- Ahitimisha kwa kukagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi Njombe
- Amtaka Mkandarasi kuandaa mpango wa kumaliza mradi huo kwa wakati
Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru amehitimisha ziara ya ukaguzi
wa Mahakama za Mkoa na Wilaya ya Njombe na baadhi ya Mahakama za mwanzo zilizo
ndani ya Kanda ya Iringa huku akiwasisitiza watumishi wa Mahakama hizo kufanya
kazi kwa kuzingatia maadili na kuiishi salamu ya Mahakama ya Tanzania
inayojengwa na maneno ya Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji.
Akizungumza na watumishi wa Mahakama
hizo kwa nyakati tofauti alipotembelea Mahakama za Wilaya na alipohitimisha ziara
ya ukaguzi wa robo ya nne ya mwaka wa
fedha 2024/2025 iliyofanyika mkoani Njombe, Mhe. Ndunguru aliwapongeza pia
watumishi kwa utendaji kazi mzuri.
“Hii ni ziara ya ukaguzi wa kawaida
ambao nimekuja kufanya kwa mujibu wa miongozo ya ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania
na kuona utendaji kazi wenu maana kama kukagua ningetumia hata mifumo ya TEHAMA
kujua idadi ya mashauri na nikajua Hakimu yupi ana mashauri mengi yenye
mlundikano ila nawasisitiza watumishi wote muishi kwenye dira ya Mahakama ya
Tanzania haswa kujiepusha na vitendo vya utovu wa maadili hasa vitendo vya
kupokea rushwa,” alisema Mhe.Ndunguru.
Jaji Ndunguru aliwasisitiza watumishi
hao kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana kwa upendo na umoja huku akiwasisitiza
wawe na utaratibu wa kujisomea na kujiendeleza kielimu ili waweze kutimiza
malengo yao huku akiwasisitiza watumishi kutunza afya zao hasa kuweka utaratibu
wa kufanya mazoezi maana afya ni mtaji. Vilevile aliwataka watumishi wawe angalau
mara moja au mbili kwa mwaka waweze kuwa na utaratibu wa kwenda kutembelea vivutio
vya utalii wa ndani ili kujifunza mambo mengi ya nchi yetu.
Kwa
upande wa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe.Bernazitha
Maziku kwa nyakati tofauti akiwa Wilaya ya Wanging’ombe
na Njombe alikiri kuwa utendaji kazi wa watumishi wa Mahakama hizo ni mzuri na unaridhisha
kwa kiwango kikubwa na taarifa zao za hali ya mashauri katika Wilaya hizo zinavutia
kutokana na kasi ya uondoshaji wa mashauri mahakamani.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa akizungumza na watumishi hao
aliwashukuru watumishi wote katika Mkoa wa Njombe kwa kuendelea kuimarisha
taswira Chanya ya Mahakama kwa jamii.
“Ni muhimu kila mtumishi kuwa muadilifu
kwa kuwa mmeaminiwa na kupewa nafasi mnazotumikia hivyo, kuweni na weledi na
uwajibikaji kwa kuwa kila mmoja ni mbobezi katika kada yake,” alisema Bi. Mkongwa.
Baada ya kikao hicho cha kuwaaga
watumishi baada ya kuhitimisha ziara hiyo ya ukaguzi Mhe. Ndunguru aliogozana
na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa, Naibu Msajili
wa Mahakama kuu Kanda ya Iringa, Mhe.Bernazitha Maziku, Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama pamoja na Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Njombe, Mhe. Matilda Kayombo walitembelea Mradi wa Ujenzi
wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe kinachoendelea kujengwa.
Baada ya kufika kwenye kituo cha utoaji haki Njombe kinachojengwa chini ya kampuni ya Shadong Mhe. Ndunguru alipokea taarifa fupi ya utekelezaji wa ujenzi ambapo ilibainishwa kuwa umefikia asilimia 81.5 kwa sasa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (wa pili kushoto) akizungumza jambo na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya ya Njombe (hawapo katika picha). Wa kwanza kushoto ni Naibu Msajiri wa Mahakama kuu Kanda ya Iringa , Mhe. Bernazitha Maziku, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama kuu kanda ya Iringa,Bi,Melea Mkongwa na wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru pamoja na viongozi wengine wa Kanda hiyo wakifuatilia taarifa fupi ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe.
Ukaguzi ukiendelea.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya viongozi wa Mahakama Iringa na Njombe pamoja na mafundi katika eneo la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama- Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni