Ijumaa, 1 Agosti 2025

KAMILISHENI KWA WAKATI MASHAURI YA KIKATIBA YANAYOHUSIANA NA UCHAGUZI; JAJI MKUU

  • Asisitiza pia uadilifu, ubunifu, umahiri katika kazi, kujiongeza, kuweka mbele maslahi ya Taifa kwa manufaa ya umma

 Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju amewataka Majaji na Mahakimu nchini kumaliza kwa wakati mashauri yote ya kikatiba yaliyopo mahakamani yanayohusiana na mchakato wa uchaguzi ili kuleta imani kwa umma dhidi ya Mahakama pamoja na kutoa fursa kwa watu waliofungua mashauri hayo kuwa na uhakika na kinachoendelea kuhusu mchakato wa uchaguzi. 

Mhe. Masaju alitoa rai hiyo jana tarehe 31 Julai, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa salamu kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliokuwa wakishiriki katika Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yaliyofanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual Court).

“Sote tunajua tutakuwa na Uchaguzi Mkuu mwezi wa 10 mwaka huu, lakini hapa katikati tunafahamu kuwa, kuna watu wamefungua kesi mahakamani zinazohusiana na hizo sheria za uchaguzi na mchakato wa uchaguzi kwa ujumla, ushauri wangu ni kwamba hizi kesi tuzimalize mapema ili kutoa fursa watu kuwa na uhakika na kinachoendelea kuwa na (certainty of electoral process) na kama kuna sababu yoyote ya kuchelewesha iwe ni sababu ya msingi ya kufanya hivyo,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema kuwa, suala la kutochelewesha haki ni takwa la kikatiba kwa Mahakama na ni kwa mujibu wa Ibara ya 107A (2) na Dira ya Mahakama ya Tanzania nayo inahimiza kutoa haki inayopatikana kwa wote mapema ipasavyo.

Jaji Mkuu alisema kuwa, wananchi wana imani kubwa na Mahakama katika kutafsiri sheria na kutoa haki hivyo ni muhimu kusikiliza mashauri hayo na mashauri mengine yaliyopo mahakamani mapema iwezekanavyo ili kuendeleza imani ambayo wananchi wanayo juu ya Mahakama.

Aidha, Jaji Mkuu aliwakumbusha Majaji, Mahakimu, Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea kurejea hotuba yake aliyowasilisha tarehe 03 Julai, 2025 jijini Dodoma wakati wa Sherehe za Kuwakubali Mawakili wapya ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka kuendelea kuzisoma Sheria za Uchaguzi na kuzifahamu ipasavyo ili ziweze kuwasaidia wakati wa mchakato wa uchaguzi na uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.

Alizitaja Sheria hizo kuwa ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Madiwani na Wabunge, Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Polisi na sheria zote zinazosimamia mchakato mzima wa uchaguzi.

Akizungumzia kuhusu Mafunzo ya Siku moja ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Masaju alimpongeza Jaji Kiongozi, Watoa Mada, Waratibu na Kamati ya Jaji Mkuu ya Mafunzo kwa ubunifu wa kuandaa mafunzo hayo na kuwataka Majaji hao kuuliza, kuchangia na kutoa ushauri ili kuwa na uelewa wa pamoja katika ushughulikiaji wa mashauri ya uchaguzi.

Kadhalika, Jaji Mkuu amesema pia, kuwa ni muhimu kwa Majaji na watumishi wote wa Mahakama nchini kuzingatia mambo muhimu katika utumishi wa umma na utawala wa sheria ambayo ni pamoja na umakini katika masuala yanayohusu haki kwa kuhakikisha kuwa haki inasimamiwa ipasavyo, kuwa na uadilifu, umahiri katika kazi, ubunifu, kujiongeza katika kazi na kuweka mbele maslahi ya Taifa ambayo pia ni maslahi ya umma.

“Kuna vitu ambavyo ningependa kuwashirikisha, vinavyohusu utumishi wetu wa kila siku hapa mahakamani na hivi inabidi tuviongeze kwenye Tunu zetu za Mahakama, kama mnavyofahamu sisi wajibu wetu ni kutenda haki na katika Mihimili mitatu ya Dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama, Mahakama ndio yenye kauli ya mwisho kwenye kutoa haki, hivyo sisi tuliopewa jukumu hili tuna wajibu mkubwa wa kusimamia uadilifu, ubunifu, umahiri katika kazi, kujiongeza katika kazi na kuweka mbele maslahi ya Taifa kwa manufaa ya umma,” alisisitiza Mhe. Masaju.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Jaji Kiongozi na Majaji wote wa Mahakama Kuu, Jaji wa Mahakama Kuu-Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke, Mhe. Sarah Mwaipopo alimshukuru Jaji Mkuu kwa maneno ya hekima aliyowapatia na kumuahidi kwamba watayazingatia na kumpatia ushirikiano utakaowezesha kutekeleza ipasavyo jukumu la utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju.




 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni