- Washangazwa na maendeleo pamoja na matumizi makubwa ya TEHAMA katika uendeshwaji wa Mashauri
- Wadhamiria kuanzisha na kuimarisha mahusiano na Mahakama ya Tanzania
Na NAOMI KITONKA, Mahakama- Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amepokea wageni kutoka
nchini Japan waliokuwa katika ziara yao ya kikazi katika Ubalozi wa Japan hapa
nchini jana tarehe 20 Machi 2025 katika jengo la Mahakama ya Rufani.
Ziara hiyo ilifanyika ikiwa na lengo la kuanzisha
mahusiano na kuangalia fursa mpya nchini kwa kukutana na wataalamu wa masuala
ya sheria wa Tanzania na kuelezea mchango wa Japan katika kuendeleza rasilimali
watu na sheria katika nchi nyingine.
Akizungumza katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alifungua kwa kusema, “Tunayo furaha
kubwa kuwakaribisha nchini Tanzania kipekee katika Mahakama yetu ya Tanzania
ambayo ni Mhimili muhimu katika kuwapatia haki wananchi na ujio wenu utakuwa
fursa kubwa ya kuimarisha mahusiano kati yetu.”
Prof. Ole Gabriel alisema Mahakama ya Tanzania kwa sasa
imepiga hatua kubwa katika shughuli zake kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili
Tanganyika (TLS) na Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) pamoja na Idara ya Mafunzo kuhakikisha Maafisa wote wa Mahakama
pamoja na watumishi wengine wanajengewa uwezo binafsi katika utafiti na mafunzo
yatakayowasaidia katika kukamilisha majukumu ya Kimahakama kwa haraka na ubora.
Aidha, katika mazungumzo hayo, wageni hao walipata
ufafanuzi juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania hasa
katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika
usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao, Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri (eCMS)
na Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia zoezi
la upatikanaji haki kwa haraka.
“Mahakama ya Tanzania tumedhamiria kuhakikisha wananchi
wanapata haki kwa ubora, haraka na kwa wakati, wakati mwingine bila hata kuwa
na ulazima wa kufika mahakamani kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia
huku ikikumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na suala la rushwa,”
alisema.
Mtendaji Mkuu aliongeza kuwa, mabadiliko ya TEHAMA na
kupitia ujio wa wageni hao anatumaini utawezesha kupunguza tofauti ya TEHAMA
kati ya Mahakama na wadau wake wakubwa mfano Jeshi la Polisi na Jeshi la
Magereza kwa sababu Japani wapo mbele zaidi katika maendeleo ya Sayansi na
Teknolojia na wanatambua mchango mkubwa wa matumizi yake katika zoezi la utoaji
haki pamoja na usuluhishi.
“Pia hii itasaidia utamaduni wa Mahakama kujulikana kwa
wananchi katika kipindi hiki na kuwatoa wasiwasi hasa katika matumizi ya
mtandao na mifumo katika ufunguaji wa mashauri na matumizi ya akili mnemba yaani
(AI) na kuwa katika daraja la kwanza kwenye matumizi ya Teknolojia” alisisitiza
Prof. Ole Gabriel.
Wageni hao waliongozwa na Mkuu wa Msafara huo, Bw. Ryota
Tatemoto ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na
Taasisi ya Utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Katiba ya nchini Japan.
“Ofisi yetu inahudumia nchi zaidi ya 10 za Kiasia na
tumeona ni muhimu kuanza kutoa huduma zetu kwa kushirikiana na nchi nyingine
katika nchi za Afrika na kuanzisha ushirikiano wa Kimahakama na fursa hiyo
tukaiona nchini Tanzania na huu ni wakati mzuri wa sisi kujifunza kutoka kwenu
nanyi kujifunza kutoka kwetu hasa katika ushirikiano wa Mafunzo na Utafiti
pamoja na kubadilishana uwezo katika utendaji kazi wetu,” alisema Bw. Tatemoto.
Wageni hao kutoka Japan waliambatana na Mwakilishi
kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Regina
Ulomi aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa jitihada kubwa inayofanya katika
zoezi la utoaji haki.
Kadhalika Bi. Regina alizungumzia kuhusu majukumu ya
Wizara hiyo ambapo alisema, “Kazi yetu sisi kama Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni kuhakikisha
fursa zote za kimaendeleo zinapelekwa katika sehemu husika na wageni
hawa wamelenga Mahakama ya Tanzania ili kujifunza na kubadilishana uzoefu
kwenye masuala ya Kimahakama, matumizi ya Teknolojia, kujengeana uwezo, utafiti,
mafunzo pamoja na kujifunza njia mbalimbali za usuluhishi.
Ziara hiyo ilihudhuriwa pia na Bw. Kazuaki Takahashi, Jaji
na Mwendesha Mashtaka kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Taasisi ya
utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Katiba ya Japan, Bw. Rui Higuchi, Katibu wa
Tatu kutoka Ubalozi wa Japan, Bi. Yoshino Shibata, Msajili wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Herbert George na Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo upande wa
Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Taasisi ya Utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Katiba ya Japan, Bw. Ryota Tatemoto wakati wa ziara yao walipomtembelea Mtendaji Mkuu ofisini Mahakama ya Rufani Dar es Salaam jana tarehe 20 Machi 2025.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo wakati wa ziara ya wageni kutoka Ubalozi wa Japan na Wizara ya Katiba ya Japan walipomtembelea Ofisini kwake jana tarehe 20 Machi, 2025.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu akitoa ufafanuzi wa shughuli zinazofanywa na Idara ya Mafunzo kwa wageni kutoka Japan waliofanya ziara ya kumtembelea Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Regina Ulomi (kulia) akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mbele ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha) walipomtembelea ofisini kwake tarehe 20 Machi 2025.
Wageni kutoka Wizara ya Katiba ya Japan wakimsikiliza kwa makini Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha) wakati wa ziara yao walipomtembelea katika ofisi yake ndogo Mahakama ya Rufani Dar es Salaam jana tarehe 20 Machi, 2025.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akipokea zawadi kutoka kwa Bw. Ryota Tatemoto ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Taasisi ya utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Katiba ya Japan wakati wa ziara yao kwa Mahakama ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Ryota Tatemoto (wa pili kushoto) ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Taasisi ya utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Katiba ya Japan (wa pili kushoto), wengine ni Maafisa kutoka Wizara ya Katiba ya Japan.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Wizara ya Katiba ya Japan pamoja na sehemu ya Viongozi wa Mahakama walioshiriki katika mazungumzo na ugeni huo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni