- Chaadhimisha miaka mitatu tangu kianzishwe
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama,
Dodoma
Kituo cha Huduma kwa Mteja
cha Mahakama ya Tanzania, leo tarehe 21 Machi, 2025 kimeadhimisha miaka mitatu
tangu kuanzishwa kwake, huku kikibainisha mafanikio makubwa yaliyofikiwa,
ikiwemo kupokea na kushughulikia mrejesho kwa asilimia 100.
Maadhimisho hayo
yamehudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisate Ole
Gabriel, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Eva Nkya, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo na Watumishi wa Kituo hicho.
Akizungumza kwenye
maadhimisho hayo, Mtendaji Mkuu amewapongeza Watumishi wa Kituo hicho kwa kazi
nzuri wanayofanya ya kuwahudumia wateja kwa ubora na weledi wa hali ya juu na
kukifanya Kituo kuwa Daraja kati ya Mahakam ana Wananchi.
‘Wapo Viongozi, Mabalozi
wengi sana ambao wameshapata huduma kutoka kwa Wataalam wetu wa Kituo cha
Huduma kwa Mteja. Yupo Balozi mmoja, alikuwa na suala lake fulani,
tukamwelekeza Call Centre. Yule Balozi alinipigia simu akaniuliza hao vijana waliomhudumia
kama ni Watanzania, au tuliwapata wapi. Hii inatufariji kwamba mnafanya kazi
nzuri sana,’ amesema.
Mtendaji Mkuu amesema kuwa
huduma bora zinazotolewa katika Kituo hicho zinaongeza imani ya Wananchi kwa Mahakama
ya Tanzania, hasa baada ya kupokea simu 7,143, ikimanisha kuwa ndani ya siku
moja wapo Watanzania wastani wa 150 ambao wangekuwa wanakosa kuhudumiwa na wasingeweza
kufanya shughuli zingine za kiuchumi.
‘Hawa ni watu ambao pengine
familia zao zingeweza kuwa katika matatizo, lakini pale ambapo mmeweza
kuwasikiliza na kuwapa majibu wanakuwa wamebadilisha ule msimamo wao. Kituo hiki
vile vile kimekuwa kikisaidia sana mawasiliano na Wananchi,’ amesema.
Akizungumza wakati wa
maadhimisho hayo, Msajili Mkuu ameeleza kuwa kuwepo kwa Kituo cha Huduma kwa
Mteja ni dhamira ya Mahakama ya kuimarisha na kuboresha huduma zinazotolewa
kupitia mrejesho, maoni, malalamiko na masuala mbalimbali yanayohusu huduma za
Mahakama.
‘Kwetu Watumishi wa
Mahakama, Kituo hiki kinatukumbusha juu ya kusimamia misingi ya utumishi na
kutekekeleza Mkataba wa Huduma kwa Mteja,’ ameeleza.
Mhe. Nkya amebainisha
kwamba kwa muda wa miaka mitatu, Kituo hicho kimepokea mrejesho takribani 7000
kutoka kwa Wananchi kuhusiana na mambo mbalimbali.
‘Ni jambo la kujivunia
sana kuwa juhudi hizi zimeleta matokeo chanya katika kuimarisha imani ya
Wananchi kwa Mahakama. Taarifa ya Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa Huduma
za Kimahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili inaonesha malalamiko mahakamani
yamepungua sana,’ amesema.
Naye Naibu Msajili na Mkurugenzi
wa Usimamizi na Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili,
Mhe. Maira Kasonde, akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, aliwapongeza Watumishi
wa Kituo kwa kuwa wabunifu na shirikishi.
‘Kituo cha Huduma kwa
Mteja ndani ya kipindi husika kimekuwa siyo tu jicho, bali pia sikio la
Mahakama. Kupitia Kituo hiki, Mahakama imesikia sauti ya Wananchi, tumejua nini
Wananchi wanasema kuhusu huduma tunazozitoa na tumejua wapi ambapo tumefanya
vizuri na wapi tunahitaji kuboresha,’ alisema.
Alibainisha kuwa ndani ya
miaka mitatu, Kituo hicho kimetumiwa na Mahakama kama kioo ambapo kila mtumishi,
idara na kitengo kimeweza kupata nafasi ya kujiona, kujiangalia na kuona dosari
iliyopo na kuwa tayari kuirekebisha.
‘Kwa namna ya kipekee,
Kituo hiki kimekuwa Daraja kati ya Mahakama na Wananchi. Tumewashirikisha Wananchi
katika utoaji wa huduma zetu kupitia kupokea maoni na mapendekezo yao na hivyo
kutufanya tujue wapi tunahitaji kuboresha ili tuweze kusonga mbele,’ alisema.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Kituo hicho. Hakimu Mkazi Mkuu na Mtalaam wa Kuchakata Taarifa katika Kituo hicho, Mhe. Domician Mlashani alieleza kuwa Kituo kimefanikiwa kushughulikia mirejesho yote iliyosajiliwa tangu kianzishwe.
Alieleza kuwa hadi tarehe
28 Februari ,2025, jumla ya mirejesho 6,948 ilikuwa imeshughulikiwa na kufungwa,
hii ni sawa na asilimia 100.
Mhe. Mlashani alieleza
mafanikio mengine kama wateja wa Mahakama kupunguziwa gharama, muda pamoja na
kuongezeka kwa uwazi katika kuwasilisha na kufuatilia malalamiko yao, kufuatia
uwepo wa namba ya bure (0800 750247) inayopatikana muda wote.
‘Kituo kimefanikiwa
kutembelewa na wageni mbalimbali wa kitaifa na kimataifa waliokuja kujifunza
namna tunavyofanya kazi. Tumepokea ugeni kutoka Mahakama ya Msumbiji, Mahakama
ya Uganda, Mahakama ya Zanzibar, Maktaba Kuu ya Taifa ya Tanzania, Wizara ya Katiba
na Sheria na Jeshi la Polisi, wote wakija kujifunza namna tunavyofanya kazi,’
alisema.
Mhe. Mlashani alieleza
pia kuwa Kituo kimefanikiwa kutembelea Magereza mbalimbali, kuwasikiliza na
kupokea mirejesho kutoka kwa wafungwa na mahabusu ambao ni wadau wa haki jinai.
Katika kipindi cha miaka
mitatu, kituo kilitembelea Magereza kumi ambayo ni; Ukonga, Keko, Segerea (Dar
es Salaam), Luanda (Mbeya), Karanga (Moshi), Uyui (Tabora) Butimba (Mwanza),
Kisongo (Arusha), Maweni (Tanga) na Isanga (Dodoma).
Mhe. Mlashani alieleza
pia kuwa kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanyika na yanayoendelea
kufanyika mahakamani, mirejesho ya Wananchi kwa kipindi cha miaka mitatu
inaonyesha baadhi ya maeneo malalamiko yamekuwa yakipungua kwa kiasi kikubwa.
Maeneo hayo ni yale
yanayohusu kama ifuatavyo upatikanaji wa nakala za hukumu na mwenendo wa
mashauri, utoaji wa hati za kimahakama kwa kutumia teknolojia, utoaji wa vitabu vya rufaa za Mahakama ya
Rufani, dhamana, muda wa kuanza shughuli za kimahakama na maadili juu ya
Maafisa wa Mahakama.
Hakimu Mkazi Mkuu na Mtalaam wa Kuchakata Taarifa katika Kituo cha Huduma kwa Mteja, Mhe. Domician Mlashani akiwasilisha taarifa ya Kituo hicho.
Kiongozi Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Bi. Evetha Mboya-wa kwanza kushoto-akitambulisha Viongozi mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo. Wengine katika picha ni Watumishi wa Kituo hicho ambao ni Mahakimu Wakazi.
Watumishi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania wakitambulishwa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel-katikati-akikata keki kwenye maadhimisho hayo. Picha chini ni muda wa shampaign.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni