Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali amewaelekeza viongozi wa Mahakama ngazi zote Kanda ya Arusha kusimamia ipasavyo vituo vyao vya kazi ili kuhakikisha vituo hivyo vinamaliza mashauri mengi zaidi ya yale yanayosajiliwa.
Mhe. Mahimbali ametoa rai hiyo leo 30 Julai, 2025 katika Kikao cha Menejimenti ya Kanda ya Arusha ambapo amesisitiza kuwa kazi ya msingi ya Mahakama ni usikilizaji wa mashauri, hivyo, ni lazima uhalisia huo ujioneshe katika ufanyaji kazi wa kila siku kwa kuhakikisha kuwa viongozi wanatimiza wajibu wao ipasavyo na hatimaye kuondokana na kutengeneza mashauri ya mlundikano yasiyo na sababu za msingi.
“Kila ngazi ya Mahakama ikae na kutafsiri vizuri takwimu za mashauri zilizowasilishwa hapa na kujiwekea mikakati yao wenyewe kuhakikisha hali ya usikilizaji wa mashauri inakuwa bora na kuepuka kuwa na mashauri ya mlundikano yasiyokuwa na sababu za msingi,” amesema Jaji Mahimbali.
Aidha, Mhe. Mahimbali amewaelekeza pia viongozi katika ngazi zote za Mahakama Kanda ya Arusha kuhakikisha kuwa hawatengenezi malalamiko yanayotokana na wateja kutopewa nakala za hukumu kwa wakati, kuzingatia utunzaji wa majengo ya Mahakama, kuhakikisha hati za umiliki wa maeneo ya Mahakama zinapatikana, viongozi na watumishi kujua mikakati na mipango ya Kitaifa na Mahakama kama vile Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na mipango mbalimbali ya Mahakama inayoendelea kutekelezwa.
Jaji Mfawidhi huyo amesisitiza pia ushirikiano baina ya viongozi na kuepuka migogoro isiyo na tija kazini pamoja na kuhakikisha kwamba watumishi wote wanafanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji wa hali ya juu.
Akiwasilisha taarifa ya mashauri, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Elia Mrema amesema kuwa, hali ya usikilizaji wa mashauri inakwenda vizuri na kwamba katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi Julai 29, 2025 Mahakama Kuu Arusha ilipokea jumla ya mashauri 411 na kwamba jumla ya mashauri 756 yalisikilizwa katika kipindi hicho.
Kadhalika, Mhe. Mrema ametoa pia taarifa ya mashauri ya Mahakama za Hakimu Mkazi, Wilaya na Mwanzo kwa pamoja kuwa hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2025 Mahakama hizo zimesikiliza jumla ya mashauri 5,245 na kubakiwa na mashauri 1,541 yanayoendelea kusikilizwa.
Naibu Msajili huyo ametaja changamoto zinazojitokeza wakati wa zoezi zima la ufunguaji wa mashauri ambazo ni baadhi ya wadaawa kukosea dirisha la kufungulia mashauri katika mfumo wa kielektroniki wa mashauri (e-CMS), baadhi ya wadaawa kutofautisha majina wanayoandika katika mfumo wa kielektroniki na yale yanayoonekana kwenye nyaraka ngumu (hardcopy pleadings) wanazowasilisha Mahakamani kwa ajili ya kufungua kesi.
Ametaja changamoto nyingine ni pamoja na wadaawa na Mawakili kufuata namba ya malipo (control number) mahakamani wakati wangepata namba hizo za malipo katika mfumo waliotumia kusajili mashauri yao (e-CMS) na kukiri kuwa hali hiyo imekuwa ikileta usumbufu na kuchukua muda mwingi kwa mtoa huduma mahakamani kuwahudumia.
Naye Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Arusha, Bi. Grace Kapama akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama Kuu Kanda ya Arusha pamoja na mambo mengine, amesema kuwa Mahakama katika Mkoa wa Arusha imeweka mpango wa mafunzo ndani ya Kanda katika mwaka huu wa 2025/2026 kwa lengo la kuwapa maarifa watumishi wa kada zote na hatimaye kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa Mahakama.
Sambamba na hilo, Bi. Grace amesema pia kwamba ukarabati wa Mahakama za Mwanzo utaendelea kupewa kipaumbele katika mwaka huu wa fedha hususani katika Mahakama za Mwanzo Arusha Mjini, Mto wa Mbu, Mbuguni na Endabash.
Kikao hicho kimejadili masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa shughuli za Mahakama katika Kanda ya Arusha na namna ya kuboresha utendaji kazi kwa lengo la kuhakikisha kuwa Kanda hiyo inakuwa mfano bora wa kuigwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati.
Viongozi wa Mahakama wa ngazi mbalimbali mkoani Arusha wamehudhuria kikao hicho na wameaswa kuzingatia taratibu na maadili ya kazi wanapofanya majukumu yao na kuhakikisha kuwa watumishi walio chini yao wanafanya kazi kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akifungua kikao cha Menejimenti cha Kanda hiyo leo tarehe 30 Julai, 2025 kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha. Kushoto ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Arusha, Bi. Grace Kapama.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Arusha, Mhe. Amir Msumi akifafanua jambo wakati wa Kikao cha Menejimenti
cha Kanda ya Arusha leo tarehe 30 Julai, 2025 kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano
wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Elia Mrema (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya mashauri wakati wa Kikao cha Menejimenti cha Kanda ya Arusha kilichofanyika leo tarehe 30 Julai, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bi. Grace Kapama akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama wakati wa Kikao cha Menejimenti cha Kanda ya Arusha kilichofanyika leo tarehe 30 Julai, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
Wajumbe mbalimbali waliohudhuria Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Kanda ya Arusha kilichofanyika leo tarehe 30 Julai, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni