Alhamisi, 13 Machi 2025

WANAFUNZI WA SEKONDARI YA TUNDUMA TOWN COUNCIL WANUFAIKA NA ELIMU YA SHERIA

Na Iman Mzumbwe – Mahakama, Songwe

Katika kusherekea siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake ambayo uadhimishwa tarehe 10 Machi kila mwaka. Mahakimu Wanawake Wilaya ya Momba Mkoa wa Songwe wamefanikiwa kutoa elimu ya Sheria katika Shule Sekondari ya Tunduma Town Council inayohusu makosa ya kimtandao yenye kauli mbiu isemayo; Haki katika zama za kidigitali Majaji na Mahakimu Wanawake katika kushughulikia makosa ya kimtandao’

Mahakimu hao, walitoa mada zilizoandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) zenye lengo la kuelimisha jamii juu ya Haki za msingi katika zama za kidigitali na kufafanua mchango wa Majaji na Mahakimu Wanawake katika kushughulikia makosa ya unyanyasaji wa ki-mitandao ya jamii.

Aidha, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama Wilaya Momba Mhe. Tagha Emmanuel Komba alitoa rai kwa wanafunzi wa shule hiyo ya sekondari kuto jihusisha na unyanyasaji wa kimtandao kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kushindwa kufikia malengo yao ya msingi.  Vilevile aliwaeleza wanafunzi hao kuwa wasisite kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo hivyo vya unyanyasaji ili kusaidia kupunguza uovu huo katika jamii.

Naye, Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Magreth Moses Kannonyele aliwasisitiza wanafunzi hao kuwa, watumie elimu hiyo kuielimisha jamii inayowazunguka juu ya unyanyasaji wa kidigitali, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia watu wengi kutambua aina ya makosa hayo kwani yakibainika huzaa kosa la kijinai linaloweza kupelekea kifungo au faini wakati mwingine vyote viwili kwa pamoja.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Tunduma Mhe. Demetria Simon alisema kuna watu wanafanya unyanyasaji wa kimtandao bila kujua ni kosa kisheria ndiyo maana ya kutoa elimu kwenu ili iwe chachu ya kuwaelimisha watu wengine kutambua umuhimu wa kutotenda makosa ya aina hiyo.

Mahakimu hao wanawake walioshiriki katika zoezi la utoaji elimu walikuwa Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama Wilaya Momba Mhe. Tagha Emmanuel Komba, Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Magreth Moses Kannonyele pamoja na Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Tunduma Mhe. Demetria Simon.

Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Tagha Emmanuel Komba  (mwenye suti bluu) akielizea juu ya unyanyasaji wa kimtandao unavyoathiri watoto katika jamii.

Sehemu ya Wanafunzi wa Shule Sekondari ya Tunduma Town Council iliyopo mjini Tunduma wakifualitia kwa makini elimu ya kisheria iliyotolewa na Mahakimu Wanawake katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake. 

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Tagha Emmanuel Komba (mwenye suti ya bluu) akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Wilaya Momba Mhe. Magreth Moses Kannonyele (mwenye suti nyeusi) akielizea juu ya unyanyasaji wa kimtandao unavyoathiri watoto katika jamii.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni