Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameshauri mfumo wa kodi nchini kutumia teknolojia
ya kisasa ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika kukusanya mapato.
Mhe. Prof. Juma ametoa
ushauri huo leo tarehe 30 Aprili, 2025 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini hapa alipokutana na Tume ya Rais ya Maboresho
ya Kodi kwa ajili ya kupata maoni yake kuhusiana na suala hilo.
‘Mfumo wa kodi lazima
utumie teknolojia ya kisasa, hatuwezi kuuepuka. Teknolojia ya kisasa ndiyo njia
bora zaidi ya kukwepa tamaduni nyingi zilizopo za watu kukutana katika
kushughulikia masuala ya kodi,’ amesema.
Amewaambia wajumbe wa
Tume hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti, ambaye alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Ombeni Sefue, kuwa kuna mambo mengi ambayo unaweza kufanya kama ukiwekeza kwenye
teknolojia.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa kila
kitu ndani ya Mahakama ya Tanzania kipo kwenye teknolojia na kuna data nyingi,
ikiwemo hukumu mbalimbali ambazo zimepakiwa kwenye mfumo wa TanzLii.
‘Tuliwaomba wataalam wa teknolojia
watumie akili mnemba, wajaribu kuangalia kwenye hukumu hizo changamoto zilizopo
kwenye masuala ya kikodi. Takribani dakika 10 majibu yalipatikana…
‘Akili Mnemba inaweza
kuwa na msaada sana, hizi changamoto zinaweza kuondoka, hasa tukiweza kupunguza
makutano ya mtu kwa mtu kwa sababu binadamu tunakuwa na mitazamo na tamaduni
zetu, ukiziingiza kwenye ukusanyanji wa kodi huwezi kufanikiwa,’ amesema.
Mhe. Prof. Juma
amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye teknolojia haujatumika kikamilifu
kwa kuzingatia kuwa hata Mamlaka ya Mapato Tanzaania-TRA-wana data nyingi na
wanaweza kutumia Akili Mnemba wakapata majibu na suluhisho la changamoto
zilizopo.
Ameiambia Tume hiyo kuwa
kazi yao inahitaji kuwa na fikra pana kwa sababu usuluhishi mwingi kama
kurekebisha sheria umeshafanyika, hivyo njia bora ni matumizi ya teknolojia
ambayo yatapunguza changamoto zilizopo.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa kila
Mtanzania ni mlipa kodi kwa njia moja au nyingine, hivyo mapendekezo yao kama
Tume yatagusa maisha ya mtu bonafsi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mhe. Prof. Juma ameeleza
kuwa kama Kiongozi wa Mhimili, alipata pia nafasi ya kuzungumza na Majaji wa
Mahakama ya Rufani, hasa wale waliowahi kuwa Wenyeviti katika Mabaraza ya Kodi ili
kupata maoni yao jinsi ya kuboresha mfumo wa kodi nchini na changamoto wanazoziona.
Katika maoni yao, Majaji
hao wamebainisha, pamoja na mambo mengine, kuangalia upya njia zinazotumika
kuingiza bidhaa na Maofisa Forodha kuwepo kwenye maeneo ya madini,
wafanyabiashara wadogo kulipa kodi rafiki na kuweka mud awa TRA kujibu mapingamizi.
Jaji Mkuu pia alikutana
na Jaji aliyewahi kuwa Wakili kwenye mashauri ya kodi kupata maoni yake kuhusu
suala hilo na kubainisha changamoto kadhaa, ikiwemo utatuzi wa mgogoero wa kodi
kuchukua muda mrefu unapoteza imani ya walipa kodi.
Alieleza kuwa kwa kuwa Bodi
ya Rufaa ya Kodi pamoja na Baraza la Rufaa la Kodi kuwa chini na Wizara ya
Fedha na wajumbe wake kuteuliwa na Waziri wa Fedha huathiri muonekano wa Taasisi
hizo kuwa huru mbele ya macho ya mlipa kodi.
Kadhalika, Mhe. Prof.
Juma alipata maoni kutoka kwa wafanyabiashara wenye shule binafsi na kubainisha
kuwa Watumishi wa umma ni wakali kupindukia wanaposhughulikia masuala ya kodi
na watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kutokuwa waadilifu.
Wakizungumza baada ya
maoni hayo, Wajumbe wa Tume wamempongeza Jaji Mkuu kwa maoni hayo chanya
aliyotoa na kuunga mkono mapendekezo aliyoyatoa, hususan matumizi ya teknolojia
katika kutatua changamoto za kikodi na kwamba wanatakiwa kufikiri kwa upana
kabla ya kutoa mapendekezo yao kwenye suala hilo.
Kabla ya mazungumzo hayo,
wajumbe wa Tume hiyo walitembelea Ofisi ya Jaji Mkuu kujionea mambo mbalimbali,
ikiwemo picha za Majaji Wakuu waliowahi kuhuduma mahakamani kabla na baada ya
uhuru.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni