Na FAUSTINE KAPAMA na ARAFA RUSHEKE-Mahakama, Dodoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju leo tarehe 4 Julai, 2025 amekutana
na Viongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali na kuhimiza Wanachama kuzingatia
mambo sita wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo kuisaidia Mahakama katika
kufikia uamuzi wa haki.
Mambo
hayo yaliyosisitizwa na Mhe. Masaju alipokutana na Viongozi hao ofisini kwake kwenye Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma ni umahiri (competence), uadilifu (integrity), umakini (proactive), ubunifu (creativity), uzalendo wa kitaifa (national patriotism) na kujali haki (sensitive to justice).
Viongozi
hao ni Bavoo Junus (Rais), Debora Mcharo (Makamu wa Rais), Addo November
(Mwenyekiti), Selestina Kunambi (Makamu Mwenyekiti) na Rashid Mohamed Said
(Katibu).
Akizungumzia
na Viongozi hao, Mhe. Masaju amesema kuwa ili Wanachama wa Chama cha Mawakili
wa Serikali waweze kutekeleza majukumu yao kwa mafanikio makubwa wanatakiwa
kuzingatia na kuyaishi mambo hayo sita.
Kuhusu
suala ya umahiri, Jaji Mkuu ameeleza kuwa hilo limekuwa changamoto kubwa katika utumishi wa umma na kwamba watu wengine wanaamini ili kuwa mahiri
lazima uwe na shahada nyingi.
‘Hapa
ndipo tunapopotea, watu tutalazimika kusoma shahada hizi, lakini shahada
yenyewe haikuletei umahiri. Tumejichanganya sana kwenye eneo hili, wakati fulani
tunaenda kusoma kwa sababu ya vyeo. Tusome ili tuwe na hizi shahada, lakini
zituwezeshe basi kuwa mahiri kwenye hilo eneo,’ amesema.
Mhe.
Masaju amewaeleza Viongozi hao kuwa umahiri wa hali ya juu unahitajika kwa Wanasheria
waliopo kwenye sekta ya umma katika kushiriki kwenye majukumu ya kusimamia
utawala wa sheria, mikataba, kuendesha mashauri na kuishauri Serikali katika
masuala mbalimbali.
Jaji
Mkuu ameeleza pia kuwa suala la uadilifu ni jambo la msingi katika
utumishi wa umma, hivyo amewasihi Wanachama wa Chama hicho kwenda kuwatumikia
wananchi kwa kufuata misingi hiyo.
Akizungumzia
suala la umakini, Mhe. Masaju amesema kuwa jambo hilo nalo limekuwa changamoto
kwenye sekta ya sheria, hivyo Wanasheria wanatakiwa kujiongeza kwani mtu
anaweza kujua majukumu yake na changamoto zilizopo, lakini hawezi kuchukua
hatua mpaka asubiri mtu mwingine.
‘Kuna
mambo mengi yanayotukabili, tusipokuwa makini tutakwama. Siku hizi kila kitu
mpaka tusukumwe, tunapaswa kuwa wabunifu kwani changamoto ni nyingi. Lazima tuwe
wabunifu kushughulikia hizi changamoto ili utumishi wetu ufanikiwe,’ Jaji Mkuu
amesema.
Jambo
jingine ambalo Wanachama wa Chama cha Mawakili wa Serikali wanatakiwa
kuzingatia ni uzalendo kwa Taifa kwani wanabeba maslahi ya nchi. Mhe. Masaju
amesema kuwa haitoshi kuwa mwadilifu, lazima pia Mwanachma aweke mbele maslahi
ya umma.
Jaji
Mkuu pia aliwaeleza Viongozi hao kuwa Wanachama wa Chama cha Mawakili wa
Serikali wanatakiwa kujua wanajiandaa namna gani wanapoenda mahakamani, wanatoa
ushauri gani wa kisheria kwenye maeneo mbalimbali, wanaguswa namna gani kwa watu
wanaoonewa, wanafanya nini na nafasi yao ni ipi.
Akizungumza
wakati wa ugeni huu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Mustapher Mohamed Siyani amewahimiza Wanachama wa Chama hicho kuendeleza
utamaduni na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Mawakili wa Serikali na
Mahakimu.
Naye
Rais wa Chama hicho, kwa niaba ya Viongozi wenzake, alimshukuru Jaji Mkuu kwa
kuwapa fursa ya kukutana naye kwa madhumuni ya kujitambulisha na kumpongeza kwa
kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo.
Kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kukitambulisha Chama kwa Jaji Mkuu kwani bado nikichanga na mdau mkubwa kwa Mahakama. Aliomba ushirikiano wa Mahakama ya Tanzania kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo mafunzo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni