Ijumaa, 4 Julai 2025

JAJI KAHYOZA AWAPONGEZA WATUMISHI MAHAKAMA YA WILAYA MASWA KWA KAZI NZURI

Na EMMANUEL OGUDA , Mahakama-Shinyanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza amewapokeza watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa kwa kutekeleza ipasavyo nguzo namba mbili ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya Utoaji wa Haki kwa wote na kwa wakati.

Mhe. Kahyoza aliyasema hayo tarehe 03 Julai, 2025 wakati akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu akiwa katika ziara ya ukaguzi wa katika Mahakama hiyo.

“Niwapongeze watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa hakuna mashauri yanayozidi miezi sita isipokuwa shauri moja tu. Niwashukuru kasi ya usikilizwaji wa mashauri ni nzuri, kwa Mahakama za Mwanzo umri wa shauri Mahakamani ni miezi sita, mnaweza kufikiria kushusha zaidi umri wa shauri mahakamani ikiwa ni mikakati ndani ya Kanda kuhakikisha hatuzalishi mashauri ya mlundikano lakini wadaawa wa Mahakama wanapata haki zao kwa wakati’’ alisema Mhe. Kahyoza.

Aidha, Jaji Kahyoza alitoa rai kwa Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga kujipima kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania wa (2020/2021 – 2024/2025) na kijitathmini iwapo nguzo tatu zilizopo kwenye mpango huo kama zimetekelezwa kikamilifu.

“Nguzo ya kwanza ya Mpango Mkakati ni Utawala Bora na Usimamizi wa Rasilimali, katika kutekeleza nguzo hii yatupasa tuhakikishe haki za watumishi zinalindwa, watumishi wa Mahakama wapate haki zao kwa wakati pamoja na kuhakikisha mali za Mahakama zinasimamiwa ipasavyo, kila mmoja anapaswa kujipima ametekelezaje nguzo hii,’’ alisisitiza Mhe. Kahyoza.

Kadhalika Mhe. Kahyoza ametilia mkazo nguzo ya pili ya Utoaji wa Haki kwa wote na kwa wakati pamoja na nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama  kwa kuwataka watumishi wa Mahakama kuongeza imani kwa wananchi, kudumisha ushirikishaji wa wadau kwa kufanya vikao mbalimbali.

“Tunafanya kazi na wadau mbalimbali, tusigombane, tushirikiane na wadau na kutoa uamuzi kwa misingi ya haki. Katika nguzo namba mbili suala la nidhamu kwa watumishi wa Mahakama linahitaji kuzingatiwa sana, tuendelee kuwa wasafi katika kazi zetu, hukumu zitolewe kwa misingi ya haki, Hakimu ukipokea rushwa unapoteza uhuru wako na wa Mahakama katika kutoa uamuzi, tuendelee kuelimishana, kuelekezana na kukumbushana kuhakikisha nguzo hizi tatu za Mpango Mkakati wa Mahakama zinatekelezwa kikamilifu na matokeo yanaonekana ili kuifikia Dira ya Mahakama ya Tanzania ya utoaji wa haki kwa wote na kwa wakati,’’ aliongeza Jaji Kahyoza.

Aidha, Mhe. Kahyoza aliwaeleza watumishi hao kuwa, Dira ya Mahakama ya Tanzania ni kutoa Haki sawa kwa wote na kwa wakati huku akibainisha kuwa, watumishi wa Mahakama wanapimwa na mambo makuu mawili, moja, muda ambao mashauri yanaishi mahakamani tangu kufunguliwa kwa shauri hadi kumalizika na pili ni kiwango cha ongezeko la imani ya wananchi kwa Mahakama, hivyo aliwataka kila mmoja anapofanya kazi ajue anachangia vipi kukamilisha malengo ya Mahakama ya Tanzania.

“Mkifanya kazi ya utoaji wa haki vizuri wananchi wataona na watafurahi zaidi. Kwa sasa Mahakama ipo kidijitali kwa Hakimu ambaye hutafanya vizuri utaonekana na Viongozi wetu hivyo, niwaombe tuongeze uwajibikaji katika kutimiza majukumu ya utoaji haki. Tuimarishe pia usajili wa mashauri kwa njia ya (Primary Court Mobile App) kwani eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) linaangaliwa kwa karibu kupitia nguzo hii ya utoaji haki kwa wakati,” alisisitiza.

Aliongeza kwamba, TEHAMA ni njia mojawapo ya kusogeza huduma kwa wananchi na msimamo uliopo ni kutorudi nyuma katika matumizi ya TEHAMA, hivyo aliwasihi wasiwe chanzo cha kulalamikiwa kwa kutoa huduma mbovu bali wananchi wapewe taarifa kwa kila changamoto inayojitokeza mahakamani inayosababisha mashauri yao kuchelewa.

Hali kadhalika, Mhe. Kahyoza alizungumza na wananchi waliokuwa wakisubiri kupata huduma Mahakama ya Wilaya ya Maswa sambamba na kutembelea ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyalikungu iliyopo wilayani humo ambapo amehimiza ukamilishwaji wa jengo hilo kwa haraka.

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Asha Mwetindwa amesema kuwa, kwa sasa malalamiko ya wananchi yamepungua kwa kiasi kikubwa, aliwataka Mahakimu na watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga kuendelea kuhudumia wananchi kikamilifu.

Vilevile aliwataka watumishi hao kuweka kumbukumbu za maulizo ya wananchi ili kubaini maswali yanayoulizwa mara kwa mara na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.

Jaji Kahyoza yupo katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama Mkoa wa Simiyu ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu ahamishiwe ndani ya Kanda hiyo ambapo anatarajia kukagua Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mahakama za Wilaya Maswa, Meatu na Bariadi.

   Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa (hawapo katika picha) wakati wa ziara ya ukaguzi tarehe 03 Julai, 2025.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe John Kahyoza (hayupo katika picha) alipofanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama hiyo tarehe 03 Julai, 2025.

 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Asha Mwetindwa akisisitiza jambo wakati wa ziara ya ukaguzi Mahakama ya Wilaya Maswa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza akiwa katika Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Nyalikungu Maswa wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama hiyo.


Muonekano wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyalikungu Maswa lililopo katika ujenzi.

    
Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Maswa, Bw. Ezekiel Tippe akimuonesha Jaji Mfawidhi mipaka ya Mahakama ya Mwanzo Lalago wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama Wilaya ya Maswa.

   Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza akizungumza na wananchi (hawapo katika picha) waliofika kupata huduma za kimahakama Wialaya ya Maswa wakati akiwa katika ziara ya ukaguzi tarehe 03 Julai, 2025.

Mmoja kati ya wananchi waliofika kupata huduma katika Mahakama ya Wilaya Maswa akipongeza utendaji kazi wa Mahakama baada ya Jaji Mfawidhi kuzungumza nao wakati wa ziara ya ukaguzi Mahakama hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)




8.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni