- Kutokana na mchango kwenye upatikanaji juzuu za sheria zaidi ya 400
Na FAUSTINE KAPAMA na
ARAPHA RUSHEKE-Mahakama, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mhe. Hamza Johari amekabidhi Tuzo maalum kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju na Mahakama ya Tanzania kutokana na
mchango waliotoa kufanikisha upatikanaji wa Juzuu za Sheria 446 zilizofanyiwa
urekebu.
Hafla ya kukabidhi Tuzo
pamoja na nakala 20 ya Juzuu hizo ilifanyika katika Ofisi ya Jaji Mkuu iliyopo
kwenye Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na
kuhudhuriwa na Viongozi kadhaa wa Mahakama, akiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali aliabatana na Viongozi mbalimbali kutoka Ofisi yake kwenye hafla hiyo, wakiwemo Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi na Mwandishi
Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole. Mhe. Masaju alipokea Tuzo
ya Mahakama pamoja na Juzuu hizo kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania.
Akizunguza katika hafla
hiyo, Jaji Mkuu aliishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua
mchango wake binafsi na wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla katika kufanikisha
zoezi la upatikanaji wa Juzuu hizo.
Alielezea namna yeye
binafsi alivyoshiriki tangu akiwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadaye
Ikulu na pia Mahakama ilivyotoa mchango wake kwenye hatua mbalimbali
kufanikisha upatikanaji wa Juzuu hizo.
"Sisi ni watumiaji
wakubwa wa Juzuu kama hizi maana mambo yote ya kisheria huishia mahakamani. Kwa
hiyo, juzuu hizi ni muhimu sana kwetu," alisema.
Mhe. Masaju alisema kuwa
ushirikiano uliopo kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mahakama
udumu kwani ofisi hiyo ni Wadau wakubwa.
Kabla ya kukabidhi Tuzo
na Juzuu hizo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimweleza Jaji Mkuu kuwa wamefanya
zoezi la urekebu wa sheria mbalimbali na baada ya kukamilisha zilizinduliwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutamka kuwa sheria hizo zitaanza
kutumika kuanzia tarehe 1 Julai, 2025.
"Mpango wetu ulikuwa
tukukabidhi kabla ya tarehe 1 Julai, 2025. Kutokana na mwingiliano wa majukumu
pale bungeni mwishoni tulishindwa kukukabidhi mapema," alisema.
Akizungumzia zoezi la
urekebu wa sheria hizo, Mwandishi Mkuu wa Sheria alieleza kuwa seti waliyoleta
ina Juzuu 20 zenye Sheria 446 na wameingiza marekebisho yote mpaka ya Mwezi Desemba
2023 na wanakamilisha marekebisho mengine ya mwaka 2024, ikiwemo Sheria za
Uchaguzi.
Alimweleza Jaji Mkuu kuwa zoezi hilo limekuwa la muda mrefu kama yeye anavyofahamu na amekuwa akiwasaidia kwenye kila hatua. Bw. Njole alisema pia kuwa zoezi hilo limefanywa na Watalaam wa ndani na uchapishaji umefanywa na kampuni ya Kitanzania.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari-juu na chini-akitoa maelezo mafupi kabla ya kukabidhi Tuzo na Juzuu hizo kwa Jaji Mkuu, huku Viongozi wengine wakifuatilia kilichokuwa kinajiri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni