Na Yusufu Ahmadi- IJA
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA) na Mahkama ya Zanzibar zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha
ufanisi na uwezo wa Maafisa wa Mahakama na maafisa wengine wakiwemo Makadhi
kupitia mafunzo, utafiti na uendelezaji wa uwezo wa kitaasisi.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarehe
5 Agosti 2025 Chuoni Lushoto baina ya Maafisa wa Chuo na wa Mahkama ya Zanzibar
na kushuhudiwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla pamoja na Mkuu
wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo.
Miongoni mwa maeneo ya makubaliano
hayo ni kutoa mafunzo kwa maafisa wa Mahkama na wengineo wa Mahkama ya Zanzibar,
kuandaa na kutoa mafunzo ya uongozi na usimamizi, na kukuza uwezo wa
utafiti wa kisheria na uvumbuzi katika utendaji wa Mahakama.
Maeneo mengine ni kutoa mafunzo
endelevu ya Kimahakama, mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watendaji wa Mahkama
ya Zanzibar pamoja na kuandaa kwa pamoja warsha, makongamano, semina na
mikutano ya kitaaluma.
Akizungumzia utiaji saini huo Mhe.
Dkt. Kihwelo amesema kuwa Chuo kitahakikisha makubaliano hayo yanafikia malengo
yake kwa kutoa mafunzo kwa makundi yaliyokusudiwa katika makubaliano hayo.
Pia ameongeza: “Makubaliano haya ni
sehemu ya Chuo kuimarisha upatikanaji wa haki kwa kuwajengea uwezo maafisa
wenzetu wa Mahkama na makundi mengine na hivyo kuimarisha ufanisi wa utendaji.”
Kwa upande wake, Mhe. Abdalla
ameelezea imani yake kuwa makubaliano haya yatazaa matunda.
“Ni matarajio yangu na Mahkama ya
Zanzibar kwamba mashirikiano haya yatazaa matunda kwa maslahi ya Mahkama, Chuo
na Tanzania kwa ujumla,” amesema Mhe. Abdalla.
Pia ameongeza kuwa IJA na Mahkama ya
Zanzibar vimekuwa na ushirikiano kwa miaka mingi na kwamba makubaliano haya ni
sehemu ya kurasimisha ushirikiano huo uliyodumu kwa muda mrefu.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya
Mafunzo ya Mahkama ya Zanzibar ambaye pia ni Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe.
Khadija Shamte Mzee amebainisha kuwa walifanya tathminii ili kujua ni maeneo
gani ya mafunzo wao hawako vizuri, na hivyo kuamua kuingia makubaliano na IJA
ili kuwezesha maeneo hayo.
Makubaliano hayo yameshuhudiwa na wajumbe
wengine wa Mahkama ya Zanzibar na Wajumbe wa Menejimenti ya Chuo.
Wajumbe wa IJA wakiwa katika hafla hiyo ya utiaji saini.
Maafisa wa IJA na wa Mahkama ya Zanzibar wakisaini hati za makubaliano
Mkuu wa
Chuo Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani
Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akizungumza katika hafla hiyo.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Mafunzo ya Mahkama ya Zanzibar ambaye pia ni Jaji wa Mahkama Kuu
Zanzibar, Mhe. Khadija Shamte Mzee akisema jambo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla akizungumza katika hafla hiyo
Jaji
Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya IJA.
Jaji
Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na wajumbe wa Mahkama ya Zanzibar wakati wa hafla ya kusaini Hati ya Makubaliano
(MoU) baina ya IJA na Mahkama hiyo ya Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni