Ijumaa, 25 Julai 2025

JAJI MKUU ASHIRIKI MAADHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA SIKU YA MASHUJAA TANZANIA

  • Shujaa Brigedia Jenerali Mstaafu Balozi Francis Mndolwa asisitiza Uzalendo wa Nchi

 Na MARY GWERA, Mahakama - Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju leo tarehe 25 Julai, 2025 ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (JWTZ) Jenerali Jacob John Mkunda, Viongozi wa Serikali na Watanzania kwa ujumla kuadhimisha Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa nchini.

Hafla ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa imefanyika katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo katika Mji wa Serikali-Mtumba jijini Dodoma huku ikitawaliwa na ratiba mbalimbali ikiwemo utoaji wa dua na sala.

Mara baada ya Rais Samia kuwasili katika Viwanja hivyo, ratiba ya Siku hiyo muhimu ilianza kutekelezeka mara moja ambapo ilianza kwa kutolewa kwa salamu ya Rais, iliyofuatiwa na Wimbo wa Taifa, Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Gwaride la Maombolezo kupindua Silaha chini na baadaye ilipigwa Mizinga miwili ya maombolezo iliyofuatiwa na ukimya kwa dakika moja ikiwa ni hatua ya kuwakumbuka mashujaa waliotangulia mbele za haki.

Baada ya ratiba za awali kufanyika kulikuwa na zoezi la uwekaji Silaha za Asili na Shada Maua kwenye Mnara wa Mashujaa ambapo Mhe. Dkt. Samia aliongoza zoezi hilo kwa kuanza kuweka Mkuki na Ngao, akifuatiwa na Mkuu wa Majenzi ya Ulinzi ambaye aliweka Sime.

Aidha, Kiongozi wa Mabalozi naye aliweka Shada la Maua, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma aliweka Upinde na Mshale na Shujaa wa Taifa aliweka Shoka.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Waandishi wa Habari mara baada ya sherehe hizo, Mmoja wa Mashujaa aliyeshiriki katika Vita ya Kagera, Brigedia Jenerali Mstaafu Balozi Francis Mndolwa ametoa rai kwa Wanahabari na Watanzania kwa ujumla kuwa na uzalendo wa nchi ili kuendelea kutunza amani ambayo imepiganiwa na Waasisi wa Nchi hii akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Nchi hii imetoka mbali, nchi hii inahitaji msaada wa kila mmoja wenu ili tuendelee kuwa na amani katika hii nchi, nchi nyingi zinazotuzunguka zimebomoka, lakini tuwashukuru Waasisi wetu Mwalimu Nyerere, Mzee Karume walifanya kazi kubwa sana kuwaandaa wananchi ambao sasa wanaendeleza,” amesema Brigedia Jenerali Mstaafu Balozi Mndolwa.

Ameongeza kuwa, juhudi za waasisi hao hazina budi kuendelezwa ili nchi yetu iendelee kuwa na amani.

Mbali na Jaji Mkuu, Viongozi wengine waliohudhuria katika sherehe za Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Mashaka Biteko, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Mhe. William Lukuvi na viongozi wengine.

Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania huadhimishwa tarehe 25 Julai kila mwaka lengo likiwa ni kuwakumbuka na kuwaenzi Mashujaa waliofariki wakati wakiutetea, kuupigania na kuulinda Uhuru wa Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa katika sherehe za Kumbukumbu ya Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Tanzania leo tarehe 25 Julai, 2025 katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Wa nne kulia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, wa tatu kushoto ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wa tatu kulia ni Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju, wa pili kushoto ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Mashaka Biteko na wa kwanza kulia ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Mhe. William Lukuvi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa kwanza kushoto) akifuatiwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Mhe. William Lukuvi kwa pamoja wakifuatilia kilichokuwa kikijiri wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania zilizofanyika katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo Mji wa Serikali-Mtumba jijini Dodoma. 

Meza Kuu ikiongozwa na Rais Samia wakifuatilia yanayojiri katika Sherehe za Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) na  baadhi ya Viongozi wengine wakiwa katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Kushoto kwa Rais Samia ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (JWTZ) Jenerali Jacob John Mkunda.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiweka Mkuu kwenye Mnara wa Mashujaa.

Mnara wa Mashujaa.

Mmoja wa Mashujaa aliyeshiriki katika Vita ya Kagera, Brigedia Jenerali Mstaafu Balozi Francis Mndolwa akielekea kwenye eneo la Mnara wa Mashujaa kuweka Shoka kama ishara ya kuwaenzi Mashujaa wa Kitanzania waliotangulia mbele za haki.



Sehemu ya wananchi walioshiriki kwenye sherehe za Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (kulia) akizungumza jambo na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akisalimiana na baadhi ya Viongozi waliohudhuria katika sherehe za Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Tanzania leo tarehe 25 Julai, 2025.


Burudani ikiendelea kutoka Kikundi cha Makutupora wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Tanzania zilizofanyika leo tarehe 25 Julai, 2025 katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma.

Vikosi vya Ulinzi na Usalama vikifanya Gwaride maalum lililoandaliwa wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa nchini leo tarehe 25 Julai, 2025.










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni