- Watumishi wasisitizwa kujiunga
Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama amewataka watumishi wa Mahakama ya Mkoa na Wilaya za Makete, Wanging’ombe na Ludewa mkoani Njombe kujiunga na Mfuko wa Jamii wa Mahakama hiyo wenye lengo la kusaidiana.
Mhe. Chamshama aliyasema hayo jana tarehe 27 Machi, 2025 katika Kikao cha Menejimenti ya Mahakama hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.
"Mtumishi hapa akipatwa na tatizo la ghafla hata nauli hana inakuwa haueni pesa ikatolewa kwenye mfuko na kupatiwa mtumishi ili aweze kusafiri kuliko kusubiri achangiwe pesa," alisema Mhe. Chamshama.
Alisema kuwa, Mfuko huo ni muhimu kwakuwa utakuwa na katiba ambayo itaainisha jinsi wanachama watakavyojiunga na kunufaika na mfuko huo ambao michango yake itawekwa kwenye mfumo wa kimtandao wa 'M-koba'.
Mhe. Chamshama aliwasisitiza watumishi kutosuasua kujiunga na chama hicho kwani chama hicho ni faida kwao watumishi wenyewe pindi wanapopatwa na majanga ya kifamilia haswa kwenye suala la kufiwa na mzazi, mke, mume au mtoto.
Sambamba na hilo, Mfawidhi huyo aliwakumbusha watumishi kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuwataka kila Mahakama ya Wilaya za mkoani Njombe zitenge bajeti kwa ajili ya vifaa vya TEHAMA ili watumishi waweze kutumia mifumo iliyopo ndani ya Mahakama kwa ufanisi.
Aidha, Mhe. Chamshama aliwataka watumishi kuwa na tabia ya kuwahi kazini pamoja na kuwa na nidhamu wawapo kazini na maeneo ya nyumbani wanakoishi.
Naye Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe akizungumza na Maafisa wa Mahakama alisema washirikiane kuendelea kutafuta viwanja katika maeneo mbalimbali kwa maana kila Kata inatakiwa iwe na Mahakama ya Mwanzo hili viwanja hivyo viweze kutafutiwa hati wakati mchakato wa ujenzi ukiwa unaendelea.
Bw. Mbambe alitoa pongezi kwa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe kwa kutafuta kiwanja kikubwa ambacho itajengwa Mahakama ya Mwanzo.
Kadhalika, Mtendaji huyo aliwakumbusha watumishi kujijengea tabia ya kufanya mazoezi ili kuepuka maradhi mbalimbali ya kibinadamu na kuwajuza kuwa katika siku zijazo za karibuni kutakuwa na ratiba ya kufanya mazoezi angalau mara mbili au tatu kwa wiki kwa watumishi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya pamoja na Maafisa wa Mahakama hizo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama (kulia) akizungumza jambo na Mahakimu na Watumishi wengine wa Mahakama hiyo (hawapo katika picha) wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama hiyo kilichofanyika jana tarehe 27 Machi, 2025 katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe. Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Wanging’ombe Mhe.James Muhoni (kulia) pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Makete (kushoto) wakisikiliza kwa makini kilichokuwa kikiendelea katika Kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe kilichofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo.
Baadhi ya Mahakimu na Maafisa wa Mahakama Njombe wakifuatilia kinachojiri katika kikao cha Menejimenti kilichofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama (kulia) pamoja na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe (kushoto) wakisikiliza maswali/hoja zilizokuwa zikitolewa na wajumbe wa kikao hicho.
Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya, Bi. Advera Kalunde (aliyesimama) akichangia hoja iliyoibuliwa kwenye kikao hicho. Walioketi ni sehemu ya wajumbe walioshiriki katika kikao hicho.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni