Jumatatu, 24 Machi 2025

MAFUNZO KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA WANAOTARAJIA KUSTAAFU YAHITIMISHWA

Na ASHA JUMA -Mahakama, Morogoro

Mafunzo maalum kwa Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wanaotarajia kustaafu yaliyokuwa yanafanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani hapa yalijitimswa tarehe 22 Machi, 2025.

Mafunzo hayo yalizinduliwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga tarehe 17 Machi 2025 na kufungwa na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Bw. Kategere aliipongeza Mahakama kwa mpango mzuri wa kuwakutanisha Watumishi wanaotarajia kustaafu na kuwafundisha mbinu mbalimbali za namna ya kuishi na kuanza maisha mapya baada ya kumaliza utumishi wa umma.

Aliwaasa washiriki kuwa karibu na jamii kwa kusema “Endelezeni mahusiano mazuri katika jamii kwa kuepuka visasi, migogoro na pia kufanya ibada za mara kwa mara. Kumbukeni kuwa fedha za kustaafu ni nyingi kama zikitumiwa kwa mpangilio mzuri, lakini endapo hazitatumiwa vizuri zitakwisha ghafla na kusababisha misongo ya mawazo”.

Bw. Kategere pia aliwaasa Watumishi hao na wengine kuwa wasisahau kuwekeza kidogo kidogo kwani hii itawasaidia katika kuishi maisha bora kabla na baada ya kustaafu.

Kustaafu utumishi wa umma sio adhabu kama ilivyofundishwa na kuelekezwa na wawezeshaji, bali kustaafu ni fursa ya kuanza maisha mengine mapya ambayo yanatakiwa kuwa bora zaidi na ya utulivu,’ alisema.

Washiriki wa mafunzo hayo watoka kada mbalimbali, wakiwemo Watendaji wa Mahakama, Wakurugenzi Wasaidizi, Mahakimu, Wasaidizi wa Kumbukumbu, Madereva, Wahasibu, Walinzi, Wasaidizi wa Ofisi na Waandishi Waendesha Ofisi.

Mafunzo yalijumuisha mada muhimu kama taratibu za kisheria za maandalizi ya kustaafu, stahiki za mtumishi, ujasiriamali, menejimenti ya mafao, usimamizi wa mirathi, bima ya afya baada ya kustaafu, afya ya akili, mbinu za kukabiliana na msongo wa mawazo, mifuko ya uwezeshaji na mambo ya kiimani.

Mada hizo zilitolewa na Wataalamu kutoka PSSSF, NSSF, NHIF, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na wataalam wa uwekezaji.

Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.


 
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Bi.Beatrice Patrick -kushoto na Mkurugenzi Msaidizi, Bi. Agnes Kavishe wakiwa kwenye mafunzo hayo.

 

Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. VictOR Kategere-katikati waliokaa-ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo-juu na chini.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni