·
Ashauri majukumu ya Machifu kujumuishwa
pia kwenye Sheria ya TAMISEMI
·
Jaji Mkuu aunga mkono na kupongeza
kazi ya usuluhishi wa migogoro wanayofanya Machifu hao
·
Aunga mkono pendekezo la Machifu hao kuhusu
kuvunjwa kwa Mabaraza ya Ardhi
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju ametembelewa na Machifu wa Mikoa ya Kusini na kupata fursa ya kufanya nao mazungumzo ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Akizungumza na Machifu hao tarehe 16 Septemba, 2025, Jaji Mkuu aliwakaribisha na kusema kuwa pamoja na mambo mengine anatambua kazi nzuri wanayofanya Machifu ikiwa ni pamoja na kufanya usuluhishi huku akinukuu Biblia Takatifu, Kitabu cha Mathayo Sura ya 15:9 ambayo inasema, “Heri wapatanishi maana wataitwa wana wa Mungu,” na kueleza kuwa, Machifu wanafanya jambo jema la upatanishi kwa sababu Mungu anataka tuishi kwa amani na upatanisho.
“Niendelee kuwakaribisha, hii ni Taasisi ya umma ni moja ya hiyo Mihimili inayounda Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnapokuwa na jambo la kutushirikisha msisitize,” alisema Mhe. Masaju.
Mhe. Masaju alieleza kuwa watu wakipatana kunakuwa na amani na utulivu, watu wanapata fursa ya kushiriki shughuli za kuleta na kudumisha ustawi wa jamii katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
“Sisi lazima tuwaunge mkono katika jukumu hili kwa sababu lengo la Serikali siku zote ni ustawi wa wananchi kijamii, kisiasa na kiuchumi na mimi nawafananisha ninyi Viongozi wetu wa kijadi kama Viongozi pia wa kidini kwa sababu hili mnalolifanya na huo uhuru mmepewa,” alisema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju alieleza kuwa, Machifu wana mchango na jukumu kubwa la kudumisha maadili katika jamii na kwamba kila kabila lina maadili yake ambayo yatadumisha usalama wa jamii, umoja wa kitaifa na amani katika jamii.
“Ninyi ni watu wenye hekima na akili, mnajua ni yapi tukiyafanya yataleta mkanganyiko na haya ni mambo ya msingi sana kuzingatiwa na kila mmoja anayetekeleza majukumu haya, haya hayawahusu ninyi peke yenu yanatuhusu hata sisi viongozi Serikalini, kila mmoja ana jambo la msingi la kusisitiza hapa,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Kadhalika, Mhe. Masaju alirejea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ambayo pamoja na mambo mengine inazungumza juu ya utawala, amani, usalama na utulivu kuwa ndio msingi mkuu wa Dira hiyo na kusisitiza kwamba, Viongozi hao wa kijadi wana jukumu kubwa na la kuchangia masuala hayo kwa kuwa wanaishi na jamii na wanazijua mila na desturi za jamii husika, wana maadili ya msingi yanayowaongoza na kwamba wanayo nafasi kubwa zaidi ya kusikilizwa katika jamii.
“Ninyi mna historia, mna mazingira mazuri hata ya kusuluhisha migogoro ya ardhi kwa sababu mnajua eneo hili lilikuwa linakaliwa na ukoo fulani na mipaka yao inapoanzia na kuishia na kulikuwa na vitu fulani vilikuwa vinafanyika katika ardhi hii kwahiyo mpo katika nafasi nzuri ya kutatua hata migogoro mingine,” aliongeza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju alisema kuwa, kufuatia umuhimu wa Machifu katika Jamii ameshauri na kupendekeza juu ya kufanya Marekebisho ya Sheria ya Serikali za Mitaa ili shughuli za Machifu zijumuishwe katika sheria hiyo ili waweze kufanya majukumu ya kuhimiza maadili ya jamii, kuangalia na kuhimiza utunzaji wa mazingira, kuhimiza amani, usalama na utulivu katika jamii, mapambano dhidi ya rushwa pamoja na kuhimiza utumishi unaowajibika.
“Hapa mimi ndipo nakusudia kumshauri Mhe. Rais kwamba ile Sheria ya Serikali za Mitaa zile ambapo ndipo tunapoishi hapa tufanye mabadiliko muwe na majukumu pale, kuna mambo ambayo mtayafanya pale kwa mfano mkawa na jukumu la kuhimiza utunzaji wa mazingira yetu, misitu, vyanzo vya maji, kuhimiza maadili ya jamii, kuhimiza utumishi unaowajibika,” alieleza Mhe. Masaju.
Akizungumzia kuhusu moja ya pendekezo lililotolewa na Machifu hao kuhusu migogoro ya ardhi kwenda Mahakama za Mwanzo badala ya Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata, Jaji Mkuu ameunga mkono pendekezo hilo.
“Mmependekeza kwamba, zile kesi za migogoro ya ardhi badala ya kwenda kwenye Mabaraza ziende kwenye Mahakama za Mwanzo, huku sisi mahakamani tutamuandalia Mhe. Rais mapendekezo yetu kwamba Mabaraza yale yaondoke, kwa sababu kuna Taasisi kama Tume ya Taifa ya Kurekebisha Sheria imeshafanya utafiti ikasema haya Mabaraza hayo yaondoke kwa sababu hakuna rasilimali ya maana duniani kama ardhi,” alieleza Mhe. Masaju.
Aliongeza kuwa, suala la utatuzi wa migogoro inayohusiana na ardhi haliwezi kuachiwa mabaraza hayo ambayo yanafanya mambo yasiyo kwa sababu kwenye Sheria ya Ardhi inayatambua kama nayo ni Mahakama, hivyo yale mabaya ikiwemo rushwa yanayozungumzwa kuhusu Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inasema yanayofanyika ni kwenye Mabaraza ambayo kimsingi hayapo Mahakama.
“Mabaraza ya Kata yapo Ofisi ya TAMISEMI, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yapo Wizara ya Ardhi, halafu lawama za rushwa zinakuja kwetu Mahakama kwa sababu mashauri yanafika kwetu yameshaharibika kwa hiyo sisi tuko tayari kama Serikali inatambua sasa jukumu hilo lipelekwe kwenye Mhimili wa Mahakama, sisi huku tunao uwezo wa kiakili na wa kimiundombinu wa kusimamia utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa sababu sisi tuna Mahakama za Wilaya kila Wilaya isipokuwa Wilaya tatu kwa sasa ambazo pia zinajengwa na vilevile tuna Mahakama Kuu,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Kadhalika, Mhe. Masaju alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa Machifu hao kuhusu Polisi wanavyokiuka maadili ya utumishi wao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuunga mkono pendekezo la Polisi kubaki na jukumu la ukamataji pekee, kuendesha ibaki kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuhukumu ibaki kwa Mahakama.
“Tarehe 19 Agosti, 2025 nilifanya mkutano wa pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka, Mkurugenzi wa TAKUKURU, Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai lakini pia walikuwepo Wakurugenzi wa Vyombo kama hivyo kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, moja ya vitu nilivyosema ni kwamba ndani ya mwezi mmoja nitabadilisha zile kanuni ili kwamba hawa washtakiwa wanaoshtakiwa Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi nao wawe wanapewa ushahidi wa upande wa mashtaka kama vile wanaoshtakiwa Mahakama Kuu wanavyokuwa,” alieleza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju alibainisha kuwa, wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha hicho ili sasa Polisi kabla ya mtu kusomewa maelezo ya awali, Mahakama iwe na Ushahidi na wanaoshtakiwa wawe na huo Ushahidi akisisitiza kuwa hiyo ndio maana ya ‘fair trial’ ambayo ipo kwenye Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza wakati wa majadiliano hayo, naye Chifu Mkuu wa Wayao Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Maendeleo ya Akida Wabu (AWADEF), Chifu Saad Wabu Mussa Mitondo II amemshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuwapa fursa ya kuzungumza naye na kusema kuwa, hatua hiyo ni kubwa katika historia ya Tanzania kwa Machifu kuzungumza na Mkuu wa Mhimili wa Mahakama.
“Hii ni Bahati kubwa kuonana na Jaji Mkuu, kwangu mimi naona hii itaniongezea siku za kuishi kwa sababu kuonana na viongozi hawa baraka,” alisema Chifu Mitondo II.
Chifu huyo alieleza kuwa, katika jamii wanamoishi kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi ainayotokana na utendaji wa Mabaraza ya Kata na hivyo kupendekeza kuwa, migogoro ya ardhi iingizwe Mahakama za Mwanzo badala ya kushughulikiwa na Mabaraza hayo.
Kadhalika, Chifu Mitondo II alimuomba Jaji Mkuu kuwafikishia ombi lao kwa Viongozi wenzake juu ya kuwa na Sheria ya Utambuzi wa Machifu nchini ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru sambamba na kuwasilisha pendekezo la Polisi kupunguziwa majukumu badala yake waishie kukamata pekee na jukumu la kuendesha mashauri libaki kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuhukumu ibaki Mahakama.
Akizungumzia kuhusu madhumuni ya ujio wao kwa Jaji Mkuu, Mwenyekiti huyo wa AWADEF alieleza kwamba ni pamoja na kufanya mazungumzo ya kubadilishana Mawazo, kushauriana kuhusu utendaji wa Mahakama na pia kushirikisha kuhusu maandalizi ya Semina ya kuwajengea uwezo Machifu wa Mikoa ya Kusini inayotarajiwa kufanyika mkoani Mbeya Oktoba, 2025.
“Dhumuni la kukutembelea hapa leo pia sisi Machifu wa Mikoa ya Kusini chini ya uratibu wa Shirika la Maendeleo la Akida Wabu ni kukushirikisha maandalizi ya Semina ya kuwajengea uwezo Machifu wa Mikoa hiyo, hivyo tunaomba ushiriki wa Mahakama katika kutoa elimu katika semina hiyo ili Machifu waweze kuwa na uelewa wa Mahakama hatimaye waendelee kuwa Mabalozi wa Mhimili huu,” alisema Chifu Mitondo II.
Kwa upande wake Afisa Itifaki aliyeambatana na Machifu hao, Bi. Leila Bhanji alisema Machifu ni Tunu ya jamii na Taifa kwa ujumla katika suala zima la kusimamia maadili, kushiriki katika malezi ya Watoto na kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali, hivyo alimuomba Jaji Mkuu kuwapa Machifu hao Dira ya Mahakama ili waweze kuwa Mabalozi wazuri wa Mhimili huo.
Jaji Mkuu amewahakikishia Machifu hao kuwa, Mahakama itashiriki kikamilifu kwa kuwatuma Maafisa katika Semina yao inayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu ili washiriki kutoa elimu kwao na kwamba utoaji wa elimu utakuwa endelevu ambapo aliekeza kuwa, Machifu hao wawe sehemu ya makundi ya wanaopatiwa nakala za Majarida ya Mahakama ‘Haki Bulletin’ ili wasome na kufahamu taratibu mbalimbali za Mahakama na vilevile washirikishwe katika matukio mbalimbali ya Mahakama.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju pamoja na baadhi ya Machifu kutoka Mikoa ya Kusini wakifanya dua kabla ya kuanza mazungumzo walipomtembelea ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania tarehe 16 Septemba, 2025.
Wakiwa katika nyuso za furaha baada ya kupatiwa majarida ya Mahakama. Katikati ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija, wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, wa pili kulia ni Chifu Mkuu wa Wayao Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Maendeleo ya Akida Wabu (AWADEF), Chifu Saad Wabu Mussa Mitondo II na wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Maendeleo ya Akida Wabu (AWADEF), Prince Ibrahim Samata.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni