 

Mhe. Mugeta alitoa nasaha hizo jana tarehe 12 Machi, 2025 wakati akizungumza na Mahakimu hao kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Akizungumza na Mahakimu hao, Mhe. Mugeta aliwaeleza kuwa, anatarajia kwamba watawahudumia wananchi na sio kuwatesa na kwamba siku zote Mahakimu hao wajiweke katika miguu na viatu vya wananchi wanaowahudumia halafu waone kama maamuzi yao ni mazuri au mabaya kadri sheria inavyoelekeza.

“Lazima kila Hakimu afanye kazi kwa kuzingatia sheria, kwa mfano kama unatoa amri ya kuvunja ndoa, ni kwa sheria ipi, unaanzia wapi na kuishia wapi, hivyo kwa chochote utakachokuwa unafanya ni vizuri ukawa unaweka rejea ili ujijengee tabia na nidhamu ya kufanya vitu chini ya sheria,” alisisitiza Jaji Mugeta.

Aliwaeleza pia wasifanye kazi ya uhakimu kwa ili mradi tu, kwani wanatoa huduma kwa wananchi wenye hisia, akili na utashi na mara nyingi wananchi hao huwa wanajua iwapo Mahakama imewatendea haki au la.

Kadhalika Jaji Mfawidhi huyo aliwataka Mahakimu hao wapya kuendelea kuvaa vizuri na kuonekana nadhifu daima hata kama mazingira ni magumu na kusisitiza kuwa, kwa asili ya kazi ya uhakimu, unadhifu ni sehemu ya kazi hiyo na Mahakimu hawana budi kufuata maelekezo hayo.

Aliwatakia kila la kheri Mahakimu hao katika kazi zao na kuwakumbusha kuzingatia mambo makuu matatu ambayo ni uadilifu, uchapa kazi na kufahamu sheria pamoja na namna ya kuitumia kwa mujibu wa miongozo iliyopo na kuwasisitiza kuwa, wasisite kuomba ushauri au kuuliza wanapopata changamoto yoyote ya kikazi.

Vilevile, Mahakimu hao wamesisitizwa kujikita katika maarifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuendelea kujifunza mifumo ya kielektroniki inayotumika mahakamani ili kurahisisha kazi zao kwa sababu matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama ni moja ya vipaumbele kwa lengo la kuwezesha  na kurahisisha kazi za kimahakama. 

Mara baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Mugeta aliwagawia Kompyuta Mpakato Mahakimu hao ambazo ni vitendea kazi vyao.

Aidha, wamekumbushwa juu ya umuhimu wa kutunza vizuri kompyuta hizo walizopewa kama vitendea kazi, kwa sababu itakapotea uharibifu au upotevu wa vifaa hivyo watawajibika wao wenyewe.

Ikumbukwe kuwa, Mahakimu hao ambao ni ajira mpya waliripoti Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mwezi Desemba, 2024 ambapo wamekuwa wakifundishwa kazi kwa vitendo takribani kwa miezi mitatu na sasa wapo tayari kwa kuendelea na kazi katika Mahakama za Mwanzo walizopangiwa Mkoani Arusha.


Mahakimu ajira mpya wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufundwa na kuiva tayari kwa kufanya kazi. Kutoka kushoto ni Mhe. Eugene Nyalile, Mhe. Sekunda Mosha, Mhe. Zarina Nassoro na Mhe. Gospel Sanava.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta akitoa Kompyuta Mpakato kwa Hakimu Mkazi ambaye ni ajira mpya, Mhe. Eugene Nyalile, zoezi hilo lilifanyika tarehe 12 Machi, 2025 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, akimpatia Kompyuta Mpakato kwa Hakimu Mkazi ajira mpya, Mhe. Gospel Sanava tarehe 12 Machi, 2025 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha akitoa Kompyuta Mpakato kwa Hakimu Mkazi ajira mpya, Mhe. Sekunda Mosha tarehe 12 Machi, 2025.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta akitoa Kompyuta Mpakato kwa Hakimu Mkazi ajira mpya, Mhe. Zarina Nassoro tarehe 12 Machi, 2025 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni