Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Wanafunzi wapatao 20 wa Shule ya Sekondari Bulonge wametembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma tarehe 12 Machi, 2025 ili kupata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya kisheria ikiwemo haki za binadamu.
Wakitoa elimu kuhusu namna Mahakama nchini zinavyofanya kazi, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola na Mhe. Victor Kagina waliwaeleza wanafunzi hao juu ya haki za msingi za binadamu zinazopatikana katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na namna Mhimili wa Mahakama unavyoshiriki katika kulinda haki hizo.
Katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi Mahakama ya wazi uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Msola aliwafundisha ni jinsi gani Mahakama inatoa fursa kwa mtu ambaye hajaridhika na uamuzi wake kwa ngazi fulani anaweza kukata rufaa kwenda Mahakama ya juu yake.
Alisema kuwa; kwa Mahakama za Mwanzo zote, rufaa zake hupelekwa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Wilaya rufaa zake hupelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania na vilevile Mahakama Kuu rufaa zake huwasilishwa Mahakama ya Rufani ili kutoa haki iliyokosekana kutolewa kwa Mahakama za chini.
“Kupitia mlolongo huo, mwananchi anayo fursa kubwa ya kutafuta haki aliyonyimwa na kwa namna hiyo Mahakama inashiriki kikamilifu katika kulinda haki za binadamu pale zinapokuwa zimevunjwa katika uamuzi uliotolewa na Mahakama za chini,” alisisitiza Mhe. Msola.
Aliongeza kuwa, mwananchi anaweza pia kufungua shauri dhidi ya Serikali kutokana utendekaji wa jambo fulani ambalo mwananchi huyo anaona limekiuka sheria za nchi, hivyo Mahakama kama mhimili wenye jukumu la kutafsiri sheria huwajibika kutoa uamuzi wenye haki hata kama miongoni mwa washtakiwa ni Serikali.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Sheria, Mhe. Victor Kagina aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujituma huku wakikuwa katika maadili ya kuwa viongozi wasomi katika kada mbalimbali wanazopenda kusomea.
Aidha, aliwakaribisha katika tasnia ya sheria kwani ni miongoni mwa tasnia mahsusi katika kulinda na kutetea haki za binadamu katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, na kuwasisitiza kusoma na kufaulu vizuri ili kuweza kupata fursa ya kufika elimu ya juu katika masomo yao ili kuja kuwa viongozi wenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Walipopewa fursa ya kuuliza maswali, Mwanafunzi Bi. Khadija Matokeo alihoji kama inawezekana kwa mwananchi kukosoa utendaji kazi wa Serikali pale unapokuwa hauridhishi.
Akijibu swali hilo Mhe. Msola alisema ni haki ya kila mwananchi kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania kuwa na uhuru wa maoni, hivyo mwananchi anaweza kuhoji, kukosoa na hata kupendekeza namna bora ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.
Akizungumza juu ya nia yao ya kujifunza kupita Kazi Mradi (School Project) Kiongozi wa Wanafunzi hao, Seleman Mrisho alibainisha kiu waliyokuwa nayo kujifunza masuala ya kisheria hususani Haki za Binadamu ambapo alisema, “tunapenda kufahamu kuhusu haki za binadamu na shughuli zinazofanywa na Mahakama kulinda haki hizo.”
Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola akisisitiza jambo wakati alipokuwa akifundisha wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Bulonge tarehe 12 Machi, 2025 katika ukumbi wa Mahakama ya wazi uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina akifufunua jambo wakati alipokuwa akifundisha wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Bulonge waliotembelea Mahakama hiyo.
Mwanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari Bulonge, Bi. Khadija Matokeo akiuliza swali kwa Mhe. Valerian Msola alipokuwa akifundisha wanafunzi hao katika ukumbi wa Mahakama ya wazi uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni