Alhamisi, 31 Julai 2025

MAJAJI MAHAKAMA KUU YA TANZANIA WAJIANDAA KWA UENDESHAJI MASHAURI YA UCHAGUZI

·       Jaji Kiongozi asisitiza uendeshwaji wa mashauri hayo kwa weledi na kukamilika kwa wakati

 Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ametoa rai kwa Majaji wa Mahakama Kuu nchini kuhakikisha usikilizwaji na uamuzi wa mashauri yote ya uchaguzi unakuwa wa haki, haraka kadri inavyopaswa pamoja na kutojifunga na mbinu za kiufundi.

 Mhe. Dkt. Siyani ametoa rai hiyo leo tarehe 31 Julai, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania yaliyofanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual Court).

Mhe. Dkt Siyani ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Majaji wa Mahakama Kuu juu ya nafasi ya Mahakama katika kuimarisha amani na utulivu wa nchi na hivyo kujenga mazingira ya kukua kwa uchumi. Aidha, Jaji Kiongozi amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanaweka utaratibu madhubuti wa kushughulikia mashauri hayo kwa haraka, haki, na ufanisi mkubwa, ili kudumisha imani ya wananchi kwa chombo hiki muhimu cha utoaji wa haki.

Akisisitiza juu ya umuhimu wa kuamuliwa kwa mashauri ya uchaguzi kwa haraka, Jaji Kiongozi ameeleza kuwa, mchakato wa uchaguzi huendana na uwepo wa mivutano ya kisiasa, hisia kali za jamii, na matarajio makubwa kutoka kwa wadau wa demokrasia, hivyo ni wajibu wa Mahakama kuhakikisha mashauri yatokanayo na migogoro hiyo ya uchaguzi, yanapewa kipaumbele na kusikilizwa kwa wakati.

“Kama ilivyo kwa aina nyingine za mashauri, ni muhimu sana kwa Majaji watakaosikiliza mashauri ya uchaguzi, kuwa waadilifu, wenye weledi wa hali ya juu na kasi katika usikilizaji wa mashauri hayo. Ni kwa kufanya hivyo wananchi watakaochagua viongozi wao kwa kuwapigia kura na viongozi wataochaguliwa kwa kupigiwa kura, wapate fursa ya kuendelea na ujenzi wa nchi.” Ameeleza Dkt. Siyani

Jaji Kiongozi amesema kuwa, mafunzo hayo yanayofanyika wakati ambao Taifa letu linaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, yamelenga kuimarisha uwezo na uelewa wa Majaji kuhusu misingi ya kikatiba na kisheria kuhusu mashauri ya uchaguzi nchini na hivyo amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo, kujiweka tayari kutimiza wajibu wao kwa ufanisi.

“Matumaini yangu ni kuwa mafunzo haya na mengine yatakayofuatia, yatawawezesha kuwa na viwango vya juu vya weledi, ufanisi na maadili zaidi katika kutimiza majukumu yenu. Muhimu ambalo ningependa kulisisitiza ni kuwa mchakato wa uchaguzi na utatuzi wa migogoro inayotokana na mchakato huo, ni kipimo kwa Mahakama,” amesisitiza Mhe. Dkt. Siyani.

Jumla ya Majaji 103 wa Mahakama Kuu wameshiriki mafunzo hayo ya siku moja kwa njia ya mtandao.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akifungua Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania yaliyofanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual Court) leo tarehe 31 Julai, 2025.

Sehemu ya washiriki (Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania) walioshiriki Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania yaliyofanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual Court) leo tarehe 31 Julai, 2025.

(Picha na INNOCENT KANSHA, Mahakama)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni