Ijumaa, 2 Mei 2025

WABUNGE WAIPONGEZA MAHAKAMA KWA MABORESHO, UTOAJI HAKI NCHINI

Na ARAPHA RUSHEKE na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Wabunge mbalimbali waliopata nafasi ya kuchangia Hotuba ya Mipango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa jinsi inavyofanya kazi katika kuhakikisha inatoa huduma bora za haki kwa Wananchi.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Kalambo, Mhe. Josephat Sinkamba ameipongeza Mahakama ya Tanzana kwa maboresho ya miundombinu ya majengo ambayo yamendelea kujenga nchini.

Naye Mbunge wa Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo ameeleza kuwa majengo mazuri ya Mahakama yanayojengwa katika maeneo mbalimbali ni ishara nzuri inayoakisi maendeleo katika sekta ya utoaji haki kwa Wananchi.

Ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizotumika kukamilisha miradi mbalimbali ya Mahakama, ikiwemo Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

‘Jengo hili ni la kwanza kwa ukubwa wa Makao Makuu ya Mahakama katika Bara la Afrika na la sita duniani. Ukamishaji wa miradi hii ni dhamira ya dhati ya Serikali yetu katika kuimarisha utoaji wa haki na utawala wa sheria nchini,’ amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Segini ameeleza kuwa wanaendelea kushughulikia uchakavu wa miundombinu ya Mahakama kutokana na uwepo wa Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya zilizokuwa zimejengwa tangu enzi ya Mkoloni.

Ameeleza kuwa Wizara imepokea ushauri wa Wabunge walioshauri Wizara na sekta ya Mahakama kuwekeza nguvu katika ujenzi wa Mahakama kwenye Tarafa kwa dhumuni la kuhakikisha zinakuwa na Mahakama kabla ya kuhamia ngazi ya kata.

Akihitimisha mjadala wa Wabunge hao, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Damas Ndumbaro amesema bajeti hiyo inaenda kufuta machozi ya Watanzania waliodhulumiwa haki kwa muda mrefu.

“Bajeti hii sisi tunaita bajeti ya haki, bajeti ambayo inaenda kumpa haki Mtanzania, kutoa shibe kwa Watanzania wenye njaa na kiu ya haki. Italeta mwanga na kuondoa giza la dhuluma ya haki kwa Watanzania wanyonge katika kona zote za Jamhuri ya Muungani wa Tanzania,” amesema.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha jumla ya fedha za Kitanzania 687,698,489,000/= kama bajeti kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Kati ya fedha hizo, 135,995,670,000/= ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi, 389,464,032,000/= ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na 162,238,787,000/= ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Wizara hiyo pamoja na Taasisi zilizopo chini yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro akijibu hoja za Wabunge wakati wa kuhitimisha hotuba ya makadirio ya Wizara ya Katiba na Sheria bungeni.

Sehemu ya Wabunge wakimpongeza Waziri wa Katiba pamoja na Naibu wake mara baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha makadirio ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.

Juu na chini Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akipongezana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Naibu wa Waziri, Mhe. Jumanne Segini mara baada ya Mkutano wa Bunge kuahirishwa.    Kushoto ni Katibu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Eliakim Maswi.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel-katiakti mstari wa mbele- akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama mara baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria katika viwanja vya Bunge. Wengine waliopo mstari wa mbele ni Msajili Mikuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya-kushoto na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu-Bi. Beatrice Patrick.

(Picha na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni