Wafurahishwa na kinara wa mageuzi
Mtendaji Mkuu asema kila Aprili ya mwaka Majaji Wastaafu kutembelea Makao Makuu
Na MAGRETH KINABO -Mahakama, Dodoma
Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,wamefurahishwa na mageuzi ya miundombinu ya majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, yakiwemo Makazi ya Majaji,na mahakama nyingine mbalimbali nchini,huku wakimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma kwa usimamizi wake imara katika Mhimili huo.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 30 Aprili,2025 na Rais wa Chama cha Majaji Wastaafu Tanzania, Mhe. Jaji Thomas Mihayo,ambaye pia ni Jaji Mstaafu wa Mahakama hiyo, kwa niaba ya wa Majaji Wastaafu wenzake walipotembelea majengo hayo.
“Tumefurahishwa na mageuzi yaliyofanyika katika miundo mbinu ya maeneo mbalimbali ya majengo ya Mahakama ya Tanzania, tumeona jinsi majengo haya yalivyojengwa na kusimikwa mifumo tofauti ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ya kisasa ambayo inarahisisha utoaji haki kwa wakati kwa wananchi,” alisema Mhe. Jaji Mihayo.
Mhe. Jaji Mihayo alipendekeza kwa Jaji Mkuu kuwa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania litumike kukuza utalii nchini.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu Mhe. Prof.Juma aliwaelezea kuhusu mageuzi hayo yaliyofanyika kwa kuangalia historia ya enzi za ukoloni hadi sasa.
Katika hatua nyingine Majaji hao walionekana kufurahia mandhari ya majengo hayo, ikiwemo mifumo ya TEHAMA kwa kuonesha tabasamu kila walipokuwa wakitembelea majengo hayo.
Majaji hao pia walitembelea ofisi ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, ambapo walipata maelezo ya picha za Majaji Kiongozi wa zamani na shughuli za Mahakama hiyo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alitoa maeleze jinsi Mahakama ilivyofanikiwa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki(IJCs) sita na kufanikiwa kuokoa kiasi cha fedha sh. bilioni 3.6.
Pia aliongeza kuwa ziara hiyo ya Majaji hao ni ya kwanza kufanyika, hivyo Mahakama itaendelea na utaratibu wa ziara ya namna hiyo kila Aprili kwa mwaka.
Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania,Mhe.Desdery Kamugisha, alipata wasaa wa kuelezea Chumba Maalum cha Kutolea Taarifa za Mahakama nchi nzima (Judicial Situation Room) kilichopo kwenye Jengo la Makao Makau ya Mahakama ya Tanzania, kinavyofanya kazi ya kutoa taarifa mbalimbali za mashauri ya Mahakama ya Tanzania nchini kwa Majaji hao.
Wakati huohuo,Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kifungu Mrisho Kariho, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, aliwaonesha Mfumo wa Maktaba Mtandao( TANZLII) unavyoweza kusaidia kupata taarifa za maamuzi na kufanya utafiti wa kisheria.
Afisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania na Kiongozi wa Timu ya Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Bi. Evetha Mboya alieleza jinsi kilivyoanzishwa na kinavyofanya kazi, ambapo alisema kina uwezo wa kupokea simu zaidi 30 tofauti kwa wakati mmoja.Pia kina mfumo unaowezesha kupata taarifa mbalimbali za siku, wiki na mwezi, kurekodi mazungumzo na hauna gharama kwa wananchi.
Alifafanua kwamba maeneo ambayo, sauti za wananchi zinasikika ni mirathi na utekelezaji wa maamuzi.
Mboya aliongeza kuwa maeneo,ambayo malalamiko yamepungua ni, upatikanaji wa nakala za hukumu,utoaji wa hati za kimahakama, dhamana, maadili ya Maafisa wa Mahakama na vikao vya Mahakama ya Rufani Tanzania.
Kituo hicho, kimefanikiwa kutembelewa na wageni mbalimbali wa kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kujifunza kutoka Mahakama ya Msumbiji, Uganda, Zanzibar,Maktaba Kuu ya Taifa ya Tanzania, Wizara ya Katiba na Sheria na Jeshi la Polisi.
Majaji hao pia walishiriki kupanda miti ikiwa ni ishara ya kumbukumbu na kuhifadhi mazingira.
Picha ya pamoja ya Majaji hao, wakiwa katika Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof .Ibrahim Hamis Juma, akifurahia jambo.
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama(Maadili na Nidhamu), Bi. Alesia Mbuya(katikati) akisalimiana na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Julius Mallaba(kulia).
Majaji hao, wakiwa katika chumba cha mikutano cha Jengo la Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Picha ya juu na chini Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo(kushoto), akiwaongoza Majaji hao, kutembelea Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni