Jumatano, 30 Aprili 2025

MSAJILI MKUU WA MAHAKAMA TANZANIA AFUNGUA MAFUNZO YA MAAFISA TEHAMA ARUSHA

Na SETH KAZIMOTO – Mahakama Arusha

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya amefungua mafunzo kwa Maofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA jana tarehe 29 Aprili, 2025 yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Maofisa TeEHAMA hao kutoka Mikoa yote nchini watapatiwa maarifa na uzoefu zaidi juu ya matumizi ya mifumo mbalimbali inayotumika mahakamani kwa lengo la kuongeza ufanisi wa Mahakama katika utoaji haki kwa Wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Nkya alisema kuwa, pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yanalenga kubadilishana uzoefu na kufanya tathmini ya safari ya mabadiliko ya kitehama yaliyofanyika katika Mahakama ya Tanzania yenye lengo la kuipaisha zaidi Mahakama katika viwango vya kimataifa katika utoaji haki.

Kadhalika, mafunzo hayo yatatumika kukumbushana majukumu ya Maofisa TEHAMA kwa lengo la kuhakikisha kuwa teknolojia inaboresha shughuli za utoaji haki katika ngazi zote za Mahakama.

Msajili Mkuu alisisitiza kuwa, kwa sasa Mahakama inategemea TEHAMA kwa asilimia mia moja katika kutimiza jukumu lake la kikatiba la utoaji haki, ambapo mifumo mbalimbali ya kitehama kama mfumo wa kielektroniki wa kuratibu mashauri (eCMS), mfumo wa kusikiliza mashauri kwa mtandao (Virtual Court) na mingine hutumika. Alisema kuwa Mahakama ilikuwa moja ya watoa huduma wachache ambao waliweza kuendelea kufanya kazi katika kipindi kigumu cha mlipuko wa Uviko 19 kwa sababu ya matumizi ya TEHAMA.

“Ni kutokana na ukubwa na umuhimu wa majukumu mnayofanya, ndio maana nimeona nije mimi mwenyewe ambaye ninashughulikia na kuratibu shughuli za uendeshaji wa mashauri ili kuongea nanyi, kwani ofisi yangu inategemea sana majukumu ya Maofisa TEHAMA katika kuwezesha majukumu ya kila siku ya uendeshaji wa mashauri,” alisema Mhe. Nkya.

Vile vile, Msajili Mkuu aLIeleza kuwa Maofisa TEHAMA ndio mabalozi wa mabadiliko chanya kwa sababu kupitia matumizi sahihi ya TEHAMA wamewezesha ufanisi, uwazi na ubunifu katika utoaji wa huduma za kimahakama.

Amewaeleza Maofisa hao kuwa majukumu yao sio tu ya kiufundi bali pia ni kuwa wasaidizi wa kimkakati  katika kuboresha mchakato mzima wa utoaji haki nchini. Katika hili, Mhe. Nkya alisisitiza kuwa kila Ofisa TEHAMA lazima ajue ipasavyo namna kila mfumo wa kielektroniki unavyofanya kazi na kuweza kuwasaidia watumiaji wa mifumo hiyo ya Mahakama.

Mhe. Nkya alieleza pia kuwa maboresho yanayoendelea ya kitehama, yawe madogo au makubwa katika utoaji huduma za kimahakama, yanaathiri moja kwa moja uzoefu wa mteja kwa huduma za Mahakama, hivyo tafakuri ya kina lazima ifanyike kuhakikisha kuwa ubora wa huduma unabaki ule ule katika ngazi zote za Mahakama.

Mheshimiwa Nkya amesisitiza suala la maadili na usiri kwa Maafisa Tehama huku wakitambua kuwa wao ndio kiungo kikubwa cha wateja wa ndani na nje ya Mahakama katika kuzifikia huduma za Mahakama. Maafisa Tehama wametakiwa kuhakikisha wakati wote wanatoa huduma kwa weledi, na kulinda taarifa za Mahakama kwa unadhifu na uadilifu wa hali ya juu.

Hali kadhalika, Mhe. Nkya alisema kuwa mafanikio ya mifumo na huduma za TEHAMA hayatokani tu na ukubwa wa teknolojia tunayotumia, yanatokana pia na msaada unaotolewa na Maofisa TEHAMA kwa watumiaji wa mifumo hiyo ya Mahakama. Hivyo, Maofisa hao  wamehimizwa kuendelea kuwa nguzo muhimu katika kutimiza ndoto ya kuwa na Mahakama ya kisasa yenye ufanisi na inayoweka Wananchi mbele (Citizen Centric Judiciary), kujenga imani ya Wananchi kwa Mahakama, kuimarisha upatikanaji wa haki na kujenga mustakabali wa Mahakama.

Ufunguzi wa mafunzo hayo ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA anayeshughulikia miundombinu, Bw. Allan Machela na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA anayeshughulikia Mifumo, Bw. Samwel Mshote.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akifungua mafunzo kwa Maofisa TEHAMA yanayofanyika katika Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mkurugenzi wa TEHAMA Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock akiongea na Maofisa TEHAMA wakati wakati wa mafunzo hayo. 

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (katikati walioketi juu na chini) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo. Kushoto kwenda kulia walioketi Ofisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Iringa, Bw. Lusako Mwang’onda, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA -Miundombinu, Bw. Allan Machela, Mkurugenzi wa TEHAMA Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, anayefuatia baada ya Msajili Mkuu ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA-Mifumo, Bw. Samwel Mshote.


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni