- Wabunge wakoshwa na Mtendaji Mkuu kwa uchapakazi
Na ARAPHA RUSHEKE na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Mahakama ya Tanzania imeendelea
kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo ili
kusogeza huduma karibu na Wananchi na kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri,
hivyo kuwezesha upatikanaji wa haki kwa haraka na gharama nafuu.
Akiwasilisha bungeni hotuba
ya Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026
jijini Dodoma leo tarehe 30 Aprili, 2025, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt.
Damas Ndumbaro amesema kuwa kwa kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025
kulikuwa na jumla ya mashauri 238,154 mahakamani.
Mhe. Dkt. Ndumbaro
amebainisha kuwa kati ya mashauri 238,154 yaliyokuwepo, mashauri 174,581
yalisikilizwa na kuhitimishwa na mashauri 63,573 yanaendelea katika hatua
mbalimbali.
‘Mashauri yenye umri
mrefu mahakamani ni 2,780, sawa na asilimia 4 ya mashauri yote yaliyobaki. Mashauri
1,325 yapo Mahakama ya Rufani; 189 yapo Mahakama Kuu; 553 yapo Mahakama za
Hakimu Mkazi na Wilaya na 713 yapo Mahakama za Mwanzo…
‘Pia, katika Mahakama Kuu
Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jumla ya mashauri 59 yalibakia
mwishoni mwa Juni 2024, 118 yalisajiliwa, 108 yalisikilizwa na 69 yalibakia,’
amesema.
Waziri wa Katiba na
Sheria ameliambia Bunge pia kuwa Mahakama ya Tanzania imeendelea kushirikiana
na Wadau wake katika mnyororo wa haki jinai ili kuhakikisha mashauri
yanamalizika kwa wakati.
Amebainisha kuwa tarehe
06 Aprili, 2025 Mahakama iliitisha kikao kazi cha pamoja kilichohusisha Wadau
kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia
Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Wadau wengine
waliohudhuria kikao hicho ni Chama cha Mawakili Tanganyika, Idara ya Ustawi wa
Jamii, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya.
‘Kupitia kikao hicho,
wajumbe walijadili taarifa ya hali ya mashauri ya mlundikano mpaka kufikia
Desemba -2024, hali ya mahabusu magerezani na mkakati wa kupunguza mlundikano
na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA-kwenye usikilizaji wa
rufaa na maombi.
Akizungumzia uteuzi wa
Majaji, Waziri Ndumbaro ameliambia Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025,
jumla ya Majaji 10 wameteuliwa (Mahakama Kuu – 5 na Mahakama ya Rufani – 5) na
hivyo kufanya idadi ya Majaji waliopo kufikia 146 (Mahakama Kuu – 107 na
Mahakama ya Rufani - 39).
Vilevile, Waziri wa
Katiba na Sheria ameeleza kuwa Mahakimu 91 wameajiriwa na hivyo kufanya idadi
ya Mahakimu kufikia 1,426 (Mahakama za Mwanzo - 195 na Mahakama za Hakimu Mkazi
- 1,231).
Kuhusu miundombinu ya majengo,
Bunge limefahamishwa kuwa Mahakama ya Tanzania imeendelea na utekelezaji wa
Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama wa Miaka Mitano
(2021/2022 – 2025/2026).
‘Lengo la Mpango huo ni
kuboresha na kusogeza huduma za Mahakama karibu na Wananchi ili kuwapunguzia
gharama na muda wanaoutumia kupata huduma za Mahakama,’ Mhe. Ndumbaro amesema.
Amebainisna kuwa katika
mwaka wa fedha 2024/2025 hadi kufikia Aprili, 2025 hali ya ujenzi na ukarabati
wa majengo mbalimbali ya Mahakama inaonesha kuwa ujenzi wa Vituo Jumuishi vya
Utoaji Haki tisa (9) ktika Mikoa ya Katavi, Songea, Songwe, Njombe, Simiyu,
Lindi, Singida, Pemba na Geita unaendelea kwa viwango tofauti.
‘Ujenzi wa majengo ya
Mahakama za Wilaya 11 na Mahakama za Mwanzo 72 unaendelea vizuri katika maeneo
mbalimbali nchini, huku ukarabati wa jengo la zamani la Mahakama Kuu Dodoma
umefikia asilimia 57,’ amesema.
Waziri Ndumbaro ameeleza pia kuwa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama umekamilika na kuzinduliwa tarehe 05 Aprili, 2025; ujenzi wa nyumba za Majaji eneo la Iyumbu Dodoma umekamilika na kuzinduliwa tarehe 05 Aprili, 2025, huku ujenzi wa nyumba ya Jaji Mkuu, jijini Dodoma ukiwa unaendelea.
Uwasilishaji wa hotuba hiyo ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo kutoka Mahakama ya Tanzania, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walishindwa kujizuia na kuibuka kwa shangwe baada ya Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu kumtambulisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel. Kitendo hicho kiliibua shangwe na fifijo bungeni, huku Wabunge wakimpongeza kwa makofi ya kutosha na kumfanya Naibu Spika kutulia kwa muda kabla ya kuendelea na shughuli za Bunge.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiingia bungeni. Picha chini akiwa tayari bungeni tayari kwa kusoma hotuba yake.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Levira akitambulishwa bungeni kama miongoni mwa Viongozi wa Mahakama waliohudhuria uwasilishaji wa hotuba hiyo. picha chini ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania , Prof. Elisante Ole Gabriel akipokea kwa heshima pongezi za Wabunge baada ya kupigiwa makofi ya kutosha yaliyomfanya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu kutulia kwa muda kuendelea na shughuli za Bunge.
Picha na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni