- Yakabidhi Magereza makasha 10 ya Mahakama Mtandao
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Mahakama ya Tanzania leo
tarehe 21 Machi, 2025 imekabidhi makasha maalumu ya kisasa yatakayotumika
kwenye Magereza mbalimbali nchini kuendesha mashauri kwa njia ya mtandao bila
washitakiwa na wafungwa kufikishwa mahakamani.
Makasha hayo 10 yamekabidhiwa
na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel kwa
Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katundu kwenye tukio la kihistoria lililohudhuriwa
na Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, ambaye ndiye alikuwa Mgeni
Rasmi, pamoja na Viongozi wengine Waandamizi wa Mahakama, akiwemo Msajili Mkuu,
Mhe. Eva Nkya na Jeshi la Magereza.
Akizungumza katika tukio
hilo, Waziri Bashungwa amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Viongozi na Mahakama
kwa ujumla kwa juhudi za kuleta mabadiliko chanya kupitia Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano-TEHAMA.
Amewapongeza pia Jeshi la
Magereza kwa kupatiwa makasha hayo na Mahakama ya Tanzania, huku akibainisha
kuwa kutumika kwa makasha hayo itakuwa Daraja linalounganisha Mahabusu na haki
na kusaidia kupunguza gharana za usafiri na maahirisho ya mashauri ambayo
yangeweza kutokea kutokana na kutokufikishwa kwa Mahabusu mahakamani.
Amesema vile vile kuwa
Mahakama Mtandao inarahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama, kuokoa
gharama za uendeshaji, kupunguza msongamano wa Wananchi mahakamani na kuwezesha
Mawakili kupata rejea za hukumu na nyaraka mbalimbali kwa urahisi.
Waziri Bashungwa amesema
pia kuwa Mahakama Mtandao inasaidia kuwabaini Mawakili vishoka ambao wamekuwa
wakiharibu mwenendo wa kesi mbalimbali, ulinzi wa taarifa na nyaraka na kuokoa muda wa Wananchi
katika utafutaji wa haki na badala yake muda mwingi wanautumia katika shughuli
za uzalishaji, hivyo kuchangia ukuaji wa Uchumi wa Nchi.
‘Ni matumaini yangu
makasha haya yatatumika kwa lengo lililokusudiwa na kusaidia ufanisi katika
Nyanja za utendaji haki nchini. Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama
kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa usawa kwa kila Mtanzania,’
amesema.
Akizungumza katika tukio
hilo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama amesema kuwa kasha hilo ni moja kati ya makasha
10 yaliyotolewa kwa Jeshi la Magereza lengo likiwa kuimarisha mnyororo wa
utoaji haki nchini.
Amesema kuwa makasha kama
hayo yamepokelewa katika Magereza ya Ukonga, Segerea na Keko katika jijini la Dar
es Salaam, Gereza la Uyui Tabora, Isaranga Moshi, Ruanda Mbeya, Maweni Tanga, Butimba
Mwanza Ruanda, Kisongo Arusha na Isanga
Dodoma.
Prof. Ole Gabriel
ameeleza kuwa makasha hayo yatasaidia kuboresha kazi za Mahakama na magereza, kwani
Hakimu hatakuwa na haja ya kuwapokea wafungwa au mahabusu, Jaji akiwa Mwanza au
Bukoba anaweza kumsikiliza mfungwa bila kusafiri au mshtakiwa kupelekwa
mahakamani.
‘Hili litasaidia kuokoa
muda na kusaidia sana katika masuala ya kiusalama kwa baadhi ya wafungwa, hasa
wale hatarishi,’ alisema.
Aliwaomba Wadau wengine
washiriki kuchangia na kuwezesha jambo hilo kwani nia ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Luluhu Hassan ni kuona haki inatendeka
kwa haraka na mwenye haki apate haki.
Kwa upande wake, Kamishna
Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu ameupongeza Uongozi wa Mahakama
kwa maboresho makubwa ambayo yemefanyika, hali ambayo imesaidia usikilizaji wa
mashauri kwa wakati na Kuharakisha upatikanaji wa haki.
Amesema kuwa hatua hiyo
imesaidia kupunguza msongamano wa Mahabusu na Wafungwa katika Magereza. ‘Tunayo
jumla ya Magereza 129 Tanzania Bara yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya Wahalifu 29,902
kwa siku. ‘Kwa tarehe ya leo, jumla ya wahalifu waliopo magerezani ni 26,917,
kati yao 19,528 ni wafungwa na mahabusu 7,389…
‘Idadi ya wahalifu
iliyopo magerezani ndogo ikilinganishwa na uwezo wa Magereza kuhifadhi
wahalifu. Haya ni matokeo ya uboreshaji wa huduma wa haki jinai unaofanywa na
Serikali ya Awamu ya Sita na ushirikiano mzuri wa vyombo vyote vilivyopo katika
mnyororo wa haki jinai, ikiwemo Mahakama,’ amesema.
Kamishna Jenerali ameishukuru
Mahakama ya Tanzania kwa kuwezesha Mahakama Mtandao katika Magereza ambapo takribani
Magereza 69 nchini yana huduma ya Mahakama Mtandao.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya Makasha hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni