Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kivukoni/Kinondoni-Dar es Salaam, Mhe. Is-haq Kuppa amewakumbusha Mahakimu wa
Mahakama za Mwanzo za Wilaya ya Kinondoni na Ubungo kutekeleza maelekezo ya Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju juu ya watuhumiwa Mahakama za Mwanzo
kudhaminiwa kwa masharti rahisi.
Mhe. Kuppa aliyasema hayo jana tarehe 31 Julai, 2025 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichojumuisha Mahakimu wa Mahakama hizo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni.
Mahakimu hao walikumbushwa pia, kwa Mahakama za Mwanzo ambazo makosa pamoja na adhabu zake kwa kuwa ni ndogo, zisizokuwa na taratibu ngumu za kisheria katika kushughulika nayo hawapaswi kuwa na uwepo wa Mahabusu kama miongozo mbalimbali kama vile muongozo wa kushugulikia dhamana (Bail Guideline) unavyoongoza.
Aidha, Mfawidhi hyo aliendelea kusema kwamba, sambamba na hilo shauri linapofika siku ya kwanza mahakamani halipaswi kuahirishwa kwa kuwa wahusika wote yaani mlalamikaji na mshtakiwa huwepo.
“Likifanyika hili litasaidia pia kutochelewesha mashauri na yatamalizika mapema na kwa wakati hivyo kupelekea dhana ya utoaji haki kwa wakati itimie,” alisisitiza Mhe. Kuppa.
Pamoja na maelekezo hayo, ulitolewa mwongozo wa kutumia Mfumo wa Ki-elektroniki wa Upimaji wa Wazi Utendaji Kazi wa Maafisa wa Mahakama (e-JOPRAS), Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wakiwa kama sehemu ya Maafisa hao walijulishwa kwamba kwa kuwa wanapimwa moja kwa moja na Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya zao wanapaswa kutekeleza ujazaji wake mara tu wanapopimwa na viongozi wao.
Ilisisitizwa kwamba, mfumo huo ni wa wazi na wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa vipengele vilivyowekwa kama vile uadilifu, ubunifu na kutojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili kama vile rushwa na kadhalika kwa kuwa watakuwa wanapimwa na kupewa alama ambazo zitakuwa za wazi na stahiki na kila mtu atakayepimwa kwa mujibu wa mwenendo wake hivyo ni jukumu la kila mmoja kuwajibika juu ya hilo.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mhe. Jacqueline Rugemarila aliwaelekeza wahusika kwa vitendo juu ya mfumo wa e-JOPRAS ambapo kila mwenye changamoto alisaidiwa hapohapo kwa msaada wa karibu wa Afisa TEHAMA wa Kituo hicho, Mhandisi Delphina Mwakyusa.
Kikao kazi hicho ni matokeo ya msisitizo wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi aliotoa katika kikao cha viongozi Kanda hiyo mapema mwezi Julai mwaka huu ambapo moja ya maazimio yake ni kufanya vikao kazi ili kukumbushana majukumu.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Kinondoni na Ubungo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni/Kinondoni, Mhe. Is-haq Kuppa (aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo za Wilaya za Kinondoni na Ubungo kilichofanyikia jana 31 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mhe. Jacqueline Rugemarila akiwaelekeza Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo namna ya kujaza taarifa za utendaji kwenye Mfumo wa Ki-elektroniki wa Upimaji wa Wazi Utendaji Kazi wa Maafisa wa Mahakama (e-JOPRAS).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni