- Yabeba ndoo 4, medali mbili
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama,
Dodoma
Timu ya Mahakama ya
Tanzania, maarufu Mahakama Sports, imeshiriki kwa mafanikio makubwa kwenye
mashindano ya Mei Mosi kwa mwaka 2025 yaliyofanyika mkoani Singida na
kufanikiwa kupata makombe manne na medali kadhaa katika michezo mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa jana tarehe 1 Mei, 2025 na Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Wilson
Dede, Timu hiyo ilishiriki katika michezo ya mpira wa miguu, netboli, riadha,
karata, draft, bao, dats na baiskeli.
Anaeleza kuwa Timu ya
Mahakama iliingia kambini Singida kuanzia tarehe 14 Aprili, 2025, ikiwa na washiriki
47, wakiwemo Viongozi na kupangwa kwenye makundi mbalimbali.
Timu ya Mahakama Sports
imefanya vizuri katika upande wa karata Wanawake na kuibuka mshindi wa kwanza
na kuzawadiwa kikombe. Kadhalika, kwenye upande wa baiskeli na bao Wanawake, Mahakama
Sports ilifanya vizuri pia na kufanikiwa kuwa mshindi wa pili, hivyo kuzoa vikombe
viwili.
Mwenyekiti Dede anaeleza
pia kuwa Mahakama Sports ilifanikiwa kutimua vumbi kwenye mchezo wa riadha kwa
upande wa Wanaume na Wanawake mita 200 na kufanikiwa kupata medali mbili baada
ya kushika nafasi ya tatu kwa kila upande.
Pamoja na makombe hayo
matatu, Mahakama Sports ilishiriki katika Bonanza kubwa la OSHA lililofanyika
mkoani Singida tarehe 26 Aprili, 2025 ikiwa na michezo mbalimbali. Bonanza hilo
lilijumuisha Timu 12 kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali na Mashirika
yaliyokuwa kwenye mashindano ya Mei Mosi 2025.
Katika Bonanza hilo, Timu
ya Mpira wa Miguu ya Mahakama Sports ilishiriki na kufanikiwa kuwasambaratisha
wapinzani wote na kuwa mabingwa wa bonanza hilo, hivyo kuzawadiwa kikombe cha
mshindi wa kwanza.
Katika mashindano ya Mei
Mosi, Mwenyekiti Dede anaeleza kuwa Timu ya Mahakama ilishiriki pia kwenye michezo
ya Mpira wa Miguu na Mikono.
‘Katika mchezo wa mpira
wa miguu, Mahakama tulikuwa kundi "B" lenye timu sita, ambazo ni
Mahakama, TRA, U-DOM, Utumishi, Afya na Maji. Upande wa mchezo wa mera wa mikono tulikuwa kundi "A" lenye timu za Mahakama, Afya, Maliasili, Tume ya Ushirika,
MSD na Fedha,’ amesema.
Mwenyekiti Dede anaeleza
kuwa katika mchezo wa mpira wa miguu, Mahakama ilicheza mechi tano na kuishia kwenye
makundi, hivyo kushindwa kusonga mbele.
Anaeleza pia kuwa kwa
upande wa netbali, Mahakama ilifanikiwa kuingia hatua ya nane bora ambapo ilicheza
na Wizara ya Mambo ya Ndani na kupoteza mchezo, hivyo kushidwa kuendelea na
mashindano katika hatua iliyofuata.
Mfukuza upeo wa Mahakama Sporst Atugonza Yusta Tibendelanda akiwa na moja ya makombe hayo. Picha chini ni mfukuza upepo mwingine Mwajabu Gwire akiwa na kombe alilonyakua baada ya kuwa mshindi wa pili kwenye mchezo wa baiskeli.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni