- Watakiwa kushiriki michezo mbalimbali kuimarisha afya
Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga
Watumishi wa Mahakama wanachama wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kufanya vikao vya mara kwa mara kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanahusu maslahi yao ya kiutumishi.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa TUGHE Mahakama ya Tanzania, Bw. Michael Masubo alipokutana na wanachama hao tarehe 25 Julai, 2025 Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwa lengo la kujitambulisha na kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na chama hicho cha Wafanyakazi.
Akielezea faida za kujiunga na Chama hicho, Bw. Masubo alisema kuwa, moja ya faida za kujiunga na chama hicho kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa watumishi mahala pa kazi.
Bw. Masubo aliwataka pia wanachama kuipitia Katiba ya Chama hicho kwani kuna mambo mengi yaliyoainishwa ambayo yana faida kubwa kiutumishi ikiwemo uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa Mahakama kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, Bw. Masubo alisisitiza juu ya uundwaji wa Kamati za Wanawake ambazo zimekuwa chachu ya kudhibiti mienendo isiyofaa kwa wanachama wanawake mfano mavazi na kuimarisha tabia njema kwa watumishi wanawake.
Aidha, aliwataka Wenyeviti na Makatibu wa Matawi ya TUGHE Mahakama kuhudhuria vikao vya Menejimenti kuelezea changamoto mbalimbali za wanachama wao kwani wao ni wajumbe wa vikao hivyo kwakuwa kushiriki katika vikao hivyo husaidia kupunguza malalamiko na stahiki zao kushughulikiwa kwa wakati.
Hali kadhalika, Bw. Masubo aliwahamasisha watumishi ambao sio wanachama wa TUGHE Shinyanga kujiunga na Chama hicho kwani kina faida nyingi ikiwemo kutambua maslahi yao na kuyafuatilia kupitia vikao mbalimbali na hatimaye hoja za jumla kupata fursa ya kuwasilishwa katika vikao vya Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Taifa linaloketi kila mwaka.
Katika hatua nyingine, Bw. Masubo aliipongeza Timu ya Mpira wa Miguu ya Mahakama FC (wanaume) ya Kanda ya Shinyanga kwa kuibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya Mei Mosi, 2025 na kujinyakulia zawadi mbalimbali zikiwemo jezi, mipira na tuzo maalum kwa Mshindi. Aliongeza kwa kuwasisitiza watumishi kushiriki katika michezo mbalimbali na kufanya mazoezi kuimarisha afya pamoja na kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa kama vile Shinikizo la Damu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watumishi wa Mahakama ambao pia ni wananchama wa TUGHE Shinyanga walisema kuwa, wamefarijika kupata elimu na kufahamu faida za kujiunga na chama hicho. Waliwasilisha maoni mbalimbali kwa Katibu huyo, kuhusu uimarishwaji wa Matawi ya TUGHE katika ngazi za Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mahakama ya Tanzania, Bw. Michael Masubo akihamasisha watumishi wa Mahakama Shinyanga kujiunga na Chama hicho.
Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama Kuu ya Tanzania, Bi. Editha Haule akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Sehemu ya Watumishi na wananchama wa TUGHE Shinyanga wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa TUGHE Mahakama ya Tanzania (hayupo katika picha) wakati alipokutana na watumishi wa Mahakama Shinyanga.
Katibu Mkuu wa TUGHE Mahakama ya Tanzania, Bw. Michael Masubo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi na Wanachama wa TUGHE Shinyanga wakati alipowatembelea wanachama hao tarehe 25 Julai, 2025.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni