Na LORDGARD KILALA, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi
Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi imepiga hatua katika Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kufuatia uzinduzi rasmi na matumizi ya ‘QR Code’ ili kurahisisha upatikanaji wa haki kazi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Matumizi ya QR Code jana tarehe 25 Julai, 2025 katika Ofisi za Mahaakama hiyo zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina alisema kuwa Mahakama ya Tanzania kupitia Divisheni hiyo imefanya mageuzi ya kidijitali kwa kuja na tecknolojia ya QR code (Quick Response) ambayo huhifadhi data iliyofichwa na ili mtu aweze kuipata ni kwa kuchungua (scanning) kupitia simu janja.
“Tunazindua QR Code kwa ajili ya Ratiba za Mashauri (Cause Lists) ya wiki katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, QR Code kwa ajili ya Juzuu za Maamuzi ya Kesi za Kazi za Mahakama ya Rufani na QR Code kwa ajili ya Kanuni za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Mahakama ya kazi, na Sheria za Kazi. Hatua hii inalenga kuboresha upatikanaji wa haki kazi kwa kutumia teknolojia kurahisisha taratibu za Mahakama ya Kazi,” alisema Mhe. Dkt. Mlyambina.
Mhe. Dkt Mlyambina alieleza kuwa, wamefikia hatua ya kuja QR Code ili kurahisisha na kuharakisha kupatikana kwa huduma za nyaraka zinazohusiana na Mahakama hiyo ambapo alisema kwa kuanzia QR Code zitatoa huduma ya upatikanaji ratiba ya mashauri ya wiki ‘Cause list’ ya Wiki ya Mashauri katika Mahakama ya Kazi, Sheria za Kazi, Juzuu za Maamuzi ya kesi za Kazi za Mahakama ya Rufani na Upatikanaji Kanuni za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo alitaja faida za uanzishwaji wa QR Code, ambapo alisema inasaidia kupunguza muda wa kutafuta taarifa kwani kupitia kwa simu janja taarifa zilizohitaji hupatikana papo kwa hapo, kuharakisha kupatikana kwa haki kwa wakati sawa na nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama, inasaidia pia kuhifadhi mazingira kwa kuondoa matumizi ya karatasi.
Mhe. Dkt. Mlyambia aliongeza kuwa, QR Code inasaidia kupunguza gharama na kuokoa muda wa uchapishaji na kudurufu nyaraka kwa nyaraka kusudiwa kupatikana katika nakala laini, huongeza pia uwajibikaji na uwazi zaidi kwa kuwa huwezesha upatikanaji rahisi wa taarifa za Mahakama unakuza uwazi, jambo linaloimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki.
Alisema kwamba, hatua hiyo inaendana na Nguzo ya kwanza ya Mpango Mkakati inalenga juu ya Usimamizi wa Rasilimali.
Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa, QR Code husaidia pia kuhusu Usalama na ufuatiliaji ambapo unaweza kujua ni watu wangapi na nani aliyepakua taarifa iliyotolewa.
“Ni rahisi kutumia OR Code kwani inahitaji kamera ya simu janja tuu sio mpaka kupitia _URLs_ teknolojia hii inajenga na kurudisha imani ya wananchi kwa Mahakama sawa na nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama,” alisisitiza Mhe. Dkt. Mlyambina.
Aidha, Mhe. Dkt. Mlyambina aliipongeza Kamati ya TEHAMA chini ya Naibu Msajili wa Divisheni ya Kazi, Mhe. Mary Mrio kwa kuja na ubunifu huo na kuwaomba waendelee kujifunza zaidi ili waje na ubunifu zaidi utakaosaidia Mahakama kwa ujumla.
Msimbo wa majibu ya haraka (QR code) ni msimbo wa machoni unaoonekana katika umbo la mraba na huhifadhi data iliyofichwa. Pia unaweza kuchukuliwa kama njia ya kuhifadhi data, kama vile diski ya kidole (thumb drive), inayotumika kuunda vitu vya masoko ya kidijitali kwenye vitu vya kimwili kupitia huduma za haraka za simu.
Matukio katika picha-Uzinduzi wa 'QR Code' Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya Kazi tarehe 25 Julai, 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni