Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Mhe. Elimo Massawe amewataka wanachama wa chama hicho Mkoa wa Pwani kukumbushana malengo makuu ya Mahakama katika kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza kwa njia ya mkutano mtandao (video conference) na wanachama wa TMJA Pwani katika kikao cha robo mwaka cha chama hicho kilichofanyika jana tarehe 15 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Gezat Park Bagamoyo mkoani Pwani, Mhe. Massawe alisema malengo makuu ya Mahakama ni kulinda uhuru wake, kuboresha uelewa wa sheria, kuimarisha maadili ya kazi na kuhakikisha huduma za haki zinapatikana mapema ipasavyo na kwa usawa na kwa wananchi wote.
“Hicho ni kiapo chetu na lengo la kuanzisha chama chetu” alisema Mhe. Massawe akiongeza kuwa, chama hicho kinakusudia kuwa na mfuko wa umoja wa uchumi kutoka katika michango ya wanachama ambapo Maafisa kutoka UTT watatoa elimu ya uwekezaji kwa wanachama kupitia Mfuko huo.
Rais huyo wa TMJA alisema kwamba, lengo kubwa ni kuwa na mfuko wa uchumi wa chama kutoka michango ya wanachama ambapo michango hiyo itakuwa ni gawiwo (share) na faida itakayopatikana katika uwekezaji huo itagawanywa kwa wanachama na asilimia kidogo itabaki kwenye mfuko ili kuendeleza chama.
Aidha, aliwapongeza wote waliokwishajiunga na mfuko wa Faraja na
kuwashawishi wale ambao bado hawajajiunga wafanye hivyo kwa haraka kwa sababu mfuko huo ni kwa ajili ya
wanachama wote kuwasaidia kuondoa msongo wa mawazo wanapopatwa na maafa ya
msiba na magonjwa.
“Niombe kila mmoja aone kwamba ana wajibu wa kujiunga na mfuko huu inaleta heshima sana pale ambapo kama Hakimu unapatwa na changamoto ya kufiwa au kuugua unapata huduma ya haraka itakayoendelea kujenga heshima yako wewe na jamii inayokuzunguka,” alisisitiza Mhe. Massawe.
Aidha, Mhe. Massawe aliwadokeza wanachama hao kuwa, tarehe 13 hadi 15
Januari, 2026 kutakuwa na Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania
(TMJA) hivyo, ametoa rai kwa wanachama
wote kuhudhuria mkutano huo.
Kwakuwa, Mkoa wa Pwani ndio wa kwanza kupata taarifa hiyo, aliwaomba wanachama hao wakatangaze kwa wanachama wengine wa Mikoa yote, kwakuwa mkutano huo utatoa hatma nyingi za Majaji na Mahakimu Tanzania.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Mkoa wa Pwani, Mhe. Aneth Senkoro aliwakaribisha wanachama hao na kuwaambia lengo la kusanyiko hilo ni kufanya kikao cha robo ya mwaka na pia kupata mafunzo ili kukumbushana wajibu wao lakini pia kufanya hafla fupi ya kuwaaga wenzao waliohama na kustaafu.
Mafunzo hayo yaliwezeshwa na Afisa Tehama wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Tumaini Malima ambaye alianza kwa kuwaasa na kuwasisitiza juu ya matumizi ya mtandao na kwamba taarifa zote zitumwe kwa barua pepe ili kuepuka matumizi ya karatasi.
Bw. Malima amemuomba Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi kuwatumia taarifa Mahakimu hao kwa njia ya matandao yaani barua pepe ili kuzoea matumizi ya mtandao.
Afisa TEHAMA huyo alitoa mafunzo kuhusu Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), Data Hub, Mahakama Mtandao na baruapepe, ambapo amesisitiza na kutoa rai kwa Mahakimu hao kuhakikisha wanaijua mifumo yote ya Mahakama maana kwa sasa Mhimili huo upo kidijitali, hivyo kuijua mifumo hiyo hakukwepeki.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi akisimamia mjadala baada ya mafunzo kuhusu washtakiwa kuruka dhamana alisema, Mahakama ya Mkoa Pwani inabidi wabuni mkakati na kuzungumza na Wakuu wa Vituo vya Polisi ili mashauri ya Mahakama za mwanzo yanapopelekwa mahakamani wahakikishe mashahidi wa pande zote mbili wapo ili mashauri yasikilizwe siku hiyo hiyo na kwamba hatua hiyo itaepusha malalamiko endapo mshtakiwa akijidhamini na kukimbia na kesi kusikilizwa upande mmoja.
Mhe. Mkhoi aliwataka Mahakimu Wakazi Wafawidhi wote wa Mahakama za Wilaya zilizopo mkoani humo kufuatilia mashauri yote yaliyopo katika vituo vyao kwa kufanya vikao kila Ijumaa ili kupitia changamoto zinazosababisha kuwa na mlundikano wa mashauri na pia kutohuisha mashauri kwenye mtandao.
Kadhalika aliwataka Mahakimu hao kukagua mfumo wa (e-CMS) kila mara na kuhakiki taarifa kama zipo sahihi kabla ya kuzituma badala ya kuwaachia Wasaidizi wa Kumbukumbu pekee.
Katika kikao hicho, Mwakilishi wa TMJA, Mhe. Vedasto Mwaria alitaja malengo makuu ya chama hicho kwamba, msingi mkuu wa chama hicho ni kutoa elimu kwa wanachama na jamii lakini pia kuangalia maslahi ya Majaji na Mahakimu.
Mhe. Mwaria aliongeza kuwa, chama hicho kinapaswa kuwa thabiti katika nyanja zote yaani katika usajili mapato na ushirikiano wake na vyama mbalimbali.
Sambamba na kikao na mafunzo hayo, kulikuwa pia na hafla ya kuwaaga Mahakimu waliohama na kustaafu akiwemo Mhe. Salum Ally Hamis ambaye amestaafu na wengine akiwemo Mhe. Herieth Mwailolo, Mhe. Fahamu Kibona, Mhe. Nicodemas Malowa, Mhe. Vulfrida Msele ambao wamehamishwa vituo vya kazi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuagwa, Hakimu Mkazi Mkuu Mstaafu, Mhe. Salum Ally Hamis ambaye kwa siku ya hiyo aliagwa kufuatia kustaafu utumishi wa umma, ambapo alisema, “Mahakama Mkoa wa Pwani imekuwa na utaratibu wa kuwaaga watumishi wanaohama na kustaafu ni utamaduni mzuri sana, mimi nimekuwa nikitoka na kurudi Pwani nimenufaika na utaratibu huu.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni