Na HUBERT MAANGA-Mahakama, Mtwara
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki hivi karibuni alifanya
ziara kukagua utendaji kazi katika Mahakama za Mkoa wa Mtwara.
Katika ziara hiyo, Jaji
Mfawidhi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe.
Seraphine Nsana, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Bw. Yusuph Msawanga
pamoja na Viongozi wengine.
Miongoni mwa Mahakama
zilizokaguliwa ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mahakama za Wilaya
Tandahimba, Newala, Nanyumbu na Masasi na Mahakama za Mwanzo Mahuta, Kitangali,
Chikundi na Nanyumbu.
Katika ziara yake, Mhe. Kakolaki
alikutana na watumishi na kupokea taarifa za utendaji kazi, kusikiliza
changamoto zinazowakabili na kutoa maelekezo mbalimbali. Aidha, katika kila Mahakama
ya Wilaya, aliongea na Mahakimu na kusisitizia utendaji wenye uadilifu.
Katika vikao na
watumishi, Jaji Mfawidhi aliwapongeza kwa utendaji kazi mzuri hasa kumaliza mashauri
kwa wakati, kutokuwa na mlundikano wa mashauri, kuzingatia unadhifu na ubunifu
wa kuhifadhi nakala laini za hukumu na mwenendo wa mashauri kwa Mahakama za Mwanzo.
"Kwa mwenendo huu,
huduma ya Mahakama itazidi kuonekana bora na kuzidi kuvutia wateja, kwa maana mteja
atakapo pata haki yake na kuridhika na huduma yetu, atawashawishi hata wengine
kuiamini Mahakama katika utoaji haki," alisema Jaji Mfawidhi.
Aidha, aliwapongeza
Mahakimu kwa mafunzo yanayotolewa redioni na sehemu nyingine juu ya matumizi ya
mifumo na manufaa yake, huku akiwasihi kuendelea kuwapa elimu wananchi.
Vilevile, aliwataka
kuendelea kuwaelewesha wananchi kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano-TEHAMA-katika usikilizaji mashauri na jinsi gani inavyosaidia
kuondoa gharama, kupunguza muda kuwezesha wateja kuendelea na shughuli
nyingine.
Katika kutekeleza maagizo
ya Jaji Mkuu, aliwataka Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuendelea kuchapa kesi
zote kwenye mfumo ili kurahisisha upatikanaji wa nakala laini za mienendo ya
mashauri.
Akizungumzia hali ya majengo
ya Mahakama na vyombo vya usafiri, Mhe. Kakolaki aliagiza majengo yatunzwe kwa
kutumia fedha za ndani zinazopatikana, magari na pikipiki yafanyiwe matengenezo
mara kwa mara ili yaendelee kutumika kwa muda mrefu.
Aidha, Jaji Mfawidhi
alihimiza Mahakama za Wilaya kuhakikisha maeneo yote ya Mahakama ambayo hayana
hati miliki yanapatiwa ili kurahisha kuombea miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama.
Wakati wa ziara yake, Jaji
Mfawidhi alikagua miradi miwili ya ujenzi ya Mahakama za Mwanzo Kitangari na
Chikundi yanayoendelea katika Mkoa wa Mtwara na kuridhika na kasi na usimamizi
wa ujenzi wa miradi hiyo.
Kadhalika, Mhe. Kakolaki alitembelea Magereza ya Lilungu, Newala na Masasi ambapo alipokea taarifa na kusikiliza changamoto za Wafungwa na Mahabusu na kuwashauri kujifunza na kukuza vipaji vya elimu ya ujasiriamali kwa manufaa yao watakaporudi uraiani.
Watumishi
wa Mahakama ya Wilaya Masasi wakimpokea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (wapili kushoto) akiteta machache na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nanyumbu.
Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Tandahimba, Mhe. Joseph Waruku (kulia) akiwasilisha taarifa ya Mahakama ya Wilaya Tandahimba mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati).
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki
akipanda mti katika viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Mahuta wilayani Tandahimba.
Ukaguzi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kitangari iliyopo Wilaya ya Newala kwa hatua iliyofikia hadi sasa.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (kulia)
akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya na Mkoa Mtwara.
Jopo
la Wadau katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati), wakilitembelea
Gereza la Lilungu.
Watumishi
wa Mahakama ya Wilaya Masasi katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (wa pili kulia).
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni