Ijumaa, 21 Machi 2025

WATUMISHI WA MAHAKAMA WANAOTARAJIA KUSTAAFU WAPATA ELIMU YENYE MATUMAINI

Na ASHA JUMA- Mahakama, Morogoro.

Mafunzo yanayotolewa kwa Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wanaotarajia kustaafu yameendelea kwa Wawezeshaji kuwapatia elimu ya menejimenti ya mafao ya hitimisho la ajira, ushughulikiaji sahihi wa mirathi na suala zima la mafao na pensheni.

Wakitoa mada katika mafunzo hayo yanayotarajia kufika ukomo kesho tarehe 22 Machi, 2025, Ofisa Mwandamizi wa Mfuko wa NSSF, Bw. Fredrick Mossi na Ofisa Mwandamizi wa Mfuko wa PSSSF, Bw. Charles Mahanga, kwa nyakati tofauti walielezea namna Mifuko hiyo inavyofanya kazi.

Wameeleza namna salama ya uwekezaji, fursa zilizopo kwenye mifuko hiyo zinazosaidia  kuweza kujiendeleza  na kuendesha shughuli mbalimbali za uchumi kama vile nyumba za gharama nafuu, viwanja ambavyo vipo maeneo mbalimbali nchini.

Kadhalika, walielezea aina za pensheni kama pensheni za ulemavu, urithi, na uzee ambayo hulipwa kulingana na uwekezaji wa Mtumishi.

Watoa mafunzo hao pia walielimisha Watumishi umuhimu wa maandalizi kabla ya kustaafu, kwani mchakato wa kufikia hatua hiyo unahitaji maandalizi ya kina na ya muda mrefu ya kiuchumi, kisaikolojia, kijamii na kiafya. Wakufunzi walishauri kuwa muda wa kujiandaa kustaafu ni angalau miaka 20 hadi 30.

Katika mwendelezo wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Business Online HR Consultants, Bw. James Rhombo alitoa elimu kwa wastaafu hao kuhusu uzoefu katika masuala ya ujasiriamali na maisha baada ya kustaafu. Pia aliwaasa washiriki wa mafunzo kujali afya zao na kuzingatia wapi na kitu gani cha kuwekeza ili waendelee kiuchumi.

Mkufunzi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Kweka aliwafundisha washiriki namna sahihi ya kuishi kwa kuzingatia afya zao kwa kupima kila mara, mwenendo wa magonjwa yasiyo ambukiza kama kisukari, presha na kuzingatia ulaji kulingana na shughuli wanazofanya.

Mtaalamu huyo pia aliwaasa Watumishi kufanya mazoezi na kuchangamana na watu, hatua itakayosaidia kujenga afya kimwili, kiakili, kijamii, kihisia na kiroho na kuwaomba pia wachangamane na watu ili wasiwe wapweke, hasa baada ya kustaafu.

Watumishi pia wamepewa elimu ya mifuko ya uwekezaji wa UTT-AMIS ambapo mafunzo hayo yametolewa na Ofisa Mwendeshaji Mkuu, Bw. Ahmed Mabruk ambaye alielezea kuhusu hisa na vipande katika uwekezaji. Alieleza kuwa vipande ni sehemu ya umiliki katika uwekezaji wa pamoja na hisa ni sehemu ya umiliki katika kampuni fulani.

Bw. Mabruk alieleza kuwa kuna aina nyingi za kuwekeza katika Mfuko wa UTT-AMIS ambazo ni uwekezaji mseto, umoja, watoto, jikimu na bondi ambapo aliwashauri kuwekeza kwani ni rahisi kwa wastaafu.

Viongozi wa Kiroho  nao  hawakubaki nyuma katika kuwapa chakula cha kiroho Watumishi hao ambapo Mchungaji Protas Makimu alifundisha masuala ya imani, ustawi wa jamii na kiroho. Mchungaji Makimu aliwaasa kujiweka mikononi mwa Mungu akisema, “Tukimtegemea yeye tutaendelea kuwa washindi kila siku na rehema zake zitaendelea kila siku kwani tunaishi kwa huruma yake.”

Kwa upande wa Sheikh wa Mkoa wa Morogorp, Twaha Kilango aliwaasa Watumishi kuwa wanapaswa kumtumikia Mungu ipasavyo, ikibidi waombe hata nafasi ya uongozi kwenye Imani zao za kidini kama Kanisani au Msikitini na kutoa sadaka zao ili waweze kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu.

Ofisa Mwandamizi wa mfuko wa NSSF, Bw. Fredrick Mossi na Ofisa Mwandamizi wa Mfuko wa PSSSF, Bw. Charles Mahanga na wawezeshaji wa mifuko hiyo wakiwa pamoja na washiriki wa mafunzo.

Mkurugenzi wa Business Online HR Consultants, Bw. James Rhombo akitoa elimu elimu na kubadilishana nao uzoefu kwa washiriki.

Mkufunzi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Kweka  akiwafundisha kuhusu Afya.

Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa UTT-AMIS, Bw. Ahmed Mabruk akiwafundisha washiriki namna ya kujiwekeza kwenye mifuko mbalimmbali.

 

Viongozi wa Dini wakiwa pamoja na washiriki.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni