Jumamosi, 26 Julai 2025

WATUMISHI WA MAHAKAMA KIGAMBONI WASHIRIKI MAFUNZO YA HUDUMA KWA MTEJA, UDHIBITI WA MSONGO WA MAWAZO

Na DHILLON JOHN, Mahakama-Dar es Salaam 

Katika jitihada za kukuza na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Mahakama, Mahakama ya Wilaya Kigamboni imetoa mafunzo kwa Watumishi wake wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama zake za Mwanzo juu ya utoaji huduma kwa mteja na jinsi ya kukabiliana na msongo wa mawazo ili kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika jana tarehe 25 Julai, 2025 yalilenga kuboresha huduma kwa wateja na kufanya watumishi kuondokana na msongo wa mawazo.

Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyikia katika Mahakama ya Wilaya Kigamboni Dar es Salaam, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale ambaye pia alikuwa Mkufunzi wa mafunzo hayo alisema, “ni ukweli ulio wazi kwamba, utoaji huduma kwa mteja mzuri unastawisha huduma za kimahakama, pia kuondoa msongo wa mawazo kunasaidia watumishi kuwa na ari, furaha na kuweza kufanya kazi zake katika amani na upendo.”

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yanasaidia kuwapatia watumishi mbinu bora za utoaji huduma na ujuzi wa kuondokana na msongo wa mawazo.

“Namna mojawapo ya kuondoa msongo wa mawazo ni kuishi katika kipato unachopata, kuweza kutunza kipato ili kutokupata msongo wa mawazo wakati unapopata shida,” alisema Jaji Ngunyale.

Kwa upande mwingine, Mhe. Ngunyale alielezea tiba ya kuondoa msongo wa Mawazo ni pamoja na kutochukulia mambo kwa hasira, kupunguza matumizi ya mitandao ya kijamii kwa maudhui ambayo si ya kuelimisha, kuepuka maudhi, kutunza kipato ambapo alisisitiza kuwa, kwa kufanya hayo itakuwa ni tiba katika kuondoa msongo wa mawazo au afya ya akili.

Jaji Ngunyale alishukuru na kuwapongeza watumishi kwa ushirikiano wao madhubuti katika mafunzo na kwa maswali na kujibiwa na watumishi wenyewe, na kukiri kuwa hatua hiyo imeonesha kuwa, wameelewa na wapo tayari kuboresha huduma kwa mteja, kutokupata msongo wa Mawazo na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Naye, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani nchini Ujerumani ambaye pia ni Mratibu wa zamani wa Masuala ya Usuluhishi wa Kimahakama katika Mji wa Berlin, Mhe. Anne-Ruth Moltmann-Willisch alisema kuwa, mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa Tanzania na Ujerumani kupitia njia za usuluhishi.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Mwanakombo Twaib alitoa shukrani kwa Mhe. David Ngunyale Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo alisema, “kutokana na mafunzo haya tutabadilika na kuwa watumishi bora wenye kufanya kazi kwa bidii na weledi pia.”

Mhe. Mwanakombo alimuomba Jaji Ngunyale asiwachoke pale wanapomuhitaji kwa mafunzo na nasaha zake ili kuimarisha utoaji haki kwa wakati.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale akitoa mada wakati wa mafunzo kwa Watumishi wake wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama zake za Mwanzo yaliyofanyika jana tarehe 25 Julai, 2025.

Washiriki wa mafunzo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Mwanakombo Twaib akishiriki katika mafunzo hayo yaliyokuwa yakitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale (hayupo katika picha). 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya-Kigamboni mara baada ya mafunzo. Wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Mwanakombo Twaib, wa tatu kulia ni Mhe. Christina Lugulu, Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo-Kigamboni.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama-Kigamboni jijini Dar es Salaam.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni