Ijumaa, 4 Julai 2025

MAFUNZO YALETA TIJA YA UANDISHI MZURI WA HUKUMU ZA MAHAKIMU KIGOMA; JAJI NKWABI

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi amekiri kufurahishwa na mabadiliko makubwa ya uandishi wa hukumu za Mahakimu wa Kanda hiyo hatua iliyofikiwa kutokana na mafunzo kadhaa yaliyotolewa kwa Mahakimu hao.

Mhe. Nkwabi aliyasema hayo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Kigoma kwa nyakati tofauti akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya za Kanda hiyo uliofanyika kati ya tarehe 30, Juni mpaka 04, Julai 2025.

“Nimeona tija kubwa ya uwepo wa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo Mahakimu na watumishi wengine, na tusiishie hapo tu, bali tuwafikie na wadau wetu, hii itaboresha mpango mkakati wetu wa kumaliza mashauri na kutoa haki kwa wakati,” alisema Mhe. Nkwabi.

Katika hatua nyingine, Jaji Nkwabi aliwapongeza watumishi na watendaji wa Mahakama za Wilaya sita (6) za Kanda hiyo kwa ushirikiano wanaouonesha katika vituo vyao wa kumaliza mashauri zaidi ya 300 katika robo ya nne ya mwaka  wa fedha 2024/2025, ambapo imefanya Kanda kuvuka mwaka bila kuwa  na mashauri ya mlundikano.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa alibainisha kuwa, Mahakama Kanda ya Kigoma itaendelea kudumisha utamaduni wake wa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na weledi katika kutatua changamoto kwa haraka  kwa watumishi na wananchi wanaohudumiwa na Mahakama zote zilizopo ndani ya Kanda hiyo.

Naye,  Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay, alimhakikishia Jaji Nkwabi, kuwa Kanda ya Kigoma itaendelea kuboresha miundombinu ya majengo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kuendelea kuratibu mafunzo ya ndani kwa watumishi ili kuongeza weledi na kuwajengea uwezo zaidi katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

Bw. Matotay aliongeza kuwa, pamoja na hayo Kanda itaendelea kuwapatia wadau uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya uratibu na usimamizi wa mashauri mahakamani (e-CMS).

Mahakama za Wilaya zilizokaguliwa ni Kigoma, Kasulu, Kibondo, Uvinza, Buhigwe, Kakonko, pamoja na Magereza ya Wilaya Kigoma na Kasulu. Katika ziara hiyo, Mhe. Nkwabi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili mbelwa pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay.

Ziara hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo na kutoa pongezi kwa watumishi wa Mahakama hizo kwa utunzaji bora wa mazingira ya Mahakama hizo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi akizungumza jambo na watumishi (hawapo katika picha) wakati wa ziara yake ya ukaguzi katika Wilaya ya Kasulu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Wilaya Uvinza alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama. Upandaji wa mti umefanyika ili kuhamasisha upandaji miti katika maeneo ya Mahakama zote za Kanda hiyo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay akifafanua jambo kwa msisitizo wakati wa kikao cha ukaguzi wa shughuli za Mahakama ya Wilaya Buhigwe.

Picha ya pamoja ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kakonko. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni