Jumanne, 19 Agosti 2025

TAASISI UTATU ZA HAKI JINAI ZATAKIWA KUREKEBISHA KASORO ZINAZOATHIRI UTENDAJI HAKI

 Na. Innocent Kansha na Arapha Rusheke - Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju, amefungua kikao kazi cha menejimenti na viongozi wa mikoa na wilaya kutoka Taasisi za Haki Jinai zinazounda Utatu katika Ukumbi wa Kituo cha Jakaya Kikwete Convention, Jijini Dodoma Agosti 19, 2025.

Akizungumza na washiriki, Jaji Mkuu Masaju alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa mshikamano na kwa uzito unaostahili akibainisha kwamba; haki ni msingi wa amani, maendeleo na ustawi wa Taifa.

“Tunapojihusisha na masuala ya haki, tunapaswa kulichukulia jukumu hilo kwa uzito, kwani haki ni msingi wa maisha ya pamoja na haki hupendwa na Mwenyezi Mungu. Huu ni mkutano wa muhimu ambao umenisukuma na mimi kuja. Nimeona kaulimbiu zenu ambazo ni za msingi sana. Nikianza na Mahakama ambao ni waalikwa, sisi tuna kanuni za uendeshaji wa ofisi ambazo ndiyo misingi mikuu inayotengeneza kaulimbiu na salamu kama ambavyo tumeziona hapa,” alisema Jaji Mkuu Masaju.

Mhe. Masaju aliongeza kuwa, Mahakama wao wana kitu kinaitwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, ‘ukiangalia hiyo misingi (core values) ya ofisi zenu inaleta imani kwamba, mmedhamiria kwa dhati kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi ipasavyo ili kudumisha amani na usalama wa Taifa,’ alisema.

Jaji Mkuu alisisitiza Sekta ya Sheria kuhakikisha inatenda haki kwani kwenye Dira ya Mahakama kuna kaulimbiu ambayo inasema haki sawa kwa wote ambayo ipo katika ibara ya ‘107A sub article 2 a na d ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inasema ‘kutenda haki sawa kwa wote mapema ipasavyo’ huku a na b ikisema, ‘kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi’ na ‘kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi.’

Akizungumzia changamoto zilizopo, Jaji Mkuu alibainisha kuwa ziara yake katika Gereza la Isanga ilimfanya abaini uwepo wa msongamano wa wafungwa gerezani, ucheleweshaji wa upelelezi na kesi, pamoja na malalamiko ya kunyimwa dhamana na watuhumiwa kuteswa wakiwa katika vituo vya polisi. Alisisitiza kuwa hatua za haraka zinahitajika kuhakikisha mfumo wa  haki unafanya kazi kwa ufanisi na haki inatendeka bila upendeleo.

“Nilipoenda Gereza Kuu la Isanga tarehe 10 Julai ,2025; nilipowasikiliza Wafungwa na Mahabusu, waliwasilisha malalamiko yao ya kucheleweshewa upelelezi na kwa Mahakama walilalamikia kwa wao kuchelewa kupewa vitabu kwa ajili ya kukata rufaa na hasa kwa wale wanaoenda Mahakama ya Rufani, lakini pia kuchelewa kupewa nakala za hukumu na mwenendo ili wakate rufaa zao, kuchelewa kusomewa mashtaka hasa kwa kesi zinazosikilizwa na Mahakama Kuu, kuchelewa kusikilizwa kwa rufaa zao na hususani Mahakama ya Rufani na matumizi mabaya ya kifungu cha 92 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai [Sura ya 20] kinachohusu kufutwa kwa mashtaka,” aliongeza Jaji Mkuu.

“Katika ziara hiyo, nilielekeza kwamba kwa mahabusu wa Mahakama za Mwanzo hakukuwa na sababu yeyote ya msingi kuwa na mahabusu wa mahakama hizo kwa sababu The Primary Courts Criminal Procedure Code ilipotungwa iliyafanya makosa yote yanayosikilizwa na Mahakama za Mwanzo kudhaminika.

kunakudhaminika kwa kuwa na wadhamini lakini pia hata kujidhamini. Kwa kipindi cha siku 21 baada ya maelekezo hakukuwa hata na mahabusu mmoja wa Mahakama za Mwanzo magerezani na hali hiyo imeendelea hivyo mpaka kwa taarifa ya jana, yaani 18 Agosti, 2025,” aliongeza Jaji Mkuu.

Akitoa agizo kwa Mahakimu wa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, Jaji Mkuu alielekeza wanajibu wa kuwajulisha washtakiwa kwenye makosa yenye dhamana kuwa kosa linadhaminika hata kama hawakuomba dhamana na kuwatajia masharti ya dhamana. Alisisitiza kuwa uamuzi wa ama  kutoa dhamana au kumnyima ufanyike siku hiyo hiyo ambapo mshtakiwa anayosomewa shtaka isipokuwa tu pale kunapokuwa na sababu za msingi za kuhairisha.

Aidha, alisisitiza kuwa Mahakama peke yake haiwezi kubeba jukumu la haki kwani Wadau wote wa mfumo wa haki jinai wanapaswa kushirikiana kwa dhati huku Majaji na Mahakimu wakipaswa kutenda haki bila hofu, chuki au upendeleo wowote.

Pamoja na hayo, Jaji Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, akibainisha kwamba haki ni kipaumbele kikuu cha maendeleo ya Taifa. Aliwakumbusha Washiriki kuzingatia na kuviishi viapo vyao kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais kwa Mahakama ya Tanzania kutenda haki kwa mujibu wa viapo vyao kwani vinaimarisha uwajibikaji wa kutoa haki bila woga au upendeleo.“Hakuna taasisi inayoweza kutoa haki peke yake; ushirikiano ni muhimu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wote,” alisema Jaji Mkuu.

Vilevile, Jaji Mkuu, Mhe. Masaju alisema kuwa, malalamiko kuhusu Watuhumiwa kunyimwa dhamana, kuteswa katika vituo vya polisi, kukaa muda mrefu vituoni, kuchelewa kusikilizwa kwa kesi zao na mambo mengine ya namna hiyo yanaathiri upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.

“Haya tunayoyaona ya msongamano wa wafungwa na mahabusu gerezani, kucheleweshwa kusikilizwa kesi au kucheleweshwa upelelezi au kuteswa na kuwekwa kwenye vituo kwa muda mrefu ni changamoto na kasoro za mfumo wa haki jinai katika Taifa letu, tunatakiwa tushughulike nazo changamoto hizi na tuzimalize,” amesisitiza Jaji Mkuu. ‘Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani alipokuwa ananiapisha kuwa Jaji Mkuu, pamoja na majukumu yanayojulikana Kikatiba na Kisheria lakini pia alinihimiza ni simamie haki, na wakati anazindua Dira alisema Mahakama ya Tanzania tendeni haki kwa mujibu wa viapo vyetu,” alisema.

Aidha, Jaji Mkuu akaongeza kuwa, ‘Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ndiyo inajukumu na uwezo wa kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini kwa mujibu wa Ibara 59 B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika Ibara ndogo ya 4 ambayo inasema Mkurugenzi wa Mashtaka katika kutekeleza mamlaka yake atakuwa huru na hataingiliwa na mtu yeyote au mamlaka yeyote na atazingatia mambo yafuatayo; nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu ya utoaji haki na kulinda maslahi ya umma.”

Alisema, kwenye zoezi la utendaji haki Ofisi ya Mashtaka inaungana na Mahakama ya Tanzania katika Ibara ya 107A, kwani Mahakama ya Tanzania ndiyo mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utaoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwenye Ibara ndogo ya 2 inasema katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia Sheria Mahakama zitafuata kanuni zilizoainishwa zikiwemo; kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi, kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi, kutoa fidia ipasavyo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine na kwa mujibu wa Sheria mahsusi iliyotungwa na Bunge, kukuza na kuendeleza usuluishi baina ya wanaohusika katika migogoro na kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.

Akiongezea alisema Ibara ya 107 B imeweka wazi kuwa katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki; Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia masharti ya Katiba na yale ya Sheria za nchi huku akibainisha kuwa viapo vya Majaji na Mahakimu wa ngazi zote ni kufanya kazi bila hofu katika kuamua, kutokua na huba, chuki wala upendeleo na kutakiwa kuviishi viapo hivyo kwani katika mnyororo wa haki jinai Wadau wote wanawajibika kushirikiana kwa pamoja.

Akitoa ushauri kwa Taasisi hizo za Haki Jinai, Jaji Mkuu Masaju alisema kuwa, ni vema wanapoweka mikakati wajue kinachopaswa kufanywa huku sambamba na hilo wakiimarisha upelelezi wenye umakini kwasababu hapawezi kuwa na mfumo wa haki unaobagua watu.

Jaji Mkuu alielekeza kuwa mwezi mmoja kuanzia leo (19/08/205) upande wa Mashtaka utalazimika kuwapa washtakiwa maelezo ya mashahidi. Alisema hili litaakisi matakwa ya kikatiba juu ya usawa wakati wa utendaji haki. Jaji Mkuu aliendelea kusema kuwa utatolewa utaratibu wa utoaji wa maelezo ya mashahidi wakati wa usikilizwaji wa hoja za awali yaani preliminary hearing ili kutokumfanya mshtakiwa kuwa gizani asijue ni ushahidi gani utaletwa na nani ataeleza nini wakati upande wa mashtaka tayari wana maelezo yake ya onyo.

Jaji Mkuu alibainisha faida ya zoezi hilo kuwa zitakuwa ni pamoja na; kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa gerezani, kutokuwepo kabisa kwa mahabusu wa mahakama za mwanzo isipokuwa kwa sababu maalum ambazo zinatambulika na kuboresha zaidi mnyororo wa utoaji haki kwa wote na katika ngazi zote muhimu.

Kuhusiana na kesi zinazosikilizwa na Mahakama Kuu, Jaji Mkuu alielekeza plea taking zisisubiri vikao (sessions). Amesisitiza mara baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuwa amesajili hati ya mashtaka na mwenendo kabidhi kufanyika kwenye Mahakama za chini, basi kesi hiyo ipangiwe kusikilizwa kwa mfumo wa cause list badala ya kusubiri vikao.Kuhusu Nolle Prosequi Jaji Mkuu alisema kifungu cha 92 cha CPA kimekuwa kikitumika vibaya. Wakati mwingine kesi zimeendeshwa hadi kufikia hatua ya hukumu halafu kesi inafutwa na upelelezi kwenda kufanyika tena. Alielekeza kifungu hiki kisomwe vizuri, kwani hakitoi nafasi ya kufanywa upelelezi zaidi. Alibainisha alipokuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kesi zilipokuwa zikifutwa kwa Nolle na kurudishwa tena alikuwa akiitisha jalada la zamani na kupitia maelezo ya mashahidi huku akilinganisha na ya kesi mpya iliyofunguliwa na alipokuwa akikuta kuna mambo yameongezeka alikuwa akizikataa kesi hizo mpya. Alishauri upelelezi ufanyike kwa umakini na kwa kina, na kama ushahidi hamna basi mshtakiwa aachiwe na sio kutumia kifungu hiki kufuta na kurudisha kesi upya huku mshtakiwa akiendelea kushikiliwa.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju akiwa kwenye mkutano wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.


Mkurungenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Bw. Sylvester Mwakitalu akitoa neno wakati wa ufunguzi wa wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifuatilia kwa makini ufunguzi wa mkutano wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju akifungua mkutano wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju akifungua mkutano wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju akifungua mkutano wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju akifungua mkutano wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.



Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifuatilia kwa makini ufunguzi wa mkutano wa utatu wa Taasisi za wadau wa haki Jinai leo tarehe 19 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma, kulia ni Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Ally Possi




Wadau wa Haki Jina wa Kikao Kazi cha Mwaka cha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Ofisi ya Mkurungenzi wa Upelelzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) na Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wakiwa kwenye picha ya pamoja ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju.

(Picha na INNOCENT KANSHA- Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni